Siku ya Wanawake Duniani,Kitaifa kufanyika kila baada ya miaka mitano
KILA mwaka
Machi 8, Watanzania wataungana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, katika
kuadhimiasha Siku ya Wanawake Duniani lakini Serikali ya Tanzania imesema
sherehe hizo kitaifa zitafanyika kila baada ya miaka mitano.
Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Sihaba Nkinga, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Wizara
hiyo iliyoko Chuo Kikuu cha Dodoma ilisema kuwa,
Maadhimisho hayo kwa mwaka huu
yatafanyika katika ngazi ya mkoa kufuatia uamuzi wa Serikali wa mwaka 2005 kuwa
yatakuwa yanafanyika kitaifa kila baada ya miaka mitano.
"Uamuzi wa kuadhimisha siku hii
kitaifa kila baada ya miaka mitano,
ulikusudia kutoa nafasi kwa Serikali yenyewe na wadau wengine kuweza
kupima mafanikio ya shughuli za maendeleo ya wanawake, changamoto zilizoko na
kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo", alisema.
Katibu Mkuu amesema, Kaulimbiu ya Siku
ya Wanawake Duniani kitaifa kwa mwaka 2017 inasema ‘Tanzania ya Viwanda; Wanawake ni Msingi wa
Mabadiliko ya Kiuchumi.’ Kaulimbiu hii inasisitiza kuwajengea wanawake uwezo wa kitaaluma, kibiashara,
upatikanaji wa mitaji, masoko na mikopo ili waweze kushiriki kwa usawa, na
kunufaika na fursa zilizopo badala ya kuwa wasindikizaji tu.
Dhamira ya Kaulimbiu ya ‘Tanzania ya Viwanda; Wanawake ni Msingi wa
Mabadiliko ya Kiuchumi’ inalenga kuhamasisha jamii na wadau wote nchini
kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake ili kuwawezesha kushiriki na kunufaika
na fursa za maendeleo katika kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi
wa viwanda.
Kaulimbiu hii imetoholewa kutokana na Kauli Mbiu ya
Umoja wa Mataifa inayosema ‘Women Economic Empowerment in the Changing World of
Work’ ambayo kwa tafsiri ya Kiswahili ni ‘Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Katika
Dunia ya Mabadiliko ya Kazi.’
Kaulimbiu ya Umoja wa Mataifa inalenga
kuzihamasisha Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwawezesha wanawake kiuchumi
ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika sekta za
umma na binafsi.
Kaulimbiu
ya Kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani
ya mwaka huu imeandaliwa kwa kuzingatia Mazingira ya Nchi yetu;
vipaumbele vya kimaendeleo na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya
kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati.
Comments
Post a Comment