Askofu Lebulu aadhimisha Jubilei ya Dhahabu ya Upadri

 
Na Sarah Pelaji, Same-Kisangara Juu
Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu ameadhimisha Jubilei ya dhahabu ya  Upadri  yaani miaka 50 tangu alipopata Daraja Takatifu la Upadri.
Jubilei hiyo imeadhimishwa Desemba 11 mwaka huu katika Parokia ya Kisangara Juu Jimbo Katoliki Same ambapo parokia hiyo pia imeadhimisha miaka 50 tangu ilipoanzishwa na katika parokia hiyo ndipo Askofu Mkuu Mstaafu Lebulu alipewa Daraja Takatifu la Upadri na  Askofu Joseph Kilasara Desemba 11 mwaka 1968.
Katika maadhimisho hayo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashamu Gervas Nyaisonga amesema kuwa, kwa niaba ya Maaskofu wakatoliki Tanzania, anampongeza Askofu Lebulu kwa kufanya kazi ya utume uliotukuka huku akimsihi aendelee kulisaidia Kanisa akitumia hekima na vipawa alivyojaliwa.
“Ni wazi Askofu Lebulu amestaafu na anaadhimisha jubilei hii ya dhahabu lakini bado ana nguvu na anahitajika katika Kanisa. Sisi tunamuombea Mungu azidi kumpa nguvu ili tuendelee kufanya kazi pamoja huku tukiiga mfano wake ambao ni kielelezo kwetu sisi watoto wake na wengine wana urika wenzake.
Ana karama mbalimbali ambazo zimeshuhudiwa na wengi na sisi maaskofu tunamfahamu na kutambua vipawa vyake hivyo tunamuomba aendelee kulisaidia Kanisa kwa mashauri yake na hata pale tutakapomuhitaji katika masuala mbalimbali ya kulijenga Kanisa,” amesema Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda.
Akihubiri katika Misa hiyo Takatifu, Askofu wa Jimbo Katoliki Same Mhashamu Rogathy Kimaryo amesema kuwa, anampongeza Askofu Lebulu kwa utume wake tangu alipopewa Daraja Takatifu la Upadri miaka 50 iliyopita.
Pia anampongeza kwa kuliongoza Jimbo la Same kama Askofu takribani kwa miaka 20.
“Mimi ninayefanya kazi katika jimbo hili ninatoa ushuhuda kuwa Askofu Lebulu anazo karama mbalimbali zinazoonekana wazi.
Kwanza kuliongoza jimbo la Same kwa miaka mingi ni dhahiri kwamba alitumia vipawa vyake maana kupewa kuongoza Jimbo la Same kunahitaji kujikubali na kulikubali kwanza jimbo hili. Lina umasikini  wa miundo kwa mazingira yake ya milima iliyopo.
Siyo kazi rahisi kufanya uchungaji hapa. Pili Askofu Lebulu ana karama za kuombea na kubariki watu, kuhubiri, sala, kazi na mwalimu mzuri.
Kumbe anapoadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya upadri wake tunamshangilia na kumpongeza kwa kazi iliyotukuka ambayo imeacha alama wazi katika Kanisa,” amesema Askofu Kimaryo.
Pia amempongeza licha tu ya kufanya utume katika jimbo la Same, amefanya pia utume katika Jimbo Kuu Katoliki Arusha ambalo lina maeneo mbalimbali yenye changamoto za miundombinu na ni jimbo kubwa lenye watu wa tamaduni mbalimbali.
Amewaasa waamini wa Jimbo Katoliki Same kuendelea kumuombea Askofu Mkuu Mstaafu Josaphat Lebulu kwani ni Askofu ambaye alitoa Jimbo Katoliki Same mbali na kulifikisha mbali.
“Alianzisha Chanjale seminary na wengi wenu mlisomea hahapo. Isingekuwa Chanjale Seminary wengi wenu msingekuwa jinsi mlivyo na msingekuwa na maisha mliyo nayo sasa. Kwanza Chanjale Seminary ni seminary maalumu kwani inasomesha hadi wasichana. Ameleta maendeleo mbalimbali ya kiroho na kimwili. Hongera sana,” amesema Askofu Kimaryo.
Aidha amewapongeza waamini wa Kisangara Juu kwa kujitoa kujenga Kanisa kubwa la kisasa kwa kutumia nguvu zao wakati huu wanaposherehekea Jubilei ya miaka 50 ya parokia hiyo.
Amewataka wasomi walioko mjini wa parokia hiyo kuendelea kusaidia nyumbani kwao ili Kanisa la Mungu limalizike na kuwa maridadi kwa ajili ya kutolea sadaka Takatifu.
Kwa upande wake Askofu Mkuu Mstaafu Lebulu amesema kuwa, anapenda kuwashukuru wazazi wake waliomlea katika misingi ya imani ya Kanisa Katoliki, kumsomesha hadi kufikia Daraja Takatifu la Upadri. Pia anawashukuru Maaskofu kwa ushirikiano wao kwake, mapadri, watawa na waamini walei walioweza kumvumilia katika mapungufu yake.
Amemshukuru Mungu kwani yeye ni mkosefu aliyesamehewa na akastahilishwa kuwa Padri na Askofu hadi alipostaafu salama.
Amewaasa maaskofu, mapadri na waamini kuwa wamoja katika utume wa kuliongoza Kanisa.       
Askofu Mkuu Mstaafu Josaphat Louis Lebulu amezaliwa 13 Juni 1942. Alipewa Daraja Takatifu la Upadri na Askofu Joseph Kilasara Desemba 11 mwaka 1968 katika Parokia ya Kisangara Juu. Aliwekwa wakfu na Kardinali Laurean Rugambwa mwaka 1979 na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Same mwaka 1979 mpaka 1998. Mwaka 1999 alisimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha  hadi 27 Desemba 2017 ambapo alistaafu.


Comments

  1. Hongera sana baba Lebulu ulitulisha upya kiapo cha ubatizo waamini na mapadri Arusha wakabadilika sana.Pia ulikomesha ujengwaji wa Baa tengeru kwenye makuti ukafungua kituo cha maombi Sayuni kinabariki sana waumini hatuendi tena madhehebu mengine kuombewa.

    ReplyDelete
  2. Mume wangu amerudi!!! Baada ya miaka 1 ya ndoa iliyovunjika, mume wangu aliniacha na watoto wawili na maisha yangu yalivunjika. Nilitaka kuyamaliza, nusura nijiue maana alituacha bila chochote. Nimekuwa nimevunjika kihisia wakati huu wote na maisha yanaonekana kutokuwa na maana. Siku moja mwaminifu, nilipokuwa nikivinjari mtandao, nilikutana na baadhi ya shuhuda kuhusu Dk DAWN. Baadhi ya watu walishuhudia kwamba alimrudisha mpenzi wao wa zamani, wengine walishuhudia kwamba anarejesha tumbo na kuponya magonjwa kwa mimea. Nilipendezwa zaidi na upatanisho na mume wangu, ambao Dk. DAWN aliwezesha kumrudisha mume wangu ndani ya siku 3. Sasa mume wangu amerudi na tumekuwa tukiishi kwa furaha tangu wakati huo. Shukrani zote kwa Dk DAWN. Hapa, ninaacha mawasiliano yake kwa kila mtu. Maana kuna changamoto za aina yoyote,
    Barua pepe ( dawnacuna314@gmail.com )
    Whatsapp: +2349046229159

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI