Papa Francisko: Miaka 4 ya Kumbu kumbu ya kuchaguliwa kwake!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 4 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na tangu mwanzo amejipambanua kuwa ni mtu wa watu mintarafu hotuba yake ya mwanzo kabisa, aliyoonesha na kushuhudia: amani na utulivu wa ndani; upole na unyenyekevu kiasi cha kuomba sala kutoka kwa watu wa Mungu ili waweze kumsindikiza katika maisha na utume wake. Tangu wakati huo, Baba Mtakatifu aliwataka waamini kutembea kwa pamoja kwa kujiaminisha katika sala na huruma ya Mungu.
Ikumbukwe kwamba, Papa Francisko hakuwa kati ya Makardinali waliokuwa wanatajwa sana na vyombo vya habari kuwa wangeweza kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki baada ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuamua kung’atuka kutoka madarakani! Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Kardinali Parolin anakaza kusema, Baba Mtakatifu anapenda kuendeleza safari ya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, iliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kweli zile cheche za mageuzi zilizoletwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ndani ya Kanisa ziweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kanisa halina budi kufanya hija ya kumwelekea Kristo Yesu, huku likiwasaidia watu kukutana na watu, ili kwa pamoja waweze kusonga mbele!
Hii ndiyo dhana ya Sinodi inayopewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa halina budi kuwaambata wote kwa kujiaminisha chini ya ulinzi, tunza, uongozi  na karama za Roho Mtakatifu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma umelisaidia Kanisa kurejea tena katika mhimili wa maisha na utume wake yaani huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu! Kumbe, Kanisa linapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi. Malango ya huruma ya Mungu yamefungwa kwenye Majimbo mbali mbali, lakini Mlango wa huruma ya Mungu ambaye ni Kristo Yesu, bado uko wazi kwa wale wanaotaka kutubu na kumwongokea Mungu ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na kifani!
Kardinali Parolin anasema, Maadhimisho ya Mwaka Huruma ya Mungu imekuwa ni fursa kwa waamini kutambua umuhimu wa Sakramenti za huruma ya Mungu yaani: Ekaristi Takatifu na Kitubio. Kumekuwepo na mwamko mkubwa kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho sehemu mbali mbali za dunia, jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake umuhimu wa upendo na mshikamano wa huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kipindi hiki cha Kwaresima mwaliko ni kutubu na kumwongokea Mungu; kusali, kutafakari, kufunga na kujinyima; yote haya yanamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma ya upendo wa kidugu kwa maskini ni utambulisho makini wa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia.
Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” ni zawadi kubwa kwa  waamini katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Familia inakabiliana na changamoto nyingi ambazo ni matokeo pia ya dhambi ya asili ambayo imemwachia mwanadamu majeraha makubwa katika maisha yake. Wosia huu ni chachu ya mageuzi katika maisha na utume wa familia. Shutuma na hali ya kutoelewana ni sehemu ya safari ya maisha ya Kanisa hapa duniani! Baba Mtakatifu Francisko anasema, anakubali kukosolewa, lakini ukosoaji huu uzingatie ukweli, hali na huruma ya Mungu kwa binadamu, ili hatimaye, kuweza kusoma alama za nyakati na utashi wa Mungu, tayari kuumwilisha katika uhalisia wa maisha ya binadamu.
Kardinali Parolin anasema, moyo wa binadamu ni kiini cha mageuzi yanayotekelezwa na Mama Kanisa na kwamba, Kanisa daima liko katika mchakato wa mageuzi yanayojikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kuliweza Kanisa kujizatiti zaidi katika maisha na utume wake. Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, kumekuwepo na maamuzi makubwa yaliyofanyika na kutekelezwa, lakini haya ni mageuzi ambayo yanapaswa kupata chimbuko kutoka katika undani wa maisha ya familia ya Mungu. Lengo ni kuwawezesha waamini kurejea katika mambo msingi ya maisha na utume wa Kanisa, kwa kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kutangaza na kushuhudia asili na kiini cha Kanisa.
Kardinali Parolin anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kuwa karibu zaidi na Papa Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anayeendelea kushuhudia kwa walimwengu utajiri mkubwa wa amani, utulivu wa ndani, furaha na ucheshi hata pale anapokabiliwa na matatizo na changamoto katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kuna changamoto nyingine ni kubwa kiasi hata cha kutishia maisha, lakini bado Papa Francisko anayaangalia matukio yote haya kwa amani na utulivu wa ndani sanjari na kuendelea kujiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa wale wanaomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Yote haya anasema Kardinali Pietro Parolin katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Papa Francisko anapoadhimishwa kumbu kumbu ya miaka 4 tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki yanampatia faraja, imani na matumaini ya kuendelea kusonga mbele katika maisha na utume wake, kama Katibu mkuu wa Vatican.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI