TANZIA: BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA LAMPOTEZA MKUU WA IDARA YA UCHUNGAJI


 
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC linasikitika kutangaza kifo cha Mkuu wa Idara ya Uchungaji Barazani hapo Padri Gallus Thomas Marandu kilichotokea tarehe 26 Machi mchana saa 6.30.

Marehemu alianza kusumbuliwa na tumbo akiwa nchini Ethiopia hivi karibuni katika semina ya uchungaji iliyoandaliwa na Umoja wa wanachama Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki AMECEA. Alipata matibabu kabla ya hali kubadilika ghafla siku ya jumapili(Machi 26) ambapo alikimbizwa hospitali ya Temeke, hata hivyo jitihada za kuokoa uhai wake zilishindikana. 

Akiongea na blogu hii, Katibu Mkuu wa TEC Padri Raymond Saba amesema Baraza na Kanisa Katoliki limesikitishwa sana na msiba huo kwani marehemu alikuwa muadilifu mwenye ari kubwa ya utendaji kazi lakini alikuwa kiungo kikubwa katika kamisheni ya wahamiaji na wasafiri kazi aliyoifanya kwa mafanikio makubwa.

"Taratibu za awali ni kuwa marehemu ataagwa hapa TEC siku ya Jumatano mchana majira ya saa 6 kabla ya kuanza safari ya kwenda kumpumzisha huko Arusha Njiro," amesema Katibu Mkuu

TEC imetoa pole kwa wanafamilia wote  na shirika la Roho Mtakatifu "Holly Ghost Fathers."

Padri Gallus Marandu alizaliwa tarehe 26/9/1956 huko Rombo Moshi, aliweka nadhiri mwaka 1982 kisha akapata daraja la Upadri mwaka 1986. Alianza utumishi TEC mwaka 2001 kama katibu wa tume ya mahusiano baina ya dini mbalimbali, 2005 akahudumu katika kamisheni ya wahamiaji na wasafiri pia utamaduni na mwaka 2013 akawa msaidizi wa Katibu Mkuu pia akisimamia idara ya Uchungaji.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi AMINA.
 







 

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU