HABARI ZAIDI

Ijumaa, 14 Juni 2019

Huwezi kutenganisha utume wa walei na maendeleo ya Kanisa- Kard.Pengo asema

IMEELEZWA kuwa waamini walei nchini wamekuwa chachu ya maendeleo ya Kanisa kwa ushiriki wao kikamilifu katika mipango na utekelezaji wake katika hatua mbalimbali.
Hayo yameelezwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya utume wa walei Tanzania, yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Msimbazi Center jijini Dar es salaam na kufikia kilele chake Juni 16, 2019.
Kardinali Pengo ameeleza kuwa walei hawapaswi kujiona kuwa ni watu wa kuambiwa tu kana kwamba hawana mchango wowote, bali wanapaswa kuona kuwa wao ni sehemu muhimu ya maendeleo ya Kanisa.
“Kabla ya Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani waamini walei walisubiri watekelezewe kila kitu kana kwamba hawana chochote cha kutoa. Baada ya mtaguso huo Kanisa limetambua nafasi ya walei na hivyo ni lazima wajue kuwa wana sehemu muhimu ya kufanya, siyo tu kulipa zaka na kusikiliza maelekezo” ameeleza Kardinali Pengo.
Aidha Kardinali Pengo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha waamini kutoka majimbo yote nchini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa jubilei hiyo.
Pia ametoa mwito kwa waamini kushiriki matukio mbalimbali yanayotangulia kilele cha jubilei hiyo ikiwa ni pamoja na semina mbalimbali zitakazotolewa na maaskofu na watu walioandaliwa, ikiwa ni njia moja wapo ya kuadhimisha miaka 50 ya utume wa walei.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Idara yaUtume wa Walei ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Raphael Madinda ameeleza kuwa uwepo wa walei katika Kanisa umekuwa chachu ya kuongezeka kwa miito mitakatifu ambayo inachipuka kupitia familia.
Amesema kuwa kupitia familia ambao ndio walei ndiko Kanisa linapata miito mbalimbali kama vile upadri na utawa, huku akitoa wito kwa waamini walei kuendelea kuziimarisha familia zao kwani mchango wake katika ustawi wa Kanisa ni mkubwa.


Ask. Nyaisonga aongoza waamini Iringa kwenye Jubilei za Mapadri

askofu Mkuu wa Jimbo Kuu  Katoliki Mbeya Mhashamu Gervas Nyaisonga  hivi karibuni ameongoza waamini wa Jimbo Katoliki  Iringa katika maadhimisho ya jubilei mbalimbali za mapadri wa jimbo hilo.
Walioadhimisha Jubilei ni pamoja na Monsinyori Julian Kangalawe Pelate ambaye ameadhimisha miaka 50 ya Upadri.
Pia walikuwemo mapadri walioadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya upadri akiwemo Padri  Richard Chatila Paroko wa Parokia ya Kihesa,  Padri Paul Msombe Paroko wa Parokia ya Ipogolo,  Padri Baptist  Duma Paroko wa  Parokia ya Mdabulo,  Padri Christopher Nyoni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki RUCU na Padri Cephas Mgimwa ambaye pia anafanya kazi Chuo Kikuu  cha Kikatoliki RUCU ambaye hakushiriki Misa hiyo yupo nje ya nchi kwa majukumu mengine.
Akitoa homilia katika Misa hiyo ambayo imefanyika katika ukumbi wa Seminari ya malezi Mafinga na kuhudhuriwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, Askofu wa Jimbo Katoliki Ifakara Mhashamu Salitarius Libena na mapadri kutoka ndani na nje ya Jimbo pamoja na waamini, Askofu Nyaisonga amewataka wanajubilei hao kutambua kwamba bado hawajamaliza kazi hivyo  wanapaswa kuweka juhudi zaidi katika kutakatifuza ulimwengu.
“Ninawasihi mmbaki kuwa mashahidi  wa Injili katika ulimwengu. Tunawategemea kufundisha ukweli wa Injili na muwe mashahidi wa Imani yenu kama walivyokuwa Mashahidi wa Uganda,” amesema Askofu Mkuu Nyaisonga.
Maadhimisho hayo ambayo yameadhimishwa siku ya Sikukuu ya Mashahidi wa Uganda Askofu  Nyaisonga amesema kuwa matukio yote ya mashahidi hao hayatokani na kifo cha ushahidi bali maisha yao kwani waliishi kikamilifu na walikuwa tayari kumwaga damu kwa ajili ya imani yao.
“Sisi leo tunapomshukuru Mungu kwa hilo,  tunao mashahidi wengine ambao hawakumwaga damu,  bali wametoa jasho lao,  wamemtumikia Mungu kwa miaka 25 na 50 miaka hiyo si mchezo” amesema Askofu Nyaisonga na kuongeza;
“Mapadri hawa wanamshukuru  Mungu kwa kuwa hawana mastahili yoyote,  sisi leo tunawasifu kwasababu bila shaka miaka hiyo wamedhihakiwa kwa useja wao, ufukara, utii, maudhi, mambo mengi tu,  wameamini kwa dhati hata Mwenyezi Mungu amewatambua, wamevumilia na kuamini ndiyo maana tunawasifu na kuwapongeza leo.”
Amewalezea wanajubilei hao kuwa miaka hiyo 25 na 50 umri wao unawaambia wana imani na hadi sasa wanapenda wito wao na wameushikilia.
  Hamjamaliza kazi, mzidi kuita Roho ya Bwana iwaongoze. Mna wajibu wa kuendelea kuwa mashahidi wa sasa,” amesema.
Vile Vile amewataka waseminari ambao wanalelewa katika seminari hiyo nao pia wawe mashahidi kama msimamizi wao wa Seminari Mt Kizito na sio kumudu taaluma tu.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanajubilei wenzake,  Paroko wa Parokia ya  Ipogolo Padri Paulo Msombe amesema wanamshukuru Mungu, wazazi jamaa na marafiki kwa malezi yao katika kuchochea wito wao.

“ Tunashukuru pia Askofu wetu Ngalalekumtwa kwa malezi yake tangu alipokuwa Rector  wa Seminari hii ya Mafinga hata sasa Askofu kwa malezi yake  ambayo yametusaidia kufika hapa tulipo,” amesema  Padri Msombe.

Askofu Nzigilwa apongeza Utume wa Halmashauri ya Walei Tanzania


Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mhasham Euzebius Nzigilwa ameungana na waamini na viongozi wa Halimashauri ya Walei Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam katika kuadhimisha jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya utume wao.
Akitoa homilia yake wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya adhimisho hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Msimbazi centre Dar es salaam, Askofu Nzigilwa amesema kuongezeka kwa imani nchini kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa utume wa halimashauri ya walei.
 “Nia ya Askofu Mkuu wa Jimbo hili Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo ya kutaka kujengwe nyumba za mapadri kwaajili ya kuwasogezea waamini huduma za kiroho kutoka kwa mapadri ilichagizwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa halimashauri ya walei.
Na utume wao tangu mwanzo umelipa jimbo letu nguvu ya kuinjilisha na kukua kwa imani,” amesema Askofu Nzigilwa.
Aidha ametoa wito kwa Halmashauri ya Walei Jimbo na kwa waamini wote waliobatizwa kuendelea kuishi kitakatifu katika wito wowote wanaoitiwa na Mwenyezi Mungu na wanao wajibu wa kuulinda.
Amesema ipo miito mingi na miongoni mwake ni wito wa kuwa watakatifu ambao amepewa kila Mkristo mbatizwa sanjari na wito wa uinjilishaji unaomgusa kila mbatizwa na kama Yesu alivyoagiza na kufundisha aliposema muwe watakatifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mtakaifu,enendeni ulimwenguni kote mkaihubiri Injili na aliposema kama Baba alivyonituma mimi,nami nawatuma ninyi, ni wazi kuwa kwa mafundisho hayo ya Yesu kila mtu anatumwa wito wa uinjilishaji.
“Ndugu zangu  utakatifu wa maisha ndiyo silaha na nyenzo ya uinjilishaji na maisha hayo hayo matakatifu yanafundisha zaidi kuliko mambo tunayofundisha na kufundishwa.
Sasa ni wakati wa kila mbatizwa kujitahidi kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu,”amesema.
Ameongeza kuwa katika kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu ni sharti kila mmoja apambane ipasavyo na vikwazo vitakavyomfanya asitekeleze hayo na kushindwa kuishi kitakatifu.
Amevitaja miongoni mwa vikwazo huku chakwanza kikiwa ni watu kusikiliza na kutekeleza maelekezo ya ibilisi jambo ambalo ni kovu kubwa linalopelekea kushindwa kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu kwa kuishi kitakatifu.
Pia Askofu Nzigilwa amewaasa waamini na watu wote kuacha tabia ya kuyapelekea maelekeo yao kwa wengine badala yake kila mtu anapofanya kosa akiri kosa lake na si kutafuta kisingizio kwa wengine kama walivyofanya Adamu na Eva kwenye bustani ya edeni walipokula tunda ambalo hawakutakiwa kula na kila mmoja ajue anapofanya hivyo anasikiliza na kutekeleza maagizo ya ibilisi.
“Wanadamu huona haraka makosa ya wengine kuliko mapungufu yao wanasahau fundisho la Yesu ambalo anatufundisha kuona mapungufu na makosa yetu wenyewe na si ya wengine na bila kujua kwamba jambo hilo litawafanya kutokuishi kitakatifu,” amesema.
 Amesema bila kusimama imara  kazi ya uinjilishaji na kuuishi utakatifu itakuwa ngumu kwasababu ni lazima kila mmoja apambane na hila za ibilisi kwamaana utakatifu ni zawadi na ni miongoni mwa matunda ambayo Mungu ametupatia hivyo ni wajibu wa kila mtu kuupalilia utakatifu na ni kwanamna gani atastawisha mbegu hiyo maishani mwake.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa harimashauri ya walei Jimbo Kuu Katoliki Dar es salam Ndg.Richard Sillo amemshukuru Askofu Nzigilwa kwa kuwakumbusha wajibu wao na wao wanaahidi kwamba wataendelea kuutumikia wajibu wao waliopewa kwa kushirikiana na wengine.
Jimbo Kuu Katoliki  Dar es salaam limeadhimisha jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya halimashauri ya walei kijimbo kabla ya kilele cha kitaifa kufanyika June 16, 2019 kwenye viwanja vya Msimbazi Centre Dar es salaam na kukusanya waamini wa majimbo yote 34.
Maadhimisho hayo yatakuwa ya kwanza tangu kuanzishwa kwa halimashauri ya waei mnamo tarehe 24 June 1969.