Ushoga siyo haki ni udhalilishaji wa binadamu
Katika kuadhimisha miaka 70 ya
azimio la ulimwengu la haki za binadamu viongozi wa dini kutoka Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wamekutana na kuweka wazi kuwa wanalo jukumu
la kusimamia haki huku wakibainisha kuwa vitendo vya ushoga vinadhalilisha utu
wa mwanadamu.
Akitoa mada katika kongamano hilo
Katibu Mkuu wa TEC Padri Dkt. Charles Kitima amesema kuwa katika jamii zote,
haki za binadamu zipo hasa katika mila na desturi na kwamba haki za msingi ni
stahili za kila binadamu kwa sababu ya utu wake.
“Maandiko Matakatifu yanatambua
haki za binadamu kwa mfano haki ya kuwa na familia, kuoa na kuolewa. Ndiyo
maana ushoga unapigwa vita. Ndoa iwe na fursa ya kuendeleza ubinadamu.
Utaletaje ndoa ambayo haina ya kuzaa” amehoji Padri Kitima.
Aidha amesema kuwa viongozi wa
dini hawana budi kupigania na kusimamia haki za wanyonge kama ambavyo
wanaendelea kufanya bila woga. Ameongeza kuwa Kanisa Katoliki linahuisha
mchango wa kimaadili kwa jamii, na hivyo kuhimiza umuhimu wa kulinda haki za
binadamu.
“Tangu mwaka 1997 viongozi wa
dini wamepambana na haki katika migodi na kuisaidia serikali. Miaka 20 mmepiga
vita na kusimamia haki ya mnyonge mpaka haki ifanyike. Hivyo viongozi wa dini
tuna kazi pia ya kulinda haki za umiliki wa ardhi kwa manufaa ya wananchi wote”
amesema.
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza
la Ulamaa BAKWATA Sheikh Issa Athuman Issa amesema kuwa mwili wa binadamu ni
dhamana kutoka Mungu na hivyo haki za binadamu hazina budi ziangaliwe kwenye
jicho la kiimani.
“Wengine wanazungumzia kuwa mwili
wake ni milki yake na anaweza kuutumia kadiri anayotaka. Vifungu 2 na 3
vinaungana na dharura tano kadiri ya Uislamu: Moja, kuhifadhi dini: kuheshimu
yanayorudiwa; Mbili, kuhifadhi nafsi yake na ya wengine “Wewe, usidhuru, na
usiwe na sababu ya mwingine kudhurika. Tatu, Kuhifadhi akili: dhidi ya ulevi,
madawa ya kulevya. Nne, kuhifadhi nasaba au koo, kwa utaratibu wa kuoana. Kama
ushoga hauhifadhi ukoo. Tuliogope na tulilinde sana swala la koo na nasaba. Na
tano ni kuhifadhi hadhi ya mtu, nafsi yake” amesema .
Pia aeongeza kuwa msingi wa
kwanza ni kumfanya mtu ajitambue thamani yake na hivyo viongozi wa dini
wanapaswa wahakikishe kuwa binadamu anatambua thamani yake. “Tuambukize kwa
watoto wetu kujitambua kuwa wana thamani kama binadamu” ameeleza.
Akielezea juu ya maadhimisho hayo
Askofu wa Jimbo Katoliki Mbinga Mhashamu John Ndimbo amesema kuwa azimio hilo
ni chimbuko la viongozi wa dini mbalimbali kukaa pamoja na kutathmini mikakati
itakayowawezesha katika kulinda na kutetea haki za binadamu.
“Azimio hili ndani ya miaka 70
limetufanya sisi wa dini mbalimbali tuje pamoja tuzungumze pamoja, tukae pamoja
tuangalie watu wetu wanaishi namna gani na wanapata haki zao” amesema.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Pwani
Sheikh Hamis Mtupa amebainisha kuwa vitendo vya ushoga havipaswi kukingiwa
kifua mbele kwa kuwa havikubaliki kwa Mungu na hata kwa jamii.
“Kuna haki nyingine ambazo huwa
zinasemwa kuwa ni haki za kibinadamu lakini siyo haki za kibinadamu bali ni
haki za kudhalilisha utu wa mwanadamu. Ni kama vile mahusiano ya jinsi moja,
wanawake kwa wanawake au wanaume kwa wanaume. Ni jambo ambalo halifai. Ni jambo
ambalo tunapaswa kuliondoa kwani linamuudhi Mungu” ameweka wazi.
Kwa upande wake Askofu wa AIC
Pwani Askofu Charles Salala amesema kuwa
kitu muhimu ni jinsi ambavyo jamii ya sasa inavyorithisha maadili kwa kizazi
kinachofuata.
“Jinsi tunavyoishi sasa ndiyo
huamua jinsi kizazi kitakachofuata kitakavyokuwa. Tunahitaji kuwekeza kwa
watoto na vijana wetu” amesema.
Maadhimisho hayo yamefanyika
Desemba 10 katika ukumbi wa mikutano Golden Tulip jijini Dar es salaam na
kuhudhuriwa pia na wadau wa masuala ya haki za binadmu nchini.
Comments
Post a Comment