Prof Makubi: Corona bado ipo wananchi msibweteke
MGanga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi
amewataka wananchi waendelee kuchukua
tahadhari juu ya maambukizi ya ugonjwa
wa covi 19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Prof. Makubi ameeleza hayo hivi karibuni alipokuwa anazungumza na Gazeti Kiongozi kuhusu kile kinachosadikiwa
na jamii kuwa tayari kuna dawa ya corona.
“Ninachiotaka kuwaambia wananchi ni
kwamba, hakuna dawa ya corona. Mpaka sasa dawa haijapatikana nna ile tuliyoleta
kutoka Madagascar bado inafanyiwa uchunguzi kujiridhisha.
Wananchi hawa vijana na wale waishio
vijijini wanapaswa waelewe kuwa, virusi
vya corona havibagui umri wala mahali.
Vijijini corona ipo tena ni rahisi
kusambaa hasa kwenye minada na magulio. Hivyo waendelee kuchukua tahadhari kama
zinavyoelekezwa na serikali pamoja na
wataalamu wa afya ikiwemo WHO.
Amewataka wenyeviti wa Mitaa, Vijiji, kata
nk. kuweka mikakati ambayo itawasababisha wananchi waendelee na shughuli zao za kiuchumi.
“Kwa mfano minada inaweza kuongezwa kwenye
maeneo ambayo yako wazi. Mnada wa wawanyama peke yake, wa vyakula peke yake, wa
nguo nk.
Na kila anayeingia avae barakoa. Kwa watu
wa kijijini wanaweza kujitengenezea barakoa kwa kutumia vitambaa vya cotoni
vyenye leya mbili, wawe na maji na sabuni ya kunawa mikono na kuepuka kugusana.
Wakae umbali unaopendekezwa na wataalamu,” amesema.
Amewataka wananchi waepuke mikusanyiko
isiyo na maana na kama hakuna lazima ya kwenda kwenye mikusanyiko wananchi
watulie majumbani mwao.
“Ninawashukuru wananchi kwa kuonesha
juhudi ya namna ya kujikinga wengi wanavaa barakoa, wananawa mikono hivyo
waendelee hivyo hivyo maana hakuna dawa.
Kwenye baa
waweke maji, wahudumu wanawe, wateja wanawe
Meza ziwe mbalimbali viti kadhalika,”
amesema.
Amewataka wananchi kupuuza taarifa za
uongo zinazoenea mtaani kuwa kuna dawa ama kuwa ugonjwa huu hauui, na kwamba
vijijini wapo salama.
Ugonjwa huu upo na mpokee taarifa na maelekezo
kutoka kwa serikali, wizara ya afya na wataalamu wa afya tu. Msisikilize
porojo za mtaani,” amesisitiza.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki
Rulenge Ngara Mhashamu Severine-Niwemugizi amewasisitiza waamini wa jimbo hilo
kufuata malekezo wanayopewa na serikali pamoja na wataalamu wa afya na
wasipuuzie kwasababu wapo waamini
wanaotunga maelekezo ya ugonjwa huo.
“Nina wasiwasi juu ya wananchi wanaoishi
vijijini kwani ugonjwa huu ukiingia kijijini kwa kasi wananchi wanafariki sana
kwani katika shughuli zangu za kichungaji nikipita mtaani ninaona vijiweni
wananchi hawana ile social distance(umbali kati ya mtu na mtu.
Wengine ukiwaambia kunawa mikono wanaona
ni matumizi mabaya ya maji kwani kwao
maji ni kama mali ghafi kwasababu ya ukosefu wa maji vijijini.
Amesema elimu vijijini bado inahitajika
kwa wananchi wa vijijini ambao wanauchukulia ugonjwa huu kwamba si wao,”
amesema.
Akieleza kufungua shughuli za ibada
kupitia barua yake ya kichungaji aliyoitoa hivi karibuni amewataka waamni wake
kuendelea na shughuli za ibada kwa kuchukua maelekezo yaliyotolewa na Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania.
Pia kujikinga kwa kufuata maelekezo ya
serikali na wataalamu wa afya.
Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Mwanza
Askofu Mkuu Renatus Nkwande amewataka waamini wake (Mwanza na Bunda) kuendelea
kuchukua tahadhari hasa kwa wale wanaoishi bvijijini kwamba wavae barakoa na
kunawa mikono kila wakati.
“Seikali yetu na wataalamu wa afya
wameshasema hakuna dawa ya ugonjwa huu hivyo ninawasisitiza wajitahidi kufuata
maelekezo ya serikali.
Pia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
limetoa maelekezo mbalimbali ya kujikinga kwenye ibada ,mbalimbali hayo
yazingatiwe maana ugonjwa huu kweli upo,” amesema.
Comments
Post a Comment