Kanisa Katoliki Musoma kupambana na ukatili wa kijinsia

ASKOFU wa  Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila, ambaye ni mwenyekiti wa  Mara Alliance ameahidi kupambana na ukatili wa kijinsia unaosababisha watoto kukatisha masomo.
Askofu Msonganzila ametoa ahadi hiyo mbele ya aliyekuwa mke wa Nelson Mandela Mama Graca Machel wakati wa kikao cha kupokea  taarifa ya  utafiti  wa Mradi wa watoto waliopo nje ya mfumo wa shule, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika  jengo la Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mradi  unaotekelezwa na Mara Alliance kwa kushirikiana na Mama Graca Machel Trust(GMT) na Serikali.
 Amesema kuwa mbali na kuwepo kwa changamoto ya watoto kuacha shule au kutokuwa kwenye mfumo wa shule kutokana na umasikini, maradhi na nyinginezo, suala la ukatili  wa kijinsia ndani ya mkoa wa Mara limekuwa ni changamoto kubwa.
“Mara imesheheni mimba na ndoa za utotoni pamoja na mila kandamizi ya ukeketaji ambayo inasababisha  watoto wengi kuwa nje ya mfumo wa shule.
Kanisa limekuwa likipambana  na ukatili huu siku hadi siku na sasa kupitia mradi Kanisa Katoliki mkoani hapa linaahidi kushirikiana na Mara alliance  na serikali kwa ujumla katika kupambana na mila potofu.
“Elimu ndiyo injini ya maendeleo, kupitia elimu mtoto wa kike wa mkulima anaweza kuwa daktari na mtoto wa mkulima anaweza kuwa Rais wa Taifa.  Watoto hawa walioko nje ya mfumo wa shule wakipata elimu wanaweza kutimiza ndoto zao na wakabadili  historia ya maisha yao” amesema Askofu Msonganzila
 Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa hiyo ambayo jumla ya watoto walioko nje ya mfumo wa shule zaidi ya milioni moja ndiyo waliotambuliwa hadi sasa, Mwasisi wa Mradi huo,  Mke wa aliyekuwa Raisi wa Msumbiji Samora Machel na Rais wa Afrika Kusini  Nelson Mandela ,Graca Machel amesema kuwa amelipongeza Kanisa Katoliki kwa mfumo mzuri  waliouunda  unaoshirikisha taasisi mbalimbali za dini na kijamii  zilizojikita  katika jamii moja kwa moja kusaidia kutekeleza mradi huo.
 Machel amesema kuwa  Kanisa Katoliki lina mfano mzuri wa kuigwa na jamii zingine hasa katika kupambana na suala zima la ukatili hasa kwa watoto wa kike  ambao ndiyo wanaoonekana kukosa fursa mbalimbali za elimu kutokana na kukatishwa masomo kwa sababu ya mimba za utotoni na ndoa za utotoni.
Aidha, Mwanzilishi wa Memkwa nchini Tanzania Dk Naomi Katunzi amesema kuwa watoto hawa waliotambuliwa ndani ya mradi huo,wanatarajia kuanza masomo yao rasmi Aprili 1 mwaka huu na kwamba hadi sasa jumla ya vituo  215 ndani ya mkoa wa Mara vimeshapatikana kwa ajili ya kuanza kufanya  masomo kwa watoto hao,na vituo vingine vitaendelea kuongezeka kulingana na idadi ya wanafunzi.
Meneja Mradi Mkoa wa Mara Godfrey Wawa  amesema kuwa suala la  uchumi ndani ya familia linatakiwa kushughulikiwa ili kuwapatia  nafasi watoto wengi kuwa ndani ya mfumo wa shule kwani utafiti unaonyesha kuwa changamoto za watoto wengi kuwa  nje ya mfumo wa shule zinatokana na umasikini na wengine kupewa kujumu la kutunza familia kwa maana ya wazazi baada ya kufanyishwa shughuli ndogondogo za biashara.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI