Vyombo vya Kanisa vyatakiwa kuzipa kipaumbele habari za Covid-19
KATIKA kukabilianana Covid-19, vyomba vya habari vinavyomilikiwa na Kanisa
Katoliki, vimetakiwa kuzipa kipaumbele habari zinazohusiana na mapambano dhidi
ya virusi vya corona husani zile zinazotia matumaini, kuondoa hofu na woga kwa
wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Flavian Kasala, katika mahojiano Maalum na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza hilo, yaliyofanyika katikati ya juma jijini
Dodoma. Askofu Kasala amehimza vyombo hivyo kutumia hata lugha za asili pale
inapobidi ili kuhakikisha ujumbe unaeleweka kwa makundi yote ndani ya jamii.
“Ni kweli lazima tuwe na mashaka, lakini mashaka haya
yanatakiwa kuwa yenye matumaini…kumbe vyombo vyetu virudishe hayo matumaini
kwamba binadamu anaweza kupigana vita na kushinda na hili ndilo wazo letu
kubwa,” amesema.
Pia ametoa wito kwa vyombo hivyo vya habari, kuhakikisha
vinautumia ulivyo ujumbe wa TEC kuhusu ugonjwa huo wa Corona hasa kwa kuendana
na mazingira halisi ya eneo husika, ili kuufanya ueleweke kwa kila mwananchi
ndani ya jamii ambapo amependekeza kutumia hata lugha ya asili ikibidi ili
kufikia lengo hili.
“Sasa vyombo vya Kanisa Katoliki ikiwemo TvTumaini, radio
zaidi ya 15 na magazeti vina uwezo kabisa wa kuchukua ujumbe wa corona ambao
pengine umeandikwa kwenye lugha ngumu ya kitaalam na kuulainisha, ukafikia watu
kwanza kwa hali yao, umri wao, na pengine hata mazingira yao na hata kwa lugha
zao za asili … kwa sababu corona haichagui na si kwamba watu wote wanaelewa
Kiswahili fasaha kwa asilimia 100, lakini ujumbe utaeleweka zaidi na mtu
unapozungumzwa katika mila na desturi yake,” amesisitiza.
Upande wa radio na televisheni, Mhashamu Kasala amesema ni
vyema kama vyombo hivyo vitatoa ujumbe wa corana kabla na wakati wa habari ama
vipindi vingine, kwa kuweka manani kwamba kila mwanadamu ana hulka ya kupenda
kitu fulani, hivyo kupitia vipindi hivi atapata cha kujifunza juu ya changamoto
hii iliyoukumba ulimwengu.
“Kila mwanadamu ana kitu anachokipendelea…kuna anayependa
muziki, kuna anayependa nyimbo za dini na mengine mengi, hivyo kuhakikisha kila
mtu anaupata ujumbe huu, ni vyema ukawa unarudiwa mara kwa mara yaani mwanzoni
mwa kipindi, katikati na hata kama ni nyimbo ama muziki basi kila baada ya
wimbo mmoja mnaweka kibwagizo ama tangazo kuhusu corona,” ameeleza Askofu
Kassala.
Upande wa magazeti ya Kanisa hilo, Makamu wa Rais huyo wa
TEC, ameyataka kuhakikisha yanatoa habari yenye kubeba ujumbe wa corona na
kwamba ujumbe huo hauna budi kuwekwa kurasa za mbele ili uweze kuonekana kwa
watu mbalimbali, wakiwemo wale wanaonunua na wasio wanunuzi.
“Habari ziwe kurasa zambele ili hata wale wasionunua lakini
wanapita kwenye meza yalipotandazwa magazeti hayo, basi waanze kwanza kosoma
habari za corona …yaani katika pitapita yao na kusoma vichwa vya habari vya
magazeti, basi wakutane na vichwa vya habari vinavyohusiana na ugonjwa wa
corona,” amesema.
Miongoni mwa vyombo hivyo vya Kanisa upande wa radio na
majimbo husika yakiwa kwenye mabano ni pamoja na Radio Ukweli (Morogoro), Radio
Mwangaza (Dodoma), Radio Fadhila (Tunduru-Masasi), Radio Faraja (Shinyanga),
Radio Chemchem (Sumbawanga), Radio Huruma (Tanga), Radio Mbiu (Bukoba), Radio
Tumaini (Dar es Salaama), Radio Kwizera (Tulenge-Ngara), Radio Habari Njema
(Mbulu), Radio Taa Bora (Tabora), Radio Hekima (Mbinga) na Radio Maria
Tanzania.
Upandewa Magazeti ni KIONGOZI (Baraza la Maaskofu-TEC) na
TumainiLetu (Dar es Salaam) huku upande wa televisheni kanisa hilo linajivunia
TV Tumaini (Dar es Salaam)
Comments
Post a Comment