MSIBA MZITO: TEC yaomboleza



BAraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC limepata pigo baada ya kuondokewa na Mkuu wa Idara ya Uchungaji Padri Galus Marandu wa Shirika la Roho Mtakatifu(C.SS.P) aliyefariki dunia Jumapili tarehe 26 Machi 2017 Jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Katika Ibada ya Misa Takatifu ya kumuaga Padri Marandu iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili TEC, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amesema Kanisa Katoliki nchini limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mtendaji mahiri na mwajibikaji mwenye ubunifu katika kuhudumia jamii.
“Katika uhai wake, Padri Marandu alikuwa mchapa kazi na alifanya kazi kwa umakini na ufanisi mkubwa. Kipindi cha miaka 15 aliyofanya kazi TEC, Padri Marandu ameacha matunda  yanayoonekana wazi na jamii inajivunia hasa kwa kuhakikisha anawajenga watu katika upendo,  amani, umoja na mshikamano kwa kuwaunganisha watu wa Dini mbalimbali kuwa kitu kimoja kwani jambo hilo si la mchezo na kwa mtu mwingne ni ngumu kufanya hivyo lakini yeye alifanikiwa,” amesema Mhashamu Ngalalekumtwa na kuongeza kuwa;
“Kwa kweli Baraza limempoteza mtu muhimu, lakini kikubwa ni kujifunza na kuenzi kazi zake alizozifanya hapa Duniani, hasa kuwaweka  watu kuwa pamoja bila kuwatofautisha imani zao, hasa katika kuendeleza tume mbalimbali alizokabidhiwa na Baraza la Maaskofu ikiwemo, Tume ya Wahamiaji na Wasafiri wa Bahari na Nchi  Kavu, Tume ya Mila na Utamaduni wa Kanisa na pia Tume ya Mahusiano na Dini mbalimbali.”
Rais huyo wa TEC amebainisha kuwa Padri Marandu alifanya vizuri zaidi pia katika ngazi ya utawala kama Naibu Katibu Mkuu wa (TEC) na Mkuu wa Idara ya Uchungaji, kazi ambazo hazitasahaulika kutokana na uwajibikaji wake mathubuti.
Askofu Ngalalekumtwa amelishukuru Shirika la Roho Mtakatifu, kumtoa Padri Marandu, kuhudumia na kufanya kazi katika Ofisi za Baraza na kuimarisha hayo yote , hasa mahusiano na dini mbalimbali jambo lililoleta tija kubwa katika Taifa la Tanzania.

Katibu Mkuu TEC azungumzia kifo cha Padri Gallus
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC Padri Raymond Saba, amesema kuwa, Familia ya Mungu nchini Tanzania imepokea msiba huo mzito kwa huzuni, masikitiko na imani kwa mapenzi  ya Mungu ambayo yametendeka ndani ya mtumishi wake Padri Gallus Marandu ambaye alianza kufanya utume wake kwenye Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania mwaka 2001 akiwa ni Katibu Mtendaji wa Idara ya mahusiano na dini mbalimbali.
“ Mwaka 2005 aliteuliwa kuwa Katibu mtendaji wa Idara ya Wahamiaji, Wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na Utamaduni. Kunako mwaka 2013 aliteuliwa kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika uhai wake, Marehemu Padri Gallus alitekeleza wajibu wake kwa weledi, uadilifu, ari na moyo mkuu, kiasi cha kuchangia sana katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania katika medani mbali mbali za maisha.”

Mwanzoni mwa mwezi Machi Padri Gallus alishiriki kwenye semina elekezi juu ya matumizi sahihi ya rasilimali watu na fedha huko Aaadis Ababa Ethiopia ambapo semina hiyo iliunganisha nchi wanachama wa Umoja Wa Wanachama Mabaraza Ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA.
Padri Raymond Saba ametoa pole kwa Maaskofu wa Kanisa Katoliki, wafanyakazi wa Sekretarieti ya TEC, wazazi wake, ndugu jamaa na marafiki, wana shirika wa Mapadri wa Roho Mtakatifu, Umoja wa dini mbalimbali na madhehebu ya Kikristo na Kanisa lote la Tanzania kwa kuondokewa na mtumishi mwema na mwaminifu ambaye bado alikuwa anahitajika katika jamii.

Askofu Eusebius Nzigilwa; Padri Marandu hakujali maslahi yake binafsi
Akitoa homilia kwenye Misa hiyo Takatifu,  Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa amesema kuwa, Padri Gallus alikuwa ni mtumishi aliyejituma kwa kuhudumia watu pasipo kujali faida yake mwenyewe .
“Mimi binafsi niliridhishwa na utendaji wake wa kazi na maaskofu walizitambua kazi na jitihada zake. Ukiona mtu anafanya kazi mahali kwa muda mrefu pasipo kuhamishwa, ujue huyo ni mtaalamu na kazi zake zinafahamika sana. Hilo ni fundisho tosha kwa kila mwanajamii na waamini, kuiga na kulienzi katika maisha yao ya kila siku, kwani wengi wanafanya kazi kwa kutanguliza faida binafsi na si ya Mungu,” amesema Askofu Nzigilwa.
Amesema kuwa, Baraza la Maaskofu, linazitambua kazi za Marehemu Padri Marandu, na kwa kawaida kuna kikomo cha kufanya kazi hizo, hasa kwa watendaji wengi waonaohudumu kwa kipindi cha miaka 6 na kuhamishiwa mahali pengine, lakini Padri Marandu alidumu kwa miaka 15, hivyo ni wazi kuwa kazi zake zilithaminika na utendaji wake ni mzuri, ndio maana Maaskofu hawakuona  kama kuna haja ya kumhamisha.
 “Ametoa mwaliko wa kuwajibika na kutenda kazi pasipo kuwa na vigugumizi, kwani wengi wanashindwa kutenda kazi vizuri kutokana na vigugumizi vyao, ambapo vinawakwamisha katika kazi nyingi za uinjilishaji, kwa kutojikabidhi kwa Kristo na kuwaasa waamini waishi kwa uzima katika kumtegemea Kristo na si nguvu zao wenyewe,” amesema Asofu Nzigilwa.
Askofu Nzigilwa, amewataka waamini na jamii kuendeleza yale yote ambayo Padri Marandu aliyafanya, hasa kuwaweka kuwa wamoja kwa kupitia dini zao japokuwa jambo hilo si la mchezo, wameona matunda  yake.
 “Sote hapa tu mashuhuda katika hilo, kuwa marehemu alipambana katika kuleta ustawi kwa kutuunganisha na watu wa Dini nyingine, lakini kubwa tutambue alikuwa akituunganisha kwa kutuletea maendeleo ya roho na mwili na daima maendeleo popote hayana dini wala kabila,” amesisitiza Askofu Nzigilwa.
Adhimisho hilo lilihudhuriwa pia na viongozi wa Dini mbalimbali, Askofu Titus Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara na Mhashamu Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa, ambaye ndiye aliyekuwa mhubiri katika Misa hiyo Takatifu pia alikuwepo Naibu Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro.
 
Historia ya Utume wake

Mwaka 1994 mpaka 1998 alikuwa ni mmojawapo wa Walezi katika Novisieti ya Shirika iliyopo Magamba Lushoto. Wakati huohuo alikuwa Msarifu wa Novisieti.
Mwaka 1998 mpaka 2002 alifanya shughuli za Uchungaji katika kisiwa cha Pemba Jimbo Katoliki Zanzibar. Wakati huohuo tarehe 11/2/2001 aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mahusiano baina ya Dini Mbalimbali. Kati ya mwaka 2002 na 2005 alihamishiwa Bagamoyo katika Jimbo Katoliki Morogoro ambapo alikuwa Wakili Paroko na Mkurugenzi wa Hija na  Makumbusho ya kikatoliki ya Bagamoyo.
Tarehe 8 Septemba mwaka 2005 aliongezewa majukumu ya kuwa Katibu wa Tume ya Wahamiaji na Wasafiri na kushughulikia mambo yanayotokana na shughuli za Tume ya Kipapa ya masuala ya Kiutamaduni na Urithi wa Kiutamaduni wa Kanisa.
Mwaka 2006 alihamishia makao yake kwenye Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mahusiano ya Dini Mbalimbali pia akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Utamaduni na Tume ya Wasafiri na Wahamiaji.
Mwaka 2013 mpaka 2016 alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Katibu Mtendaji wa Idara ya Uchungaji pamoja na kusimamia Tume ambazo alikuwa amekabidhiwa kabla.
Kati ya Aprili 2014 na Novemba 2014 alikaimu Ukatibu Mtendaji wa Idara ya CARITAS.

Kifo chake

Marehemu alipata tatizo la kuumwa takribani majuma mawili yaliyopita akiwa mjini Addis Ababa Ethiopia alipokwenda kuhudhuria semina ya uchungaji iliyoandaliwa na Umoja Wa Wanachama Mabaraza ya Maaskofu ya Afrika Mashariki na Kati AMECEA. Ingawa alipata matibabu akiwa huko, tatizo halikutatuliwa kikamilifu. Kwa hiyo aliporejea nchini aliendelea na vipimo mbalimbali na matibabu. Baada ya kutopata nafuu akapangiwa kulazwa Jumatatu ya tarehe 27 Machi asubuhi ili aweze kufanyiwa upasuaji.
Hata hivyo siku ya Jumapili tarehe 26 Machi 2017 mnamo saa 6 mchana hali ya marehemu ilibadilika ghafla. Ilibidi baadhi ya watumishi wa TEC kumkimbiza hospitali ya Temeke. Hata hivyo jitihada hizo hazikufanikiwa kwani marehemu alifariki dunia saa 6.30 mchana akiwa njiani kupelekwa hospitali. Baada ya kufikishwa hospitali madaktari walibaini kuwa Padri Gallus alikwishafariki mnamo saa 6 mchana akiwa njiani.
Marehemu anazikwa huko Usa River Seminari Jimbo Kuu Katoliki Arusha.
Mpaka anafariki, Padri Gallus Thomas Marandu alikuwa Mkuu wa Idara ya Uchungaji Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Raha ya milele umpe Ee Bwana na Mwanga wa milele umwangazie apumzike kwa amani, AMINA.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU