‘Kanisa haliwezi kuendelea bila matumizi sahihi ya rasilimali’
MWENYEKITI wa Mawasiliano Jamii AMECEA
Askofu Charles Kasonde amesema kuwa, utaalamu juu ya matumizi sahihi ya
rasilimali watu na fedha ndiyo chanzo cha maendeleo endelevu katika Kanisa.
Askofu Kasonde amezungumza hayo wakati
akifungua Warsha ya siku nne ya wakurugenzi wa Kichungaji na Mawasiliano pamoja
na wanahabari wa AMECEA juu ya uratibu madhubuti wa rasilimali fedha na watu
iliyofanyika katika Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia (Addis Ababa
Ethiopia).
Warsha hii ya kujifunza namna ya
kuandika miradi bora yenye vigezo ni muhimu katika Kanisa kwani wakati huu
ujuzi wa kuandika miradi umekuwa na changamoto mbalimbali ambazo bila
kuzifanyia kazi hatutaweza kuendelea.
Ni wazi kwamba tunategemea wafadhili
kupitia miradi. Wafadhili kwa sasa wamepungua na sisi waombaji tumeongezeka.
Hivyo kwa namna moja ama nyingine vigezo na masharti vimeongezeka ndiyo maana lazima tuwe na utaalamu na
ubunifu katika kuandika miradi.
Ninaamini kila mmoja akipata ujuzi huu
kama wanahabari na waratibu wa Kichungaji katika nchi zetu za AMECEA
tutapunguza mzigo wa kuendesha taasisi katika Mabaraza yetu ya Maaskofu.
Utaalamu huu hatuwezi kuukwepa kwani bado nchi zetu ni masikini hatuwezi
kujiendesha bila wafadhili wetu,” amesema Askofu Kasonde.
Aidha amesisitiza kuwa makini na wafadhili
ambao wanatuma fedha kwamba lazima baada ya kupokea fedha na kuzitumia,
anayetekeleza mradi lazima aandike ripoti iliyo na utaalamu, kwa uwazi na
uaminifu ili kuondoa maswali na mashaka kwa wafadhili.
“Kuchelewesha ripoti, kuandika ripoti
isiyoeleweka, iliyo na maswali mengi kumesababisha wafadhili kupungua kwasababu
wanaona baadhi si waaminifu wa rasilimali fedha. Ninawasihi kutumia akili zetu
kujitoa kabisa kusikiliza warsha hii ili kuleta mabadiliko katika nchi zetu na
majimbo yetu,” amesema Askofu Kasonde.
Amepongeza Ofisi ya Mawasiliano AMECEA
pamoja na ya Kichungaji kwa kuwaunganisha wanachama wa AMECEA pamoja ili kupata
elimu ya namna ya kuratibu rasilimali fedha na watu. Amesema kuwa inaonesha
uhai wa AMECEA na kuleta umoja na mshikamano kati yao kwani wote wanakabiliwa
na changamoto zinazofanana na ni vyema kushirikishana changamoto hizo ili
kuleta ufanisi katika utendaji kazi.
Askofu Kasonde ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Solwezi nchini Zambia amesisitiza uwajibikaji, uwazi,
ukweli na uadilifu katika kutekeleza miradi kwakuwa hayo yanasaidia kujenga
fursa zaidi ya kufadhiliwa tena siku za mbeleni.
Akizungumza katika warsha hiyo, Katibu
Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia Padri Abba Hagos Hayish amesema
kuwa, Baraza hilo limefarijika kupokea mkutano huo (warsha) ya namna ya
kuratibu rasilimali fedha na watu hususani miradi kwani hata Kanisa la Ethiopia
lina changamoto hizo za kutafuta fedha kwa ajili ya kujiendesha.
“Ninawashukuru kwa kuichagua Ethiopia
kufanyia warsha hii. Maaskofu, mapadri pamoja na waamini wanawapokea kwa mikono
miwili kama ndugu zao.
Mfahamu kuwa wakristo wakatoliki hapa
Ethiopia ni wachache. Hata hivyo pamoja na uchache wetu jamii ya hapa
inalitegemea Kanisa Katoliki kutoa huduma za kijamii hususani elimu na huduma
za afya.
Tunatoa huduma kwa watu zaidi ya
milioni 50, hivyo namna ya kupata rasilimali fedha ni changamoto. Kumbe Warsha
hii itawaongezea ujuzi wanahabari wetu, waratibu wetu Katika ofisi ya
Kichungaji namna ya kuandika miradi ili wapate ujuzi huo. Huu umekuwa ni muda
mwafaka kwetu,”amesema Padri Abba Hayish.
Comments
Post a Comment