‘Dhambi ya ubinafsi chanzo cha uharibifu wa mazingira’ Maaskofu
IMEELEZWA
kuwa dhambi ya ubinafsi ni sababu kuu inayopelekea uchafuzi wa mazingira na
kutishia uumbaji, hata kufikia hatua ya kutishia uhai wa mwanadamu kwa sababu
ya kutafuta utajiri unaopindukia.
Hayo yamebainishwa na Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe
wa Kwaresima walioutoa hivi karibuni kwa waamini wote nchini, ukiwa na dhima
isemayo ‘Furaha ya Injili na uumbaji’.
Wameeleza kuwa wanadamu
wamepewa vyote na Mungu ili wavitunze, lakini pale wanapokuwa wakala wa
uharibifu wa uumbaji, wanakuwa amesahau wajibu waliopewa wa kuilima na kuitunza
nchi. Pia wametoa mwito kwa wanadamu kutumia kipindi hiki cha kwaresima
kumrudia Mungu kutokana na kukosa utii wa kutunza mazingira.
“Tunashuhudia leo hii
uharibifu mkubwa wa mazingira, mito inakauka, hewa inachafuliwa kutokana na
shughuli za viwanda na motokaa, ardhi inachafuliwa kwa mifuko ya plastiki na
taka ya sumu.. ukataji wa miti umepelekea mwanadamu kuumba jangwa na
kusababisha mmomonyoko wa ardhi, uchimbaji wa madini unaacha athari kubwa za
kimazingira na kudhuru afya ya mwanadamu. Mwanadamu anasahau kuwa kila kiumbe
kina thamani kubwa mbele ya Mungu…” wameeleza.
Aidha wameweka wazi
kuwa jamii inayopuuza mustakabali mwema wa mazingira na uumbaji, ni jamii
isiyojijali yenyewe na isiyojali vizazi vijavyo. Wameonya kuwa ni hatari kubwa
kupumbazwa na tama za kujitajirisha au uzembe wa kutojali ambao unapelekea
kufanya uharibifu mkubwa kwa dunia iliyo makazi ya pamoja.
“Ubinafsi unapofusha
macho ya dhamiri zetu na tunashindwa kulinda na kutetea mifumo ya kimazingira
ambayo imeumbwa kwa ajili ya kututunza” wameongeza.
Pia Maaskofu
wametahadharisha hali ya mwanadamu kujitafutia furaha kupitia vitu, starehe
chafu, mali zisizo halali, na kusema kuwa hali hiyo siyo tu inatishia uumbaji,
bali hupelekea mwanadamu kutishia uhai wake mwenyewe kwa sababu ya kutafuta
utajiri unaopindukia.
“Kwaresima ni mwaliko
wa kurudi na kuishi tena maisha ya kumpendeza Mungu. Ni mwaliko wa kufungua
masikio ya mioyo yetu na kuisikiliza sauti ya Mungu, inayookoa na
kututhibitishia furaha ya kweli” wamesema.
Na Pascal Mwanache, Dar es salaam
Comments
Post a Comment