Mitandao isiwalevye

ASKOFU wa Jimbo Katoliki Mpanda Mhashamu Gervasi Nyaisonga amekiri kutoridhishwa na namna vijana wanavyoongozwa na ajenda za mitandao ya kijamii ambayo inakuwa ni ya mihemko zaidi badala ya kufikiri namna ya kutatua changamoto zinazowakabili ambazo zipo ndani ya uwezo wao.
Akizungumza na gazeti Kiongozi kuhusu ajenda mbalimbali zinazojadiliwa kwenye mitandao ya kijamii amesema vijana wanajikita zaidi kujadili siasa ama wanasiasa badala ya masuala ya maendeleo ambayo alisema ni kupoteza muda.
“Kijana anaweza kutumia fursa ya akili yake, nguvu yake na sehemu anayoishi kuwa mbunifu wa kazi zinazomuongezea kipato lakini hawezi kupambana na mambo ambayo hawezi kuyatolea maamuzi,” Askofu Nyaisonga amesema na kuongeza.
“Kijana anashinda kwenye mitandao akilalamikia polisi, waziri, serikali nk, huko ni kupoteza muda kwani hawezi kubadilisha chochote. Mitandao ya kijamii imekuwa bangi ya kutuliza maumivu ya changamoto za vijana. Jambo hilo si sahihi kwani hata yule anayejadili ama kuandika jambo kwenye mitandao hiyo, hana uhakika na anachokisema, hakijui wala hakielewi vizuri.”
Amesema vijana wengine wanatumiwa na wanasiasa kuweka ajenda za kumjadili mtu mmoja ama wawili kwa maslahi yao binafsi na kusema huo ni uvivu wa kufikiri na kufanya maamuzi.
“Uvivu unawasababisha vijana kulalamika kila kukicha badala ya kutafuta mbinu mbadala za kujibu changamoto zao. Utakuta kwenye vijiji vyetu ama mitaa yetu watu wa nje wanakuja wanatumia fursa wanaendelea kiuchumi baadaye wanaondoka na kutuacha tukilalamika.”
Amewataka vijana wasipoteze muda kwa masuala ambayo hawawezi kuyafanyia maamuzi bali watumie muda mwingi kwa mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wao.
“Kataeni ajenda za mitandao ambazo zinawekwa na wanasiasa ama vijana wanaotumiwa na wanasiasa kwasababu ya masilahi binafsi. Mabadiliko yatoke ndani ya mtu. Msihamishe wajibu wenu kwa mtu mwingine. Imefika mahali wajibu wenu mnamtwisha mtu mwingine kwenye mabega wakati hawezi kuwasaidia,” amesisitiza.
Amewataka vijana kuwa wabunifu katika kutenda, kufikiri na kufanya maamuzi kwani kwa sasa katika jamii utaona kijana anakimbilia gari ili alidandie lakini hawazi kujifunza kuendesha gari.
Aidha amesisitiza kuwa vijana wengi wana utajiri mwingi na akili zao ni kama mgodi wa madini wenye utajiri mkubwa lakini hawajui thamani yake mpaka mtu aje achimbe achukue madini na kuacha mashimo tu ndipo washtuke.
“Msikubali kutumiwa na wanasiasa ama wafanya biashara mkakosa dira ya maisha. Wenzenu wanawatumia ili wapate faida halafu wawaache kama kisiwa kilichotengwa. Muda ndio huu wa kubadilika.”
Amewasisitiza kuwa na mang’amuzi sahihi ya maisha ikiwemo kujitambua huku akimnukuu Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela ambaye alikuwa anatambua wajibu wake binafsi kama baba wa familia na Rais wa nchi.
“Hayati Mandela aliwahi kusema; ‘Ninatambua kuwa nina wajibu wa kuilea familia yangu na wajibu wa kuwatumikia wananchi kama rais wa nchi. Nitajitahidi kuwa baba mwema wa familia na rais mwaminifu kwa watu wangu, lakini pale nitakapokabiliwa na changamoto kwa vile familia yangu ni sehemu ya serikali basi nitafanya yale ya nchi kwanza kwani mke na watoto wangu ni wananchi pia wa Afrika Kusini’: Mandela alijitambua (self awareness) na ndicho kilichompatia mafanikio makubwa ya kujituma na kutimiza wajibu.” Amesema Askofu Nyaisonga.
Ametoa suluhu ya changamoto hizo akisema kwanza vijana watumie mitandao ya kijamii kujadili ajenda zinazojenga na si watu. Taifa, dini mbalimbali pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kuweka mikakati ya kuandaa semina kwa ajili ya vijana (capacity building) kwa ajili ya kuwafundisha namna ya kujitambua.
“Tatizo vijana wengi hawapo sahihi kwa namna wanavyofikiri na kutenda, lakini hawajitambui kwamba hawapo sahihi na wakielezwa wanaona kama wanakosewa haki. Ila ni lazima tuwekeze kwa vijana, pia watumie majukwaa yao kwenye mitandao kujadili masuala mbalimbali yanayojibu maswali yao.
Kanisa hususani Katoliki, liweke utaratibu wa namna ya kuwaleta karibu vijana hawa pamoja na viongozi wao wa dini ili waelimishwe, wapewe motisha na miongozo ya maisha. Wasitengwe na kuachiwa huru pindi wanapopata sakramenti ya kipaimara.”
“Mwezi huu kuanzia tarehe 8-12 tulikuwa Arusha kwa ajili ya kushiriki Siku ya Vijana wa Skauti Afrika. Siku hiyo ni muhimu kwa vijana kwani inawakutanisha vijana wote waafrika kutoka nchi mbalimbali ili kubadilishana uzoefu na namna ya kutenda. Lakini cha kushangaza nilikuwa mimi na mapadri wawili wa Jimbo Katoliki Bukoba pamoja na baadhi ya vijana.
Siku ya kufungua alikuwepo mkuu wa wilaya na siku ya kufunga alikuwepo waziri wa elimu aliyefunga kongamano hilo. Binafsi sikufurahia nchi yetu ya Tanzania kwa kutoithamini siku hiyo muhimu kwa vijana.
Tulikuwa wachache mno kiasi kinachoonesha kuwa hatutilii manani makongamano ya vijana. Hatushiriki majumuiko yao ambapo mababa wa kiroho ni wajibu wetu kukaa na vijana, kuwasikiliza, kujibu maswali yao na kuwaimarisha kiimani.
Ninakumbuka siku kama hiyo mwaka jana tulifanyia Ghana. Ushiriki wa serikali ulikuwa mkubwa, walialika mabalozi kutoka nchi mbalimbali kushiriki, mawaziri, wabunge, viongozi wa dini na wengine walishiriki kwa heshima kubwa.
Hivyo ninaiasa jamii tuwasaidie vijana kwa hali na mali ili waweze kufikiri na kutenda vizuri kwa kusudi la kuleta mendeleo katika jamii,” ameeleza Askofu Nyaisonga.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI