PAPA FRANSISKO AENDELEA KUHUBIRI AMANI, HURUMA NA HUDUMA DUNIANI


Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekazia umuhimu wa Kanisa kutoka ili kutangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Kristo aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kwani hawa kimsingi ni amana na utajiri wa Kanisa. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwa kweli ni sauti ya wakimbizi na wahamiaji, watu wanaoonekana kuwa ni kero kwa baadhi ya mataifa, kiasi cha kusahau kwamba, hata hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; ni watu wenye heshima na utu wao unaopaswa kulindwa na kudumishwa.
Baba Mtakatifu anaendelea kukazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu, Injili ya familia, pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu! Ni Baba wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika damu ya Wakristo wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake; Uekumene wa maisha ya kiroho unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya Kikristo kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kama njia ya kupambana na changamoto mamboleo!
Uekumene wa sala unaowawezesha Wakristo kukutana ili kumwabudu, kumshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu asili ya wema na utakatifu wote. Lakini zaidi, Baba Mtakatifu Francisko anakazia Uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamiii, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Baba Mtakatifu anaendelea kujipambanua kuwa kweli ni mtu wa watu kwa ajili ya watu ili kuwapeleka watu hawa kwa Kristo Yesu kwa njia ya Kanisa lake.
Ni kiongozi ambaye amebahatika kuwa na lugha rahisi inayoweza kupenya akili na nyoyo za watu kwa urahisi pamoja na kuwashirikisha katika maisha na utume wake, ndiyo maana tangu mwanzo amekuwa akiwaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala! Ni kiongozi ambaye amethubutu kulipyaisha Kanisa ili liweze kuendelea kuwa aminifu kwa Kristo Yesu, dhamana inayokumbana na vizingiti vingi, lakini Baba Mtakatifu bado anasonga mbele kwa imani, matumaini na ujasiri mkuu. Lengo ni kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi, daima mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza.
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni tukio ambalo limewawezesha waamini kutafakari Fumbo la Huruma ya Mungu, chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani; huruma ni kiungo muhimu sana kinachomuunganisha Mungu na mwanadamu, chemchemi ya upendo wa daima kutoka kwa Mwenyezi Mungu licha ya udhaifu na mapungufu ya binadamu! Ameliwezesha Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee katika mambo msingi ya maisha na utume wa Kanisa ili kujibu changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Huu ni mchakato unaopania kumwilisha utajiri mkubwa unaofumbatwa katika mafundisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwani Kanisa linataka kukoleza majadiliano yanayofumbatwa katika huruma bila ya ukali! Kumbe, Baba Mtakatifu anaonesha kuwa ni mchungaji anayeguswa na mahangaiko pamoja na changamoto za watu wake, ili kuwasikiliza na kuzijibu changamoto hizi katika mwanga wa Injili.
Papa Francisko anataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: haki na amani; utunzaji bora wa mazingira na huduma kwa maskini kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Ni kiongozi anayeshuhudia Injili ya furaha inayobubujika kutoka katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake. Anawathamini na kuwajali wanawake wanaochangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya Kanisa hasa wakati huu wa mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Papa Francisko ni kiongozi anayeendelea kutoa changamoto kubwa ndani na nje ya Kanisa! Huu ni mwaliko wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu!
Wakati kama huu, Kanisa linapenda kumshukuru kwa namna ya pekee kabisa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliyeonesha ujasiri, imani na matumaini thabiti kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kukubali kung’atuka kutoka madarakani, ili kuwaachia wengine kuendeleza maisha na utume wa Kanisa. Anaendelea kusali kwa ajili ya Kanisa na kwa hakika atakumbukwa daima kutokana na ujasiri wake wa kiimani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI