“Viongozi wa Dini elezeni ukweli vita ya dawa za kulevya”

VIONGOZI wa dini nchini wameaswa kupaza sauti zao katika mambo mbalimbali yanayoendela, badala ya kuongea chini chini hasa wakati huu taifa linapoendelea kupambana na utokomezaji wa dawa za kulevya. Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Same Mhashamu Rogathy Kimaryo wakati wa Misa Takatifu ya kuzindua Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara kwa upande wa Bagamoyo.
“Ni lazima tuwafundishe vijana wetu unyenyekevu na ukweli. Hii vita ya dawa za kulevya, kwani tumeianza jana? Tulikuwa wapi siku zote? Mambo ya dawa za kulevya na watumishi hewa siyo mambo ya ghafla, fanyeni tafiti kwa nini jamii imekengeuka?” amesema.
Amewaasa viongozi wa dini kutokuwa waoga katika kupaza sauti na kuongea ukweli pale inapobidi ili kulinusuru taifa.
“Tusipoziba ufa tutajenga ukuta, hii ni hekima ya waswahili. Viongozi wa dini tusiongee chini chini, tuongee vitu visikike. Tusidharau chochote tuheshimu viongozi wetu, lakini tuwaambie ukweli kwamba haya mambo ya dawa za kulevya hayajaanza jana wala juzi, yapo tangu zamani sasa unashangaa nini sasa hivi,” amesema Askofu Kimario.
 Wakati huo huo, Askofu Kimaryo amewataka viongozi wa dini kueneza neno la Mungu kwa busara na unyenyekevu bila kuweka majivuno ndani yake ili liweze kuwasaidia waamini.
 Askofu kimario ameongeza kuwa shughuli za viongozi wa dini zinapaswa kulenga kumuinua binadamu katika hadhi yake bila kusahau au kupoteza misingi thabiti ya utume waliokabidhiwa na Mwenyezi Mungu.
 “Shughuli za viongozi wa dini zinapaswa kulenga kumwinua binadamu katika hadhi yake bila kusahau au kupoteza misingi thabiti ya utume na kuyatekeleza maono waliokabidhiwa na mwenyezi Mungu,” amesema Askofu Kimaryo.
 Aidha Askofu Kimaryo amesema kuwa kwa sasa waamini wanakabiliwa na uelewa mdogo wa imani, hivyo wanapaswa kujiwekea misingi ya kulisoma neno la Mungu kulitafakari na kulichambua badala ya kuogopeshwa na watu wasiokuwa na mapenzi mema juu ya imani na sheria za Kanisa Katoliki.
Sanjari na hayo amefafanua kuwa siyo vyema viongozi wa dini kuficha imani yao, bali jukumu lao kubwa ni kuonesha unyenyekevu na kutetea ukweli badala ya ubaya mara baada ya kutokea dosari mbalimbali katika taifa.

 “Siyo vyema viongozi wa dini kuficha imani yao au kutetea uovu wa aina yoyote, bali jukumu letu kubwa ni kuonesha unyenyekevu na kutetea ukweli badala ya ubaya mara baada ya kutokea dosari mbalimbali katika Taifa,” amesema Askofu Kimaryo.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI