SALA YA JUBILEI YA MIAKA 150 YA UKRISTO, TANZANIA BARA
Ee
Mungu mwenyezi/ Baba wa milele /tunakushukuru kwa zawadi ya Mwanao mpendwa Yesu
Kristo /aliyetwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu / akazaliwa na Bikira
Maria. / Yeye alihubiri neno lako/ na kukamilisha ukombozi kwa mateso / kifo na
ufufuko wake wa ajabu./Hatimaye aliwaagiza Mitume wake akisema / “Enendeni
ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. / Aaminiye na kubatizwa
ataokoka / asiyeamini atahukumiwa/ (Mk 16:15-16).
Kwa
kuitika agizo hilo/ wakati ulipowadia / kwa mapenzi yako uliwavuvia Watawa
mashuhuri wa Shirika la RohoMtakatifu / ambao kwa ujasiri wa ajabu walifika
huku kwetu/ wakausimika Msalaba katika kituo cha Bagamoyo./ Msalaba huo ni
ishara ya ushindi wa Mwanao dhidi ya dhambi na mauti. / Wamisionari hao
wakishirikiana na wenzao waliofika baadaye / walikuhubiri Wewe. / Nasi tuliopata
imani kwa mahubiri yao /tunakukiri Wewe kuwa Bwana Mungu wetu / mwingi wa
huruma/ mwenye fadhili / si mwepesi wa hasira / mwingi wa rehema na kweli. /
(Ayubu 4:3).
Basi,
tunaposherehekea yubilei ya miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania Bara /
tunakuabudu katika maongozi yako./ Tunakushukuru kwa kuongezeka kwa imani/
inayoonekana katika idadi ya Waamini Walei / Makatekista / Watawa / Mapadri na
Maaskofu wazalendo. / Tunakushukuru kwa kutuwezesha kuhudumia taifa letu katika
elimu / afya na huduma nyingine za kijamii.
Tunajua
kuwa bila wewe hatuwezi kitu / tunakuomba uwe pamoja nasi katika kukabiliana na
changamoto mbalimbali kwenye taifa letu siku hizi hasa / ulevi wa pombe na dawa
za kulevya / usafirishaji haramu wa binadamu / ugaidi / maradhi, / ubakaji /
ulawiti / dhuluma / ushirikina na ulegevu wa dini. /
Tunamwomba
Mama Bikira Maria /Nyota ya uinjilishaji mpya / na Mlinzi wa Taifa letu
/atuombee kwako daima/ ili tuendelee kuihubiri injili yako katika maisha yetu
ya kila siku.
Tunaomba
hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.Amina.
Imeidhinishwa
kutumika : Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa
RAISI WA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI
TANZANIA
Comments
Post a Comment