Hospitali ya Mt. Fransisko Ifakara yazindua jengo kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD).
Hospitali ya
Rufaa ya Mtakatifu Fransisko Ifakara inayomilikiwa na Jimbo Katoliki Ifakara
imezindua jengo maalumu kwa ajili ya idara ya huduma kwa wagonjwa wa nje yaani
OPD, ambalo limejengwa na serikali ya Uswisi kupitia shirika lake la maendeleo
la SDC.
Jengo hilo ni
moja kati ya mengi yaliyojengwa na mengine kufanyiwa ukarabati katika hospitali
hiyo kuanzia mwaka 2012 na limefunguliwa na Mheshimiwa Manuel Sager ambaye ni
Balozi wa Uswizi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo na uhusiano la Uswisi
(SDC).
Pamoja na
ujenzi wa jengo hilo na ukarabati wa majengo mengine, Shirika la SDC linaendelea
pia kuboresha miundombinu mingine ya Hospitali
hiyo ili kuwezesha utolewaji wa huduma za afya katika hospitali hii kuwa
rahisi, bora na ufanisi zaidi huku ikihudmia wagonjwa wapatao milioni moja kwa
mwaka kutoka katika mkoa wa Morogoro na mikoa jirani.
Akiongea
katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo, Askofu wa Jimbo Katoliki Ifakara
Mhashamu Salutaris Libena ameishukuru Serikali ya Uswisi na shirika lake la
maendeleo pamoja na Ubalozi wa Uswisi Tanzania kwa kuwezesha ujenzi na
ukarabati wa majengo mbalimbali ya hospitali hiyo.
“Tunaishukuru Serikali ya Uswisi kwa
kushirikiana nasi, na tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu mpaka kizazi
kijacho, tunaahidi kutekeleza na kusimamia yote tunayokubaliana kwa lengo la
kuendeleza muungano huu, lakini pia kazi kubwa iliyofanyika hapa ni mchango
mkubwa kutoka kwa Serikali na watu wa Uswisi hasa katika nyanja ya afya,” amesema Askofu Libena.
Katika hotuba
yake Mheshimiwa Balozi Sager amezipongeza juhudi za wote walioshiriki kuiboresha
hospitali hiyo huku akisema ana uhakika kazi hiyo itaendelea katika maeneo
mengine ya hospitali na kwamba anaona fahari kwa Serikali ya Uswisi kuweza
kuboresha sekta ya afya kwa Watanzania hususani jimboni Ifakara.
“Jengo hili
ni sehemu moja kati ya nyingi zinazohitajika ili kutoa huduma bora za afya kwa
jamii, rasilimali watu wenye ujuzi na ufanisi wa kiutendaji wa shirika pia ni
sehemu muhimu katika uboreshaji wa huduma za afya, pia nashukuru kwa heshima
kubwa mliyonipa ya kuzindua jengo hili la OPD na kuwekwa kumbukumbu ya jina
langu kwenye ukuta wa jengo hili.” Amesema Balozi Sager.
Naye Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro Dr Kebwe Steven Kebwe amesema anaheshimu mataifa yote
yanayotoa misaada nchini na kuliomba Taifa la Uswisi kutositisha msaada na
ushirikiano na Tanzania katika maeneo mbalimbali kama ilivyo katika Mkoa wa
Morogoro.
Hafla hiyo
imefanyika katika viwanja vya Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mt.Fransis Ifakara na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dr Kebwe
Steven Kebwe, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bwana James Ihunyo, Askofu wa Jimbo Katoliki
Ifakara Mhashamu Salutaris Melchior Libena, Balozi wa Uswisi Nchini Tanzania
Mheshimiwa Florence Tinguely Mattli, Mkuu wa idara ya maendeleo na ushirikiano
wa ubalozi wa Uswizi Bi, Romana Tedeschi
pamoja na Mkuu wa Sekta ya Afya wa Ubalozi wa Uswisi Dr. Thomas Teuscher.
Taifa la
Uswizi na Jimbo Katoliki Ifakara yana historia nzuri ya mahusiano inayokaribia
karne moja kwa sasa na hospitali ya Mtakatifu Fransisko na taasisi zingine za
Mafunzo na utafiti zilizopo Ifakara zimekuwa zikishirikiana na taasisi
mbalimbali za Uswisi zikiwemo Swiss Tropical and Public Health Institute (Swiss TPH) pamoja na Solidar Med.
Aidha
kupitia ushirikiano huo kati ya Uswisi na Tanzania Shirika la SDC la nchini Uswisi limechangia
Shilingi Bilioni 17 au Dola za Kimarekani Milioni 7.8 kwa Kipindi cha Miaka
Mitano kuanzia Mwaka (2012 - 2017) ili kusaidia mpango mpana unaojumuisha
ujenzi na ukarabati wa majengo ya Hospitali, ununuzi wa vifaa vya matibabu,
uboreshaji wa mifumo ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT),
pamoja na uboreshaji wa huduma za afya utawala na usimamizi.
Kwa sasa Hospitali
ya Mt. Fransisko ina uwezo wa kulaza zaidi ya wagonjwa 370 na inatoa huduma
mbalimbali za afya ikiwa ni pamoja na huduma za madaktari bingwa huku ikiwa
miongoni mwa hospitali 10 zinazomilikiwa na Mashirika ya Kidini ambazo
zilipandishwa hadhi na Wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto
na kuwa Hospitali ya rufaa katika ngazi ya Mkoa Mwaka 2012.
Comments
Post a Comment