Tabora kuenzi ndoto za Padri Nyamiti kuanzisha chuo cha muziki

KUFUATIA kifo cha Padri Prof. Charles Nyamiti kilichotokea Mei 19, 2020 katika Hospitali ya Mt. Anna Ipuli, Jimbo Kuu Katoliki Tabora limedhamiria kuendeleza ndoto za mtaalamu huyo wa muziki hasa za kuanzisha chuo cha muziki.
Akizungumza na KIONGOZI mapema wiki hii Mratibu wa Idara ya Liturujia, Jimbo Kuu Katoliki Tabora ambaye pia ni mwanafunzi wa muziki wa Padri Nyamiti, Padri Deogratius Mwageni, amesema kuwa Padri Nyamiti alikuwa anatamani kuanzisha chuo cha muziki na yeye mwenyewe alikubali kujitoa ili aweze kufudisha nadharia ya muziki na vitendo.
“Kwa kuanzia alikuwa na wanafunzi watatu ambao ni waseminari walioko likizo na mpaka siku ya mwisho kabla ya kifo chake alikuwa anafundisha muziki. Siku hiyo ya Jumatatu alifundisha kwa muda mrefu tena bila kuchoka mpaka alipoombwa apumzike. Ndipo akaenda kupumzika kidogo na akiwa mapumzikoni hali yake ilibadilika hivyo akapelekwa hospitali na baada ya vipimo akakutwa ana malaria kali” ameeleza Padri Mwageni.
Ameongeza kuwa alilazwa hospitalini hapo ambapo alikuwa anaendelea vizuri na hata kuongoza sala kabla ya kukutwa na mauti siku ya Jumanne Mei 19.
Akitoa maoni yake kwa jinsi alivyomfahamu Padri Nyamiti, Padri Mwageni amesema kuwa Taifa linakumbwa na changamoto ya kuwafundisha wataalamu wa muziki wa Kanisa ili kuendana na matakwa ya liturujia na uhalisia wa kiafrika.
“Padri Nyamiti alikuwa mdau wa muziki wa kiafrika. Aliwahi kusema kuwa, nyimbo tunazoziimba siyo za kiafrika. Tunanakili muziki wa kizungu na akahoji kama tunaweza kufanya hivyo kwa nini tusinakili muziki wetu? Na alitoa himizo kuwa wataalamu wetu wa muziki tulionao waende vijijini wasikilize wanavyoimba, wazinakili zisipotee, na baadaye wataalamu wa mafundisho ya Kanisa watawekea mwafaka” amesimulia.
Ameongeza kuwa “Alikiri kwamba nyimbo nyingi za makabila zinakiuka mwafaka na kanuni (za kizungu). Akashauri, tunaweza kuweka nadharia zetu za kiafrika ili ziendane na mazingira yetu; kanuni ambazo zitaelezea muziki wa kiafrika.”
Kwa mujibu wa Padri Mwageni, marehemu Padri Nyamiti ameacha hazina kubwa ya vitabu vya muziki na mafundisho ya Kanisa katika lugha mbalimbali.

Wito kwa wanamuziki wa Kanisa
“Elimu haina mwisho. Kwa miaka 14 Padri Nyamiti amesoma muziki akiwa darasani. Lakini mpaka mwisho amekuwa kila siku akijifunza Piano licha ya kuwa mtaalamu mbobezi wa piano. Hii ina maana kuwa muziki ni taaluma inayohitaji kujiendeleza. Ukikaa tu kinapotea hata kile ulichonacho” amebainisha.
Aidha amewakumbusha wanamuziki wa Kanisa Katoliki kuwa uzuri na ufaulu wa muziki katika liturujia una mizizi yake katika kufanya maandalizi ya kutosha na kujifunza badala ya kubweteka.
“Kiburi kimetuharibu. Walimu wengi hatutaki kujiendeleza na kuelekezwa. Yeye daima alikuwa msikivu na alipenda kuelekezana kwa hoja. Muziki ni taaluma, hakuna mwenye umiliki. Tujifunze kila siku” ameongeza.

TEC yatoa salamu za rambirambi
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Dkt. Charles Kitima ameeleza kuwa TEC inaungana na waamini wa Tabora kuomboleza kifo cha Padri Nyamiti aliyekuwa mhadhiri mbobezi na mahiri katika fani ya Teolojia hususani mafundisho sadikifu ya Kanisa (Dogmatics) na kutoa mchango mkubwa katika malezi ya mapadri.
“Kanisa linatambua mchango wake uliotukuka katika kuandaa wataalamu katika fani ya Teolojia akiwa katika chuo cha CUEA kwa takribani miaka 34. Padri Nyamiti alijivunia imani yake kwa Kristo katika mazingira ya kiafrika (Utamadunisho wa imani) na ataendelea kukumbukwa kwa machapisho yake zaidi ya 56 aliyoyatoa” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Padri Charles Nyamiti alizaliwa 9/12/1931 Ndala, Tabora na kupadrishwa kama Padri wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora  tarehe 15/8/1962. Mwaka 1963 hadi 1975 alikuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Louvain nchini Ubelgiji ambapo alipata digrii za uzamili katika fani za Taali Mungu (Teolojia) na muziki.
Mwaka 1976 hadi 1984 alifundisha katika Seminari Kuu ya Kipalapala. Mwaka 1984 alichaguliwa kwenda Nairobi, Kenya kwenda kufundisha chuo cha CUEA. Alistaafu mwaka 2001 ila akabaki Nairobi akiandika vitabu na kufundisha masomo ya Teolojia na Muziki katika seminari kuu ya Shirika la Mitume wa Yesu hadi mwaka jana Novemba aliporudi jimboni Tabora.
Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatikani, Padri Nyamiti amewafundisha Maaskofu kama Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam; Askofu Agapiti Ndorobo wa Jimbo Katoliki la Mahenge, Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma pamoja na Askofu Severin Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge Ngara.
Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umwangazie-Apumzike kwa amani-Amina.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI