“Kufunga siyo fasheni” Askofu Mkude
ASKOFU wa Jimbo
Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude amewaasa waamini kuachana na matendo
maovu katika kipindi hiki cha Kwaresma na badala yake wajitahidi kufanya mema yanayompendeza
Mwenyezi Mungu kwa uthabiti wa moyo na nia njema.
Askofu Mkude
amesema hayo katika waraka wake maalumu wa kichungaji katika kipindi cha
Kwaresma akiwahimiza waamini kujitoa sadaka kwa kufunga na kuwasaidia wengine
wenye shida mbalimbali kwa lengo la kuwaonjesha upendo ambao waliukosa.
Aidha Askofu
Mkude amesema kuwa Kwaresma ni kipindi cha kusali, kusoma na kulitafakari
neno la Mungu, pia kulitangaza kwa wengine ambapo kwa kufanya hivyo kutasaidia
kusimamia misingi ya imani ya Kanisa Katoliki.
“Ni kipindi cha
kusali zaidi, kutafakari, kusikiliza na kusoma vitabu mbalimbali ili tuwe na
uelewa mpana zaidi, pia kulitangaza kwa wengine ili kuwaangazia nao wamjue
Mungu, wampende na kumtumikia na kwa kufanya hivyo kutasaidia kusimamia misingi
ya imani yetu vyema,” amesema Askofu Mkude.
Pamoja na hayo
Askofu Mkude ameongeza kuwa wapo baadhi ya watu ambao wanaishi maisha ya shida,
hivyo kipindi cha Kwaresma ni muda muafaka wa kuwatazama wao ambao wanahangaika
kwa kukosa chakula na mahitaji mengine ya msingi.
“Kuna baadhi ya
watu wanaishi katika maisha ya shida, hivyo kipindi hiki cha Kwaresma uwe ni
muda muafaka wa kuwatazama wenye shida na wanaohangaika kwa kukosa chakula na
mahitaji mengine ya msingi na usifunge ili uhifadhi kiwe kingi badaye utumie
mwenyewe, hapo utakuwa unajidanganya,” amesema Askofu Mkude.
Hata hivyo ameeleza
kuwa mtu yeyote anayepaswa kufunga ni yule ambaye anajitoa kwa moyo kufunga kwa
nia njema na wala si kufunga kwa sababu ya kukosa chakula, bali kufunga ni kujikatalia
kwa malengo ya kuwasaidia wahitaji.
“Mtu anayepaswa
kufunga ni yule ambaye amejitoa kwa moyo kufunga kwa nia njema na si kwa kukosa
chakula bali kufunga ni kujikataa kwa malengo ya kuhifadhi na kuwasaidia
wahitaji kwa mavazi, chakula na mahitaji mengine muhimu, hivyo tutumie vizuri
kipindi hiki kwa kujisafishia njia kwa kutubu pia,” amesema Askofu Mkude.
Comments
Post a Comment