Kwaresima dira ya muelekeo wa maisha yetu
KUNA mambo mbalimbali ya kufanya katika kipindi cha Kwaresima. Kwanza sadaka, sala na kufunga. Sadaka inaweza kuwa pesa, sadaka inaweza kuwa kujitolea kwa jili ya wengine, sadaka inaweza kuwa kuwasadia wazazi na wasiojiweza katika shughuli mbalimbali. Sadaka ni pamoja na kufanya kazi katika muda wa ziada bila malipo.
Na katika sala tunafundishwa ama tunakumbushwa kusali na Baba
aliye sirini ndani ya mioyo yetu. Siyo kupayuka. Pia tukisali tusisali kwa jili
yetu tu, bali pia kwa jili ya watu wengine. Tusali kwa ajili ya wagonjwa.Tusali
kwa ajili ya watu wanaoteseka kwa namna mbalimbali, hali kadhalika tusali kwa ajili
ya kuliombea taifa letu na ulimwengu mzima.
Ikiwa ulikuwa na bomba la mdomo linalotoa matusi, dharau,
majivuno, wivu, uwongo hivyo kwa sasa vinatakiwa vitiwe korokoroni yaani
visiwepo katika kipindi cha Kwaresima. Ni bora ule kanda, ugali, pilipili
ushibe lakini usitende dhambi kuliko kuacha kula kwa kigezo cha kufunga, lakini
ikifika usiku unafanya ulozi, unatukana, una dharau wengine, unawasemea wengine
uwongo, hutoi sadaka, husali huko si kufunga bali ni kujidanganya.
Tena, ukifunga usifanye matangazo mbele ya watu wa ulimwengu, bali
iwe siri yako na Baba yako wa mbinguni. Nakumbuka andiko lililoandikwa na
mwandishi mmoja wa gazeti hili. Aliandika habari ya Mhindi kijana
mwanamapinduzi namna alivyokuwa akimwomba Mungu kwa sala.
Mhindi huyo angali kijana mwanamapinduzi anatajwa wakati akiwa
kijana alimwomba Mungu ''Mungu nipe nguvu ya kubadili dunia'' hata hivyo
hakufanikiwa, na baadaye akamwomba Mungu akiwa na miaka 40 kwa kusali hivi
''Mungu nipe neema ya kuwabadili wale ninaokutana nao''. Kweli akabadili wana
familia na marafiki zake na akajisikia vizuri.
Sasa ni mzee anaanza kuona madhaifu yake sasa sala yake ipo hivi:
''Mungu nipe neema ya kubadilika'' kisha akasema angesali hivyo asingepotea
katika maisha. Kwaresima ni uhalisia wa maisha yetu. Ni kipindi cha toba kwa
kutafakari matendo makuu ya Mungu.
Katika kipindi hiki tunakumbuka mengi kuhusu huduma ya Yesu Kristo
katika Miji mbalimbali ukiwemo Mkoa wa Yudea.Yesu alijaribiwa na Shetani 'eti'
ampe miliki ya utajiri wa dunia na aachane na kazi anayoifanya. Lengo lake
shetani alitaka awe mtawala kuliko Mungu. Unajiuliza huyu shetani utajiri huo
aliumba yeye mpaka anataka kummilikisha Yesu?.Anajua hati ya miliki hizo
ilipo?,anajua hizo hati zilitolewa na Manispaa gani huko Mbinguni?.
Yesu alishinda majaribu. Je, sisi tunaishi katika misingi ya
kushinda majaribu katika maisha yetu ya kila siku?, je tukijaribiwa tunafanya
nini au mawazo yetu yanaelekezwa wapi kutafuta ufumbuzi wa majaribu?.Mfano wa
huyo Mhindi unaakisi kipindi cha Kwaresima, kwamba mabadiliko huanza na wewe,
kisha jirani na baadaye ulimwengu mzima (changes begin with you, and begin in
your mind; mabadiliko yanaanza na wewe, na yanaanza katika akili yako).
Mara nyingi watu wa ulimwengu hutazamia kuwabadilisha wengine ili hali
wao wenyewe hawajabadilika. Hivi fisadi anaweza kumbadilisha fisadi mwenzake. Yesu
Kristo wakati anahubiri Injili alikutana na vikwanzo vingi. Huduma ya Yesu
haikuwa ya lelemama kama ambavyo wafausi wa kweli wa kristo wanavyoteswa katika
nchi ambazo hazitaki kusikia habari ya Injili.
Kazi ya Yesu haijakamilika, kwani hata yeye alingia kwenye falme
ambazo hazikutaka kusikia habari za Injili. Aliwindwa kwa tabasamu kwa nia
mbaya. Lakini alitimiza majukumu yake kwa unyenyekevu. Ulimi wake ulimlinda
hata hukumu yake kwa Pilato haikuwa na nguvu, ingawa naye Pilato kwa sababu ya
uwogo wa umati wa watu uliomtaka Yesu asulubiwe, aliamua kutimiza matakwa ya
wajinga walio wengi.
Hiyo ilikuwa michezo michafu dhidi ya Yesu ukiachilia mbali rushwa
aliyoipokea Yuda ili amsaliti Yesu, ingawa Yuda alijutia kile alichofanya. Je,
ni watu wangapi leo hii wakikosa wanajutia makosa yao nakuwa tayari kuacha
dhambi?.Je, kuna ubaya gani katika Injili?. Yesu Kristo katika mafundisho yake
anasimamia haki.
Haki ya kuchanganyika na wenye dhambi, pia anasimama ukweli dhidi
ya yule mwanamke waliotaka kumuuwa kwa kupiga mawe, lakini wale wauwaji
walipotakiwa kujibu swali la Yesu dhidi ya yule mwanamke walikimbia.Je,
tunajifunza nini juu ya hukumu dhidi ya wengine?.
Injili inahimiza upendo, huruma, msamaha, amani, maridhiano, je,
ni wapi katika maandiko ya Injili yanahimiza watu wauane ama wasipendane. Kwaresima
inaakisi maisha yetu na maisha ya Yesu. Yeye alidharauliwa, alikatishwa tamaa
lakini alisonga mbele. Kuanguka kwake Yesu na msalaba, kisha kuinuka kwake ni
utambulisho wa mkristo kusonga mbele mpaka neno la Mungu litimie.
Maisha yetu yanazongwa na aina hiyo ya maisha aliyoishi Yesu. Tunapoanguka
tunahimizwa kusimama na kusonga mbele hadi mwisho wa maono yetu. "Nyiyi ni
chumvi katika dunia, hivyo chumvi ikikosa ladha itawezaje kutumika? ni sawa na
uzuri pasipo faida bali hutupwa na kukanyagwa na miguu ya wanadamu.
Ninyi ni mwanga katika dunia, mji ulioinuliwa kilimani kamwe
haufichiki. Wala taa haiwashwi halafu ikafunikwa ndani ya kikapu, bali
huinuliwa katika ngazi yake na hutoa mwanga kwa watu wote walio ndani ya
nyumba. Mwanga wenu ung'are kwa watu wote ili waone mema yenu wamtukuze Mungu
aliye mbinguni"
Hayo ni maneno Matakatifu. Mafunzo hayo yalikuwa muhimu sana kwa
wanafunzi wake pia ni muhimu sana kwetu hivi leo. Maelezo fulani yanaeleza kuwa
katika miaka ya nyuma chumvi ilitumika kutunza vyakula kama nyama na samaki ili
isiharibike, chumvi ilikua muhimu kama ilivyo friji katika miaka hii....
Hapa Kristo anatufundisha maisha yetu kama wanafunzi wake
yanapaswa kuwa ya mfano na ushawishi kwa jamii ili jamii ipokee ufalme wa
mbingu. Ufalme wa mbingu ni mema yote ya Mungu. Chumvi huleta mabadiliko,
hubadili ladha ya chakula mara tu inapochanganyika katika chakula husika, hivyo
nasi pia tukiwa wakristo maisha yetu yanapaswa kuleta mabadiliko.
Chumvi ina ladha,ikiingia katika chakula kinakuwa na ladha. Hapa
Kristo anatufundisha kwamba pamoja na tamaa, chuki, wivu, uchoyo, usaliti, mapigano
na hata mauaji yaliyoenea katika jamii ya sasa tukimruhusu Roho Mtakatifu aishi
maisha ya Kristo kupitia sisi, jamii itakuwa na ladha kama yetu sisi ambao ni
chumvi.
Chumvi huleta kiu, tazama maisha katika jamii zetu kila mtu
anahamaki, kuteseka na kutapatapa na mizigo ya dhambi iwe ni rushwa, tamaa, anasa,
pombe na dawa za kulevya ilimradi ni dhambi lazima inamtesa. Hivyo sisi
tuliompokea Yesu Kristo kwa ubatizo, kipaimara, ndoa na kukataa maisha ya kuoa
kwa ajili ya kuelekeza nguvu ya utumishi wa ki-Mungu, sharti tuchochee furaha,
amani kwa watu walioko katika gereza la dhambi nao watubu dhambi zao na
kumpokea Yesu.
Chumvi huenea, na ni wazi kwamba chumvi kidogo sana inaweza kuleta
ladha katika chungu kikubwa hivyo ndivyo Injili hufanya kazi. Habari za Yesu
zilianza na kikundi kidogo tu cha watu na kuenea dunia nzima. Hivyo na sisi tusife
moyo kuishi maisha katika Bwana tukiamini kuwa kazi yetu ni kubwa na mwisho
wake ni wokovu. Wapo watu ambao hufikiria imani za wengine ni upuuzi, na kwamba
wao imani zao ni sahihi. Watu hao sharti waulizwe ikiwa hawana upendo kwa
wengine imani yao yatoka wapi?.
Wapendwa wote wa Mungu, tunayo sababu ya kutambua kipindi cha
Kwaresima ni kipindi kinachoweka wazi maisha yetu ya ulimwengu, na
tunafundishwa aina ya ulimwengu tunamoishi.Yesu Kristo katika ukamilisho wake
wa neno la Mungu aliishi katikati ya watu wa mataifa mbalimbali, mikoa, miji na
wafalme wenye nguvu na waliotumia madaraka yao vibaya kuwangamiza wengine.
Ni wivu tu.Wivu ni roho mbaya inayomwingia mtu na kumfanya asifurahie
mafanikio ya kubarikiwa kwa watu wengine. Ni ile hali ya kuwa na “kijicho”
yaani hali ya kutafuta namna yoyote ile ya kuzima mafanikio ama baraka za mtu
mwingine.
Shetani anaona wivu kwa nini tuna afya njema, kwa nini
tumebarikiwa, kwa nini tuna furaha. Wivu dhidi ya Yesu ilikuwa ni sababu ya
kuteswa kwake na kufa msalabani hata yule nyoka wa bustanini aliyefanya
udanganyifu aliona wivu dhidi ya maisha ya Adamu na Eva akaamua kuwaharibia.
Mungu atupe nguvu ya kuyashinda majaribu. Kwaresima iwe njema na
yenye kuleta mabadiliko kuanzia ndani ya mioyo yetu, akili zetu na hatimaye
mabadiliko hayo mema yawe chumvi ya ulimwengu.
Na Brown Sunza
Comments
Post a Comment