WAWATA: Wanaume ndio chanzo cha kutoshiriki makongamano
Umoja
wa Wanawake Wakristo Wakatoliki Tanzania WAWATA
Jimbo Katoliki Ifakara wamewalalamikia wanaume kuwa ndio chanzo cha
kuwakwamisha wanawake kushiriki makongamano pamoja na kushiriki katika kazi
mbalimbali za Kanisa.
Hayo
yamebainishwa wakati wa kongamano la WAWATA Jimbo Katoliki Ifakara
lililofanyika katika Parokia ya Mofu kuanzia tarehe 6 mpaka siku ya kilele cha
maadhimisho ya siku ya Mwanamke Duniani tarehe 8 Machi.
Katika
risala ya wakinamama hao iliyosomwa na
katibu wa WAWATA Jimbo Katoliki Ifakara Bi Longina Mbano mbele ya naibu Askofu
wa Jimbo Katoliki Ifakara Padri Bonaventura Mchalange, wamesema kuwa kuna
baadhi ya wanaume wamekuwa changamoto kwa kutowaruhusu wake zao kushiriki
makongamano pamoja na vikao mbalimbali.
Aidha Bi
Longina amesema kuwa changamoto nyingine inayowakabili ni mawasiliano magumu
kutoka jimboni kwenda kwenye parokia kadhaa hivyo kufanya taarifa nyingi
kushindwa kufika kwa wakati.
Kutokana
na changamoto hizo WAWATA wamemwomba naibu Askofu wa Jimbo Katoliki Ifakara na
maparoko kuwaunga mkono ili kufikia malengo waliyojiwekea katika kumwinua
mwanamke na kumfanya kuwa mtegemezi wa Kanisa.
“ Baba
naibu wa Askofu tunaomba utusaidie kutoa elimu kwa wanaume kupitia kwa maporoko
ili kuweza kuwapa ruhusa wake zao kuja kushiriki nasi katika makongamano, pia
tunaomba maparoko na waumini wote jimboni kutuunga mkono katika kongamano la
kanda ya Mashariki litakalofanyika Jimboni Ifakara kuanzia tarehe 23-26 Juni mwaka huu’’ amesema
Bi, Mbano.
Naibu
Askofu amesema yeye na mapadri wenzake na hasa maparoko watashirikiana
kuhakikisha wanaume wanathamini umuhimu wa mwanamke katika Kanisa la Mungu.
‘’
Mwanamke ndio msingi wa Kanisa la Mungu kwani kila kiumbe huzaliwa na mama
yake, hivyo viongozi wa Parokia, vigango na Jumuiya mhakikishe mnakuwa imara kwa ajili ya kutetea
haki ya wakina mama hawa,’’ amesema Naibu wa Askofu Padri Mchalange.
Naye
Paroko wa Parokia ya Mofu Padri Markus Mirwatu ameupongeza uongozi wa WAWATA
Jimbo kwa kufanyia maadhimisho hayo katika Parokia ya Mofu kwani imekuwa chachu
ya kuwainua wanawake ndani ya Parokia hiyo.
‘’Nawaombeni
WAWATA Jimbo tushirikiane kuwainua wanawake hawa wa hapa Mofu ambao siku zote
wanaamini kuwa wao si kitu katika Kanisa hivyo nataka watambue kuwa wao ni bora
sana na waifanye kazi ya Mungu hasa ya
uimbaji kwaya kanisani,’’ amesema Padri Mirwatu.
Kongamano
hilo la WAWATA Jimbo Katoliki Ifakara limefanyika kwa siku 3 katika Parokia ya
Mofu na kuhudhuriwa na wanawake takribani 385 kutoka katika Parokia zote 23 za
Jimbo ambapo wamepatiwa elimu juu ya mambo mbalimbali kutoka kwa wakufunzi
ambao ni Mapadri Godfrey Hongo Paroko wa Chita na Florence Mkenda (OFM Cap)
Paroko wa Mbingu.
WAWATA hao
walitembelewa na Mheshimiwa Susan Kiwanga Mbunge wa Jimbo la Mlimba ambaye
aliwataka kuongeza juhudi katika kujiletea maendeleo kwa lengo la kupunguza
umaskini.
Wanawake
Wakatoliki Jimbo Katoliki Ifakara wameshirikiana na wanawake wenzao duniani
kote kuadhimisha siku ya Mwanamke Duniani kwa kufanya kongamano hilo huku mwaka
2018 wakipanga kufanya kongamano katika Parokia ya Kisawasawa Dekania ya
Kilombero.
Comments
Post a Comment