Askofu Nyaisonga atuma salamu za Noeli Mwaka Mpya

+  Asema Noeli ni uhai si mauaji ya watu na mazingira
+  Aitaka serikali kuboresha huduma ya afya nchini

  Na Suzan Kaneka- Mpanda
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Askofu Gervas Nyaisonga ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda amewata wananchi wote nchini Tanzania kutunza mazingira.
Ameyasema hayo mapema hii leo wakati akitoa salamu ya sikukuu za  Krismas na mwaka mpya 2019 ambapo amesema kuwa sherehe hizi zinatukumbusha kuyaishi mafumbo ya kuzaliwa kwawetu Yesu Kristo, kuzaliwa upya na kupata uzima mpya.
“Noeli ni sikukuu ya kuadhimisha uhai kwa kuuthamini kuulinda, kuutetea na kuuheshimu uhai wa mwanadamu hivyo tuadhimishe sikukuu ya Noeli kwa kuyarudia maagano yetu” amesema Baba Askofu
Nyaisonga amesema  kuwa uhai unategemea mazingira mazuri yanayomuwezesha binadamu kuishi, hivyo amewataka waumini kutunza mazingira , kuyalinda mazingira kuwa kutokata miti hovyo, kutoharibu vyanzo vya maji kwa kuchunga maeneo ya vyanzo maji na kupiga marufuku kilimo katika maeneo ya vyanzo vya maji.
Ameeleza kuwa mwanadamu anahitaji maji safi, hewa nzuri na chakula ili uhai wake uwe bora siku zote.
Sambamba na hayo amewasihi wananchi kupambana dhidi ya ugonjwa wa ukimwi kwa kujilinda, kupima na kujua afya zao, kutowanyanyapaa waathirika wa ugonjwa wa ukimwi bali kuwalinda kwa kuwapatia mahitaji muhimu na kuishi nao kwa upendo.
Hata hivyo katika kuendelea kuulinda uhai wa mwanadamu amewasihi viongozi wa Serikali hasa upande wa Idara ya Afya kuboresha mazingira ya vituo vya Afya ili wagonjwa wapatiwe huduma katika mazingira yaliyo bora, na ametoa ushauri kwa wauguzi kutoa elimu kwa akina mama wajawazito na wanaonyoyesha juu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na namna ya kijikinga.
Amewasihi waamini kupinga vikali ukatili unaojitokeza katika msimu wa sikukuu kwa kupigana na kuchomana visu, kunywa pombe kupindukia vitendo vinavyokatisha uhai wa mwanadamu tendo linalokwenda kinyume na maadhimisho ya Sikukuu ya Noeli.
Mwisho Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga amewataka waamini wakatoliki kote nchini  kuzaliwa pamoja na Yesu Kristo kwa kujiweka tayari kiroho  na kuyafuta makosa ili Mkombozi azaliwe ndani ya roho zilizosafi sambamba na kukiri Imani ya Kanisa katoliki.
“NIWATAKIE SIKUKUU NJEMA NA KRISTO AZALIWE NDANI YENU”

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU