Askofu Anyolo- Wasaidieni waamini kuzielewa nyaraka za Kanisa
MWENYEKITI
wa Idara Uchungaji Umoja wa Wanachama Mabaraza ya Maaskofu Afrika
Mashariki AMECEA Askofu Philip Anyolo,
amewataka waratibu wa Idara za Kichungaji nchi wanachama wa AMECEA kuwa makini
na kukuza mshikamano katika kukabiliana na changamoto zao za kikanda hasa
kuwafafanulia waamini nyaraka mbalimbali za Kanisa.
Askofu Anyolo amesema hayo wakati wa
warsha ya siku nne juu ya uratibu madhubuti wa rasilimali fedha na watu pamoja
na namna ya kuandika miradi iliyofanyika katika Baraza la Maaskofu Katoliki
Ethiopia-Addis Ababa (CBCCE) .
Askofu Philip amewataka washiriki
kupendekeza miongozo ya kina juu ya majukumu na wajibu wa waratibu wa Uchungaji
na kutafakari juu ya matokeo ya nyaraka za
Kitume ikiwemo "Amoris Laetitia" (Furaha ya upendo juu ya
familia iliyoandikwa na Papa Fransisko), katika Kanisa na nhi za AMECEA.
Kutafakari na kutafsiri nyaraka hizi
namna zinavyoweza kusaidia huduma za Kichungaji katika ngazi ya AMECEA,
Kitaifa, Jimbo, Jumuiya hadi familia.
“Papa Fransisko ametoa nyaraka muhimu
za familia, mazingira na mengineyo. Nyaraka hizi zina maana na ni muhimu kwa
kila mkristo mkatoliki. Ndiyo maana inafaa kushirikiana na ofisi za mawasiliano
katika kutafsiri na kuzisambaza kwa waamini. Pia kupata tafsiri halisi kutoka
kwa wataribu wa kichungaji ili waelewe na kufanyia kazi.
Pia ninawasihi kujadili yale ambayo
tumekubaliana hapa katika warsha hii ili kusaidia wengine kufanya hivyo.
Tunataka Ofisi zetu za Kichungaji ziwe na nguvu za kujibu changamoto mbalimbali
za kifamilia na na kutoa miongozo mbalimbali ya kichungaji ili kufikia malengo
yetu," amesema Askofu Anyolo.
Aidha amewasisitiza waratibu wa
kichungaji kuhakikisha kwamba wanashiriki mikutano inayofanyika katika kanda
zao na katika nchi za AMECEA ili kupeana mbinu mbalimbali za kichungaji
ikifahamika kuwa sekta ya Uchungaji ni nyeti maana inagusa maisha ya watu
kiroho na kimwili.
“Ni vyema kuungana na kujifunza kutoka kwa kila mmoja. Kujenga
mahusiano chanya kati yetu na kuimarisha imani yetu,” amesisitiza Askofu
Anyolo.
Semina hiyo ya Waratibu wa Kichungaji
imehudhuriwa na washiriki 14 kutoka
nchi 8 za AMECEA yaani; Ethiopia, Eritrea, Kenya, Malawi, Tanzania, Uganda na
Zambia na kuwezeshwa na wafanyakazi kutoka Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki cha
Afrika Mashariki (CUEA) kwa ufadhili wa USCCB.
Comments
Post a Comment