Taifa kuwa na sera ya maadili
NAIBU waziri
wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Mhe. Annastazia James Wambura amesema
wizara hiyo ipo mbioni kutunga sera ya maadili ya taifa ili kuliepusha taifa na
athari zitokanazo na mmomonyoko mkubwa wa maadili.
Uamuzi huu
unakuja baada ya wadau wa habari, utamaduni na sanaa kubainisha kuwa kwa sasa
taifa linakabiliwa na changamoto nyingi katika utekelezaji wa mipango ya
maendeleo kutokana na baadhi ya watumishi wa umma na sekta binafsi kukosa
maadili ya kiuongozi na kijamii hivyo kuhitaji kuwa na sera hiyo.
Akihitimisha
mkutano wa “TUZUNGUMZE” ulioihusisha wizara hiyo na wadau mbalimbali wa
utamaduni habari na sanaa uliofanyika katika uwanja wa taifa jijini Dar es
Salaam, naibu waziri Annastazia James Wambura amesema kwa vile maoni ya wadau
yanawakilisha jamii nzima ya watanzania, wizara yake italifanyia kazi pendekezo
hilo baada ya kukusanya maoni zaidi.
“Kutokana
na kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili nchini japokuwa tulikuwa hatujajiandaa,
lakini tutashirikiana na sekta na wizara mbalimbali ili kutunga sera hii ambayo
kimsingi itakuwa jibu sahihi la maovu mengi yanayoonekana nchini hivi sasa,”
amesema
Naibu
waziri amesema kuanzia ngazi ya familia, kazini, katika sekta mbalimbali
matendo ya mmomonyoko wa maadili yapo wazi hali inayosababisha utekelezaji wa
sera za maendeleo kuwa mgumu.
“Wapo
baadhi ya wananchi ambao wana tabia za kutokuwa waaminifu kwa taifa kwa kukwepa
kulipa kodi hali ambayo inairudisha serikali nyuma katika ukusanyaji wa mapato
na kuwapatia wananchi huduma bora za kijamii, endapo sera hii itaundwa basi
matatizo kama haya yatapungua na hatimaye kumalizika”
Ametaja
baadhi ya sababu zinazosababisha mmomonyoko wa maadili kuwa ni kukua kwa
utandawazi, ukosefu wa elimu ya kutosha ya maadili katika taasisi za elimu na
kwenye jamii, kutokuwepo na sera ya maadili ya kitaifa ambapo kila mtu anafanya
anavyotaka, kutokuwepo na ushirikiano wa kutosha kwa sekta mbalimbali, baadhi
ya wasanii kuwa na tabia zisizofaa katika jamii na baadhi ya vyombo vya habari
kuandaa vipindi visivyozingatia maadili.
“Hali
imekuwa mbaya sasa ambapo taifa linaendeshwa kwa maelekezo ya mitandaoni, yale
yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii yanapewa nafasi kubwa katika maisha ya
kila siku ya wananchi hasa watoto yawe mabaya ama mazuri, hali hii imelifikisha
taifa hapa kwani badala watu wafanye kazi za kujenga uchumi na familia zao,
wamebakia kujikita katika yale yanayoandikwa kwenye mitandao ambayo huandikwa
na watu wasiokuwa na taaluma za uandishi,” amesema
Naibu
waziri amebainisha kuwa athari za mmomonyoko wa maadili ni pamoja na kupoteza
mwelekeo wa kitaifa ambapo kutokana na kukua kwa utandawazi na watoto wengi kumiliki simu za kisasa na
kutumiana taarifa mbalimbali hivyo kuibua kizazi chenye tabia zisizofaa, taifa
kupata viongozi wasio na maadili kutokana na yaliyokithiri katika jamii na
kushuka kwa uchumi kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, ulevi, ujambazi na matumizi
ya rushwa.
Hata hivyo
amewaomba viongozi wa kidini nchini kuisaidia wizara kuhamasisha suala la
maadili mema kutokana na wao kuwa kiungo kikubwa.
“Nawaomba
viongozi wa dini wote nchini muendelee kuwafundisha waamini wenu maadili mema,
hii inatokana na ukweli kuwa mnakaa nao muda mrefu, wanakiamini kile
mnachowaambia pia mna ushawishi mkubwa, endapo mtatumia fursa hiyo vyema basi
mtakuwa mteirahisishia wizara kazi.”
Wadau wa
utamaduni, habari na sanaa walioshiriki katika kikao hicho wameitaka wizara hiyo
pamoja na kutunga sera ya maadili ya taifa pia iboreshe ushirikiano na sekta
mbalimbali juu ya maadili, kuwatumia wasanii kutoa taswira ya maadili ya taifa,
idhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii na kudhibiti maadili ya baadhi ya
vipindi vya redio na luninga, jamii na wazazi watimize majukumu yao kulinda
maadili, wizara itumie vyombo vya habari kufanya kampeni ya kuboresha maadili.
kwa
kipindi kirefu kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo
juu ya taifa kutokuwa na sera ya maadili itakayofuatwa na wananchi wote hali
ambayo imesababisha athari mbalimbali katika mipango endelevu ya kimaendeleo.
Ili
kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa sera ya maadili ya taifa, Wizara imeweka
mkakati wa kukusanya maoni ya wananchi nchi nzima kwa kuandaa mikutano na
makongamano kufanikisha lengo la kuwa na taifa lenye maadili mema.
Comments
Post a Comment