‘Huwezi kutenganisha ukombozi wa Tanzania na Ukristo’

IMEELEZWA kuwa ujio wa wamisionari wa kwanza Tanzania Bara ndiyo ulikuwa mwanzo wa safari ya ukombozi na mapinduzi katika nyanja za elimu, afya na fikra nchini Tanzania.
Hayo yamebainishwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Same Mhashamu Rogath Kimaryo katika Misa Takatifu ya uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji na elimu Bagamoyo, ambapo amesema kuwa licha ya kufanya kazi za uinjilishaji hapa nchini wamisionari ndiyo waliokuwa chimbuko la wasomi wa kwanza nchini.
Askofu Kimaryo ameeleza kuwa nguvu hiyo ya Kanisa Katoliki nchini katika kuhudumia jamii bila ubaguzi ndiyo chimbuko la mafanikio ya utume wake hapa nchini.
“Wamisionari walipofika Bagamoyo waliwakomboa watumwa, wakawaweka katika kijiji huru cha Mariani (Marian Village), hapo wakafungua shule wakaanza kuwafundisha watumwa hao kusoma. Wasomi wa kwanza Tanzania walikuwa ni hawa watumwa waliokombolewa Bagamoyo mwaka 1868” ameeleza Askofu Kimaryo.
Ameongeza kuwa kazi hiyo kubwa iliyofanywa na wamisionari wa kwanza ndiyo inayoendelezwa hata hivi leo, huku akibainisha kuwa uwepo wa shule nyingi zinazoendeshwa na kumilikiwa na kanisa Katoliki nchini ni chachu katika kuelimisha taifa.
“Kanisa siyo tajiri. Kanisa linaratibisha vitu vizuri tena kwa majitoleo makubwa. Umisionari ni unyenyekevu, ndivyo Kanisa linavyofanya kazi yake; kwa unyenyekevu, bila majivuno huku likiruhusu mpango wa Mungu” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Askofu Kimaryo ambaye aliongoza Misa hiyo ya uzinduzi wa jubilee, ameonya kuwa ni lazima watanzania watunze maeneo ya kihistoria na kuwataka wanasiasa wasisababishe kupotea kwa historia hiyo.
Ametahadharisha kuwa Bandari ya Bagamoyo ni ya kihistoria na inapaswa ibaki kama sehemu ya historia, na endapo kuna aina yoyote ya upanuzi litafutwe eneo pembeni yake ili eneo hilo libaki katika kumbumbuku ya historia.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude amewataka waamini wa Bagamoyo kuongeza kasi ya kutafuta utakatifu hasa katika kipindi hiki cha mwaka wa jubilei. Ametoa rai kwa wazazi kuwa mfano wa kuigwa katika malezi ya watoto wao kwa kuishi na kuwafundisha katekesi.
“Wazazi ishini kwa mfano ili watoto waige na wajifunze sala kutoka kwenu. Tusingoje watoto wafike darasa la pili ndipo tuanze kuwafundisha katekesi, elimu inaanza mapema lakini katekesi ianze mapema zaidi. Kila mmoja atimize wajibu wake, pamoja na Kristo tutafanikisha” ameeleza.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU