KANISA KATOLIKI LAENDELEA KUITUMIA IPASAVYO MITANDAO YA KIJAMII KUINJILISHA


Baba Mtakatifu Fransisko tarehe 19 Machi 2013 ameanza rasmi kutekeleza dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi wa Yesu. Papa Fransisko kama anavyojulikana na wengi, Baba wa maskini, shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wake ameendelea kuwa na mvuto mkubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia. Takwimu zinaonesha kwamba, katika mitandao ya kijamii ana wafuasi zaidi ya milioni 3. 5 na kwamba, picha za Baba Mtakatifu zinazobandikwa kwenye mitandao ya kijamii zinafuatiliwa na watu zaidi ya milioni10.
Hii inaonesha jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyotumia kikamilifu mitandao ya kijamii ili kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha, amani na matumaini kwa watu wa mataifa! Monsinyo Lucio Adrian Ruiz, Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, mwaka 2016, Baba Mtakatifu Fransisko alikutana na kuzungumza na Bwana Kevin Systrom, muasisi mwenza wa mtandao wa kijamii unaojulikana kama Instagram, unaoonesha matukio mbali mbali kwa lugha ya picha!
Baba Mtakatifu anasema matumizi ya picha kwenye mitandao ya kijamii ni sehemu ya mchakato unaopania kuliwezesha Kanisa kuwa karibu zaidi na watu, ili kuwatangazia na kuwashuhidia tunu msingi za Kiinjili kwa lugha ya picha. Hii pia ni sehemu ya katekesi endelevu na sehemu ya majadiliano kati ya Kanisa na walimwengu, tayari kujibu changamoto za maisha kwa mwanga wa Injili! Baba Mtakatifu anasema kwa njia ya lugha ya picha anataka kuwasindikiza walimwengu katika safari ya kuonja wema na huruma ya Mungu katika maisha yao, changamoto kubwa iliyofanyiwa kazi na Mama Kanisa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.
Picha za Baba Mtakatifu Fransisko zinazobandikwa kwenye mtandao wa Instagram zinagusa na kusuta dhamiri nyofu, ili kuchukua maamuzi magumu na kutenda ili kuwaonjesha wengine furaha ya Injili, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka! Picha yenye mvuto zaidi katika kipindi cha mwaka mmoja wa uwepo wake kwenye mitandao ya kijamii ni pale anaposali katika hali ya ukimya! Hapa, Baba Mtakatifu anaonesha na kushuhudia umuhimu wa Fumbo la Sala katika maisha ya mwamini kama kielelezo cha majadiliano ya kina kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu, kwa maneno machache hii ni taalilimungu ya mwili inayoungamwa katika hali ya kawaida kabisa.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliwahi kusema kwamba, kuna mamilioni ya watu, hasa vijana wa kizazi kipya wanaoishi katika ulimwengu wa digitali. Hawa pia wanapaswa kutangaziwa na kushuhudia Habari Njema ya wokovu, changamoto endelevu kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, linatumia fursa mbali mbali za maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii kuwafikia watu huko waliko, tayari kuwaonjesha ile furaha ya Injili. Ni wajibu wa Kanisa kujifunza lugha na mawasiliano ya watu wa Kidigitali, ili kuwakutanisha na Kristo Yesu katika maisha yao.
Hii ndiyo dhamana inayojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho ambalo limemwezesha Yesu kuwa kati pamoja na watu wake hadi ukamilifu wa dahali. Wadau mbali mbali wa tasnia ya habari wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, haki na amani duniani. Kufahamu lugha ya watu wanaoishi katika mfumo wa mawasiliano ya kidigitali kwanza kabisa kuna haja ya kujifunza lugha yao anasema Monsinyo Lucio Adrian Ruiz ili kuwashirikisha ujumbe wa furaha, upendo na matumaini! Kwa wale wanaotaka kutembelea akaunti ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Instagram wanaweza kutumia anuani ifuatayo: @Franciscus.

Pia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limejikita katika mitandao ya kijamii: tovuti www.tec.or.tz, Blogu www.tec1956.blogspot.com, youtube TEC STUDIO, facebook Tanzania Episcopal Conference, instagram barazalamaaskofu pia twitter

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI