Changamoto zinatusaidia kujua umuhimu wetu nchini- Rais TEC
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Mpanda ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Gervas Nyaisonga amewataka wahitimu
waliohitimu katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT)
kukabiliana na changamoto mbalimbali watakazokutana nazo ambazo zitakuwa
kinyume na matarajio yao, na kwamba changamoto zinasaidia kujua umuhimu wa mtu
au taasisi.
Amesema hayo katika mahafali ya 20 ya SAUT yaliyofanyika katika viwanja
vya Raila Odinga chuoni hapo Desemba 7, 2018, na kusema kuwa hata SAUT
inakutana na changamoto ambazo ni kinyume na matarajio ya uanzishwaji wa chuo
hicho miaka 20 iliyopita.
“Changamoto zinatusaidia kujua tuna nguvu kiasi gani, na kujiwekea
viwango. Matarajio yenu yanaweza yasiwe sawa na mlivyotazamia. Ni sawa na
Baraza la Maaskofu lilipoanzisha vyuo
hivi. Matarajio siyo kama tunavyoona. Chuo mama SAUT kinahitimu sasa mahafali
ya 20. Kilikuwa na matarajio makubwa. Lakini mnajua kwamba tunapita katika
kipindi chenye changamoto. Lakini tunazifurahia, kwani zinatusaidia kujua kuwa
tuna umuhimu. Mtu ahangaiki na mtu mdogo. Changamoto zinatusaidia kujua tuna
ukubwa kiasi gani. Zinatuhamasisha kutafuta focus ya uhakika” amesema Askofu
Nyaisonga.
Aidha amewataka wahitimu hao waende wakaitumikie jamii kiaminifu kwa
kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto mbalimbali.
“Jamii inawategemea. Mjione kwamba ninyi ni wapambanaji, muwe mstari wa
mbele. Kishawishi kikubwa katika dunia ya leo ni kuutafuta usalama wa sasa na
kuacha usalama wa kesho. Tazama katika upana kesho yako. Hekima ni uwezo wa
kuamua vizuri masuala yanayohusu maisha na mwenendo, malengo na mbinu zake. Ni
matumizi sahihi ya maarifa ambamo ndani yake kuna elimu. Ni kinyume cha
upumbavu” ameongeza.
Amewataka kujishikamanisha na hekima kimungu kwani hekima ya kidunia
peke yake itawapotosha. Amesema kuwa kuna hatari ya kufikiri kuwa mtu
amekamilika katika hekima kumbe tu amebaki katika hekima ya kidunia.
“Si haba ukakuta mtu na elimu yake yote akasema ipo ndoa ya jinsi moja.
Akasimama na kuthubutu kusema kuwa hii ni haki kabisa. Hii ni hekima ya kidunia
lakini imepungukiwa na hekima ya kimungu. Ziko nchi ambazo wanapeleka muswada
wa kuhalalisha mambo haya. Ukiyapima unaona kuna upungufu mkubwa wa hekima.
Mnahitimu nyakati hizi ambazo zinatambulishwa na kasi ya maendeleo, ugunduzi na
mahusiano. Ni vizuri mjue kwamba mnaenda kwenye mapambano” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la chuo cha SAUT ambaye pia ni
Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala amewataka wahitimu hao wakawe
afanyakazi mahsusi, wabunifu, wakarimu, wenye kuheshimu taratibu za kazi,
kuheshimu utu na kuwajali binadamu wengine hasa wale walio wanyonge.
“Taifa linawaangalia na kuwategemea. Msisite kutumia ujuzi kusaidia na
kuhakikisha taifa letu linajengwa na linasonga mbele na katika dira zinazowekwa
katika nchi hususani dira ya viwanda” ameeleza.
Comments
Post a Comment