Fahamu ukweli kuhusu elimu ya nyota na utabiri, chuma ulete

JE, unazungumzaje kuhusu “chumaulete” ambapo inasemekana pesa za mtu mmoja zinaweza kwenda kwa mwingine kwa kufanya ushirikina?

Jibu: Habari za “chumaulete” ni uongo wa kifukara. Ni uongo ambao kudhihirika kwake lazima ufikiri wa kinyume. Waafrika, katika dhiki zetu na ufukara wetu huwa na hadithi za kupata mali au pesa “kwa che”. Ndiyo kisa, kati yetu hustawi habari za kupata mali kwa uchawi au ushirikina, au kwa kutumia mapepo (yaani mashetani), au kwa kutumia majini, au kwa kupitia Frimasoni na kadhalika.
Kila mara tuna maelezo ya ajabu kwa wanaokuwa matajiri kati yetu, yaani usiwe na nyumba au gari kuwazidi walio wengi mhali ulipo. Wengine tutasema ni wachawi. Wengine tutasema wanatumia mapepo au “majini” kama Waislamu waaminivyo. Wengine tutasema wanapata kwa kuwa ni wanachama wa Frimasoni na kadhalika. Kifupi, hatukosi maelezo sisi!
Kumbe, kwa sababu ya dhiki zetu, Waafrika huwa tunaaminishana kwamba kuna njia za mikato za kupatia pesa au utajiri. Hiyo ndiyo imani inayotufikisha hadi kwenye ukatili wa kuwakata ndugu zetu albino vidole au kuwaua tukiamini viungo vyao vinawezesha njia za mikato kuelekea vyeo na utajiri.
Wapi na wapi! Wazungu, Waasia na Wamerikani hawajawa matajiri kwa namna hiyo. Wenzetu waliamua kufanya mapinduzi ya viwanda na kutuzidi sisi akili katika kuzivuna malighafi zetu pamoja na kuitumia nguvu kazi yetu.
Sisi Waafrika hatuzungumzii peke yake mambo ya kupata vyeo na pesa kwa njia za mikato, bali hata kupata mazao ya mashambani, maana wapo wanaoamini kwamba mtu anaweza kuhamisha mazao, kama, mahindi, mpunga, mtama, korosho, kahawa na kadhalika kutoka mashamba ya watu wengine kwa kutumia kitu kinachoitwa kwa majina mbalimbali, kama vile, “chitola” na kwa vifaa, kama vile, vijiko au mafuvu ya watoto wachanga. 
Hapo ndipo tunapoamini pia kwamba “misukule” hutumika pia kuibia mali za watu madukani na mashambani. Ndiyo katika mstari huu tunapozungumzia “chumaulete” kwa ajili ya kuhamishia pesa za watu kimazingara. Tunapoambizana habari hizo ambazo ni hewa tupu, wote hubaki masikio na pua juu kunusanusa huko na huko ili tukutane na “zali” hilo. Matokeo ya kubweteshana katika hadithi hizo, ndiko huku kubaki kwetu katika umaskini na ufukara wa daima.
Si siri, wenzetu wa mabara mengine wanajua kwamba sisi tunalazana usingizi kwa hadithi hizo ndipo huja na kutuchukulia mali zetu za kweli: dhahabu, almasi, bati, chuma, madini ya fedha, mbao na kadhalika.
 Sikiliza. Wao wanachukua vitu vinavyoleta utajiri wa kweli, sisi wanatuacha katika hadithi na usingizi wetu wa pono. Ukitaka kujua kwamba hadithi za “chumaulete” ni hadithi hewa, jaribu kumtafuta huyo mwenye “chumaulete”. Ukishampata mwambie mkachukue pesa kwenye taasisi ya fedha, kama vile, Exim Bank, Bank of India, NMB, CRDB, Mkombozi Bank, Bank of Africa, Benki ya Posta na kadhalika.
Hapo utajishangaa mwenyewe. Kwanza siyo tu hutampata mtu huyo bali hata ukimpata tapeli mmoja anayejidai kuwa na “chumaulete” hatakubali kwenda nawe kwenye benki yoyote kwa sababu anajua anasema uongo. Na tena kwa lolote atakalokufanyia atakudai wewe malipo. Hapo ukijiuliza utajua kwamba anataka malipo kutoka kwako kwa sababu hicho kidude chake hakina uwezo wowote wa kuchukua pesa iliyotunzwa vizuri.
Mimi nilishawahi kupendekeza kwa wananchi wa nchi zote za Afrika kuwapatia marais wao au mawaziri wao wa Fedha “vyumaulete”, wanapokwenda ziarani ughaibuni. Nilipendekeza wakavitumbukize hivyo vitu kwenye Benki kuu zenye pesa nyingi kama China, Marekani, Canada, Japani, Korea ya Kusini Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Italia, Saudia, Kuwaiti, Irani, India, Singapore, Malasyia au Hong Kong ili pesa za benki hizo zije kwenye benki kuu za nchi zetu.
Haijafanyika hadi leo hii. Jambo hili lingekuwa kweli, Afrika “tungelamba dume”. Halafu nilishasema wakati mmoja kwamba hata mambo ya makinikia tusijihangaishe nayo kama kweli tuna “vyumaulete”. Tuache Wazungu wachukue madini yetu, wakayafanyie kazi viwandani mwao, mwishoni twende sisi na “vyumaulete” vyetu, tukahamishe noti na pesa zote walizochuma. Yaani mambo yangekuwa rahisi kama kumeza tonge linalosindikizwa na mlenda!
Lakini, mawazo haya yote hakuna aliyewahi kuyapokea wala kuyajaribia kwa sababu kila mtu huona jinsi yalivyo ndoto za kipuuzi. Basi, kwa kinyume, huu ndio ushahidi wangu  kwamba Waafrika tunajilisha wali kwa samaki wa picha. Nimesema tena na tena, Waafrika tu mafundi wa kusema uongo usio na tija yoyote.

Hatima
Hadithi za vyumaulete ni upuuzi usio na tija kwa yoyote yule. Nilishastaajabu jambo hili kwa sauti kubwa. Hakika, wakati wenzetu wanapofanya kweli, sisi tunabwetekea masihara! Vijana pokeeni fikra mbadala! Msiwe mwili mbichi, mawazo kama wazee wa karne ya kumi na tano!

Swali: Nini mtazamo wako kuhusu elimu ya nyota na utabiri ambavyo hurushwa kwenye vyombo vya habari  na watabiri mbalimbali wa nyota?

Jibu: Msimamo wangu kuhusu elimu ya nyota na utabiri ambavyo hurushwa kwenye vyombo vya habari  na watabiri mbalimbali wa nyota ni wa kimaandiko. Maandiko Matakatifu yanaita mambo hayo machukizo kwa Mungu Mwenyezi. Na kwa kauli hii tusipinde kushoto wala kulia. Na wala tusiseme kwa kujihurumia kwa sababu eti kwa kuwa mambo hayo yanatangazwa kwenye vyombo vya habari ni kweli na halali. 
Ni mambo ya uongo, batili na ni dhambi. Nukta. Hata ikawa mamilioni ya watu wanayahusudu, uongo hauwi ukweli kwa sababu ya wingi wa  watu wanaouamini. Na tena uongo haugeuki ukweli kwa sababu ya ukubwa na umaarufu wa matangazo yanayofanyika. Katika udanganyifu huo, Wakristo tunapaswa kuyasikiliza Maandiko ambayo pasi kigugumizi yanasema mambo hayo ni ubatili  na ni dhambi.
Kwa nini ni ubatili na dhambi? Ni kwa sababu yanavunja amri ya kwanza ya Mungu. Tusisahau kuna dhambi saba dhidi ya amri ya kwanza ya Mungu inayosema, “Mimi ndimi, Mungu Mwenyezi, Mungu wako, usiwe na miungu mingine ila mimi” (soma vyema Kut 20:2-3).
Dhambi saba dhidi ya amri hii ni hizi:  imani bila msingi, kuabudu sanamu, kupiga ramli au bao na imani katika utabiri wa nyota, imani katika uchawi (ushirikina), kutokuwa na kicho (yaani kumjaribu Mungu, kufuja matakatifu na kuuza matakatifu), kumkana Mungu pamoja na kutokuwa na msimamo juu ya Mungu.
Bila shaka hapa, unaona wazi kwamba elimu ya nyota na utabiri vipo katika hiyo dhambi ya kupiga bao au ramli. Dhambi hizi zimekemewa katika Maandiko Matakatifu kwa nukuu mbili kamambe: YbS 34:1-8 na Kum 18:9-13.
YbS 34:1-8 inasema hivi: “Mtu mjinga huwa na matumaini ya bure na ya uongo. Ndoto humpa mpumbavu mabawa ya kuruka. Kama mtu anayejaribu kushika kivuli na kufukuza upepo ndivyo alivyo mtu anayeamini ndoto. Ndoto ni kama kioo, sura inayoukabili uso. Ni kitu gani kiwezacho kutakaswa na uchafu?
Je, ukweli waweza kupatikana kwa uongo? Kupiga bao, ramli na ndoto ni upuuzi, akili huwa na mawazo kama ya mama anayejifungua. Usizitie maanani ndoto isipokuwa kama zinatoka kwa Mungu Mkuu. Maana ndoto zimewadanganya wengi na wale wanaozitumaini wameaibishwa. Sheria ni kamili bila udanganyifu huo, nayo hekima ni kamilifu kwa mtu mwaminifu.”
Kum 18:9-13 inasema, “Mtakapofika katika ile nchi awapayo Mungu Mwenyezi, Mungu wenu, msifuate zile tabia za kuchukiza za mataifa ya huko. Pasiwe na mtu yeyote miongoni mwenu atakayemchoma motoni mwanawe wa kiume au wa kike kuwa tambiko, wala mtu apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao, wala
‘mwenye kuhangaisha watu kwa mazingaombwe’, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu. Maana yeyote atendaye mambo hayo ni chukizo kwa Mungu Mwenyezi na kwa ajili ya mambo hayo ya kuchukiza Mungu Mwenyezi, Mungu wenu, anawafukuza watu wa namna hiyo mbele yenu. Muwe wakamilifu mbele ya Mungu Mwenyezi, Mungu wenu.”
Sasa sikiliza. Wayahudi walizikamata sana nukuu hizi na hivyo wakajiepusha na yote yanayoorodheshwa ndani yake. Kwa namna hiyo, wakaachana na mambo ya kuamini ndoto, kutumaini utabiri wa nyota, mambo ya kishirikina na imani zingine zinazosadifiana na hizo.  Yaani waliachana na imani zote zisizo na mbele  wala nyuma zamani kabisa, hata kabla ya Yesu kuzaliwa. Ndipo Yesu hakuwakuta watu wake  na imani za kipuuzi kama zetu.

Wazungu walifaulu kuachana nazo katika karne ya 18. Sisi Waafrika na watu wengine wa nchi zinazoendelea ndiyo bado tunazing’ang’ania na hata kujipa hatimiliki kwa kuziita “jadi yetu” au “utamaduni wetu”. Wapi na wapi!

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU