Watoto walemavu na wazee waendelea kunyanyapaliwa
MOROGORO,
Serikali imeshauriwa kusaidia kujenga vituo vya
afya katika vituo vya kulelea watoto wenye ulemavu mbalimbali kutokana
na kunyanyapaliwa na baadhi ya wahudumu wa vituo vya afya vya umma wanapokwenda kupata huduma ya matibabu.
Mkurugenzi wa Kituo cha Amani Centre kilichopo
Mkoani Morogoro Padri Beatus Sewando, amebainisha hayo wakati akieleza
changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wenye ulemavu hususani wanapoenda
kupatiwa huduma za afya katika vituo vya afya.
Padri Sewando amesema kuna baadhi ya wahudumu
wa afya katika hospitali za umma ambao hutoa huduma mbaya kwa watoto wenye
ulemavu hasa kutowasikiliza kwa wakati kiasi cha kusababisha vifo vya watoto
hao.
“Tunapokwenda kwenye hospitali za umma baadhi
ya wahudumu wanawanyanyapaa mkishasema kwamba huyu ni mlemavu na wanapoona
matendo anayoyatenda, huduma zinakuwa mbaya zaidi na inasababisha baadhi ya
watoto kupoteza maisha, endapo wangepatiwa huduma kwa wakati wangepona,”
amesema Padri Sewando.
Aidha amefafanua kuwa watoto wenye ulemavu
wanapofika katika hospitali hasa za umma hupokelewa tofauti na wale wasiokuwa
na ulemavu, kiasi cha wasimamizi na walezi wa watoto hao kujisikia vibaya kwa
mapokezi hayo na kuona wazi kuwa watoto hao wananyanyapaliwa.
Pamoja
na hayo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa kulingana na sera ya afya wazee na
watu wenye ulemavu hupata matibabu bure, lakini imekuwa ni tofauti kwa watoto
hao hali inayowalazimu baadhi ya watu wenye mapenzi mema kuwakatia baadhi ya
watoto hao bima za afya.
“Hili suala linapaswa kufuatiliwa na serikali
yenyewe kama wametamka kitu waweke ufuatiliaji waone ile bure inafanyika
kweli?, kwasababu malalamishi tunayasikia hata kwenye vyombo vya habari hata kwa wazee ambao wanatakiwa
watibiwe bure sijaona wazee wanaoridhika kiasi cha kuamini anapata huduma bure,
akienda pale mzee ataandikiwa lakini dawa hamna hivyo kama serikali ina nia ya
dhati kuwahudumia wazee na wenye ulemavu ifanye mpango kuwe na fungu na akiba
maalumu ya dawa kwa ajili yao na kuwapa kipaumbele,” amesema Padri Sewando.
Hata hivyo
amesema kuwa ana imani na serikali ya awamu ya tano kuwa itatekeleza na
kusimamia vyema suala la huduma za afya kwa wazee na walemavu kwa sababu kwa
muda mrefu imekuwa kinyume na utekelezaji wa sera husika.
Wakati huohuo Padri Sewando amewaomba wahudumu
wa afya kuwa na huruma na watoto walemavu na wazee kwa kuwajali na kuwapatia
huduma sawasawa na wengine, kwani hawakupenda kuzaliwa walemavu na uzee
haukwepeki na kuwapa huduma stahiki bila manung’uniko ni Baraka pia.
Comments
Post a Comment