AMECEA yaipongeza Tanzania miaka 150 ya uinjilishaji
MWENYEKITI wa Umoja wa wanachama Mabaraza
ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki (AMECEA), Mwadhama Berhaneyesus
Kardinali Souraphiel wa Addis Ababa
Ethiopia amelipongeza Kanisa Katoliki Tanzania kwa Jubilei ya miaka 150 ya
uinjilishaji akisema ni ukomavu wa imani.
Akizungumza na Gazeti Kiongozi hivi
karibuni Addis Ababa Ethiopia, Kardinali Souraphiel amesema kuwa, anafahamu
Kanisa Katoliki Tanzania kuwa lina historia ndefu ya imani kuanzia mlango wa Imani
Bagamoyo ambapo wamisionari wa Kwanza waliingia na kusimika msalaba.
“Ninawapongeza maaskofu, mapadri wa
majimbo na mashirika ya kitawa pamoja na waamini wote kwa kuilinda imani
Katoliki ambayo ni tunda la wamisioari wa Kwanza nchini humo.
Changamoto za wamisionari za wakati ule
zilikuwa si za kawaida. Ninakumbuka wakati fulani Kardinali Pengo alinieleza
mengi kuhusu historia ya Uinjilishaji nchini Tanzania ambayo ina mvuto wa
kipekee. Mimi mwenyewe nilishawahi kufika Bagamoyo kushuhudia asili ya Ukristo Tanzania.
Ninajivunia kuwa imani Katoliki imekuwa
imara hadi sasa nchini Tanzania. Ninawaombea waamini wote pamoja na maaskofu
kuendelea kuishikilia imani yao bila kujali changamoto mbalimbali ambazo ni
sehemu ya utume.
Hongera Kanisa la Tanzania kwa utume.
Mtuombee na sisi Kanisa la Ethiopia ambapo bado wakatoliki ni wachache na si
kazi rahisi kuinjilisha hapa kwani dini zingine zina waamini wengi kuliko
wakatoliki lakini pia ninafarijika kwani mapadri, waamini na maaskofu
wanajituma kutekeleza utume wao kama inavyopaswa,” ameeleza Kardinali
Souraphiel.
Hata hivyo Kardinali Souraphiel
amefarijika warsha ya kuratibu rasilimali kufanyika katika nchi yake na Baraza
la Maaskofu Katoliki Ethiopia akisema kuwa ni heshima kwake na kwa waamini
pamoja na maaskofu na mapadri nchini humo.
“Tumeshiriki mikutano mbalimbali ya
AMECEA Dar es Salaam Tanzania ambapo nilipafurahia, tumeenda Malawi na Kenya
kwa mara kadhaa. Hivi leo ninapoona wanahabari na Makatibu wa Idara ya
Kichungaji kutoka nchi mbalimbali za AMECEA ninaona furaha ya ajabu.
Hata hivyo iwe ni moja ya maandalizi ya
Sinodi ya Maaskofu AMECEA (plenary) itakaofanyika mwezi Juni mwaka 2018 .
Hii ni mara ya kwanza Sinodi hiyo
kufanyika Ethiopia ndiyo maana tuna shauku kubwa na tayari tumeanza maandalizi
ya kuwapokea maaskofu zaidi ya 200, viongozi wa serikali, mapadri pamoja na
waamini kutoka ndani na nje ya nchi.
Hii inaonyesha umoja na mshikamano
katika jamii na ulimwengu wa sasa. Hata Kanisa Katoliki la Ethiopia kwa uchache
wao linapata faraja kuwaona ndugu zao wakiwaimarisha kiimani na kufarijika kuwa
wana ndugu zao kutoka mataifa mengine,” ameeleza.
Kardinali Souraphiel pia ameeleza kuwa,
angefarijika sana kama Papa Fransisko ataitembelea Ethiopia wakati wa safari
yake nchini Sudani kwani Ethiopia ni karibu na nchi hizo na waamini wa Ethiopia
pia wanahitaji kuimarishwa kiimani na kwamba Ethiopia ni Mji Mkuu wa Umoja wa
Mataifa ya Afrika.
“Tayari Umoja wa Mataifa ya Afrika (AU)
umemualika Papa kuja Addis Ababa kuzungumza nao pengine yatazungumzwa mengi
ambayo yatatatua migogoro katika nchi za Afrika. Ingawa Kanisa la Ethiopia
halijamualika Papa lakini tungependa kufanya hivyo ili kama atakubali kufanya
mazungumzo na viongozi wa Afrika hapa Addis Ababa nasi tungepata fursa ya
kushirikishana naye masuala mbalimbali ya kiimani,” amesema Kardinali
Souraphiel.
Comments
Post a Comment