KANISA KATOLIKI KUENDELEA KUSIMAMIA UKWELI
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, kwa masuala ya kanuni maadili na utu wema, Kanisa litaendelea kusimamia, kutangaza na kushuhudia ukweli kuhusu Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, dhidi ya ndoa za watu wa jinsia moja, jambo linalokwenda kinyume kabisa cha mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Kanisa litaendelea kusimama kidete kupigania utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; litaendelea kuhamasisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa njia ya kanuni auni. Kanisa linapania kuwalinda na kuwaendeleza watoto dhidi ya vitendo vyote vinavyotaka kudhalilisha utu na heshima ya binadamu!
Kardinali Pietro Parolin ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa Jimbo kuu la Firenze, Italia kushiriki katika kongamano lililochambua tasaufi inayofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”, kwani Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa watu wa mataifa bila “kigugumizi wala mtima nyongo” kwa sababu furaha, huruma, msamaha na upendo ni kiini cha Injili ya Kristo! Kanisa litaendelea kua aminifu kwa Injili ya Kristo; linaendelea kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, lakini pia Kanisa linatangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili bila kuyumbishwa kwani Injili ni Habari Njema kwa wote pasi na ubaguzi.
Kanisa lipo kwa sababu ya ustawi na maendeleo ya wengi, bila Kanisa linalojikita katika kweli za Kiinjili, leo hii, mwanadamu angekuwa amekwishamezwa na majanga mengi yanayotikisa mizizi ya utu na heshima yake. Kanisa haliwezi kuyaangalia matatizo na changamoto za ulimwengu mamboleo kwa jicho la kengeza! Kanisa linapenda kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto mamboleo kwa mwanga na tunu msingi za Kiinjili. Haya ni matatizo na changamoto zinazoibuliwa katika maisha ya ndoa na familia; uhai, utu na heshima ya binadamu, ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuimarisha majiundo makini ya awali na endelevu ili kweli Wakleri waweze kutoa majibu yanayosadifu changamoto na kiu ya watu wa Mungu katika maeneo yao bila kufumbia macho kweli za Kiinjili.
Kardinali Parolin anakaza kusema, hata pale Kanisa linapotikiswa kwa kashfa kama ilivyojitokeza kwa kashfa za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha msimamo wake thabiti na kushughulikia masuala yote haya kwa umakini mkubwa. Kujiengua kwa Mama Marie Collins kutoka kwenye Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Dhidi ya Nyanyaso za Kijinsia ni matokeo ya malumbano ambayo yametafsiriwa kuwa ni kikwazo cha mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo! Ili kutingisha kibuyu! Mama Marie Collins akaamua kubwaga manyanga, Jumatano ya Majivu, tarehe 1 Machi 2017. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anaendelea kukaza akisema, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea watoto wadogo, dhamana ambayo amemkabidhi Kardinali Sean P. O’Malley na Tume yake wanaoendelea kupata ushirikiano na mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo kwa kuunda mazingira salama kwa maisha, ustawi na maendeleo ya watoto: kiroho na kimwili ili kusiwepo tena na kashfa za nyanyaso kwa watoto wadogo ndani ya Kanisa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment