KANISA KATOLIKI LAOMBA MSAMAHA MAUAJI YA KIMBARI RWANDA


Baba Mtakatifu Fransisko, Jumatatu tarehe 20 Machi 2017 amekutana na kuzungumza na  Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wamepongeza uhusiano wa dhati kati ya Vatican na Rwanda. Kwa pamoja wameridhika na mchakato wa utulivu katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini Rwanda.
Ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa, umesaidia kukoleza upatanisho wa kitaifa na hivyo kuimarisha amani kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya taifa zima! Katika mazingumzo yao, Baba Mtakatifu Fransisko ameonesha kusikitishwa kwake na mauaji ya kimbari yaliyofanyika nchini Rwanda dhidi ya Watutsi na kuonesha mshikamano wake wa dhati na wahanga wa mauaji haya ambao bado wanaendelea kuteseka kutokana na athari zake.
Baba Mtakatifu akiwa ameungana na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka elfu mbili ya Ukristo aliposali kwa ajili ya kuomba msamaha, Papa Fransisko pia amerudia sala hii kwa ajili ya wakleri, watawa na waamini walei waliojihusisha na mauaji ya kimbari kiasi cha kusaliti utume wa Kiinjili. Kwa kutambua makosa yaliyotendwa na watoto wa Kanisa ambayo yamelichafua Kanisa, kwa unyenyekevu mkubwa, sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, anaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda kuomba utakaso wa kumbu kumbu ili kuendeleza matumaini na Imani iliyopyaishwa, ili kudumisha amani na kushuhudia kwamba inawezekana kushirikiana kwa dhati, ikiwa kama utu wa ninadamu na mafao yake msingi yanapewa kipaumbele cha kwanza. Mwishoni, Baba Mtakatifu Fransisko na Rais Paul Kagame wa Rwanda wamegusia masuala ya kisiasa na kijamii Kikanda hasa zaidi katika maeneo ambayo yameathirika kwa vita na majanga asilia. Wamesema kuna idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaohitaji msaada wa dharura kutoka kwenye Jumuiya ya Kimataifa na Mashirika ya Misaada Kikanda.
Kwa msaada wa:
Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI