BIASHARA HARAMU YA BINADAMU: VATICAN YAENDELEA KUPAMBANA NAYO
Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni kati ya changamoto kubwa zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwani takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya watu milioni 45 ambao wametumbukizwa katika biashara hii inayozalisha kiasi cha dola za kimarekani bilioni 32 kwa mwaka na hivyo kuchuana kwa karibu sana na biashara haramu ya silaha na dawa za kulevya duniani. Wanawake, wasichana na watoto wadogo ndio walengwa wakubwa katika biashara hii na wengi wao ni wale wanaotoka katika nchi za Amerika ya Kusini, Afrika na nchi za Ulaya Mashariki ambazo kwa miaka mingi zilikuwa chini ya utawala wa Kikomunisti.
Sababu kubwa zinazopelekea watu kujikuta wanatumbulizwa kwenye biashara haramu ya binadamu ni umaskini wa hali na kipato, unaowawadanganya watu hawa kwamba, watapata fursa za ajira na hivyo kuondokana na hali yao duni, lakini wanapofika huko wanakopelekwa, wanajikuta wakiwa wametumbukizwa kwenye utumwa mamboleo kiasi kwamba, hawana tena uwezo wa kurejea nchini mwao. Ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita, njaa na magonjwa; watu walioathirika kutokana na mipasuko ya kidini, kijamii, hali ngumu ya maisha na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Lakini, sababu kubwa zaidi ni watu kufilisika kimaadili na kiutu kutokana na kuelemewa na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa wakati alipokuwa anatoa hotuba kwenye Chuo kikuu cha Fordham, kilichoko nchini Marekani kuhusiana na jitiahada za Vatican katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu inayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Mapambano haya yamepewa kipaumbele cha pekee katika utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Biashara ya binadamu si wazo la kufikirika bali ni hali halisi inayogusa mamilioni ya watu duniani.
Hawa ni wale watu wanaotumbukizwa kwenye biashara na utalii wa ngono; biashara ya viungo vya binadamu; ndoa shuruti na kazi za suluba kwa watoto wadogo ambao wakati mwingine wanapelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita. Watoto hawa wakati mwingine wamekuwa ni kafara wa imani za kishirikina sehemu mbali mbali za dunia. Wakimbizi na wahamiaji wamejikuta hata wao pia wakitumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu. Taarifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015 zaidi ya watu milioni 65 walilazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, kinzani, mipasuko ya kijamii, kidini, dhuluma na nyanyaso mbali mbali zinazojikita katika uvunjwaji wa haki msingi za binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 alipokuwa anahutubia kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati katika kipambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; kwanza kabisa kwa kulinda na kuheshimu haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Pili kwa kusimama kidete kupambana na umaskini wa hali na kipato na tatu ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vatican daima imekuwa mstari wa mbele kupambana na biashara haramu ya binadamu ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Vatican inaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuridhia Itifaki ya Umoja wa Mataifa katika mchakato wa kupambana na biashara haramu ya binadamu, kwani ni biashara inayowanyanyasa watu zaidi ya milioni 36. Ndiyo maana Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa aliwataka viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha utashi wa kisiasa katika mapambano haya. Kanisa Katoliki pamoja na taasisi zake mbali mbali limeendelea kujipambanua kuwa ni kati ya wadau wakuu wanaopambana na biashara haramu ya binadamu pamoja na kuwasaidia waathirika ili waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida. Utumwa mamboleo unaendelea kukua na kukomaa, kumbe, unahitaji watu kulitambua hilo na kuchukua hatua madhubuti, hii ikiwa ni pamoja na kubadili mtindo wa maisha. Ikumbukwe kwamba, mafanikio katika maisha yanapatikana kwa juhudi na maarifa, kwa kujinyima na kujiwekea malengo thabiti. Serikali mbali mbali zinapaswa pia kujizatiti katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kwa kuwapatia mahitaji msingi.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, ndiyo maana kunako mwaka 2015 alipokuwa anazungumza na mabalozi pamoja na wawakilishi wa nchi na mashirika mbali mbali mjini Vatican aliwataka kuhakikisha kwamba, wanasaidia katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kikundi cha Mtakatifu Martha kilianzishwa katika jitihada hizi za Baba Mtakatifu Francisko kuwahusisha wadau mbali mbali katika mapambano haya na kwamba, cheche za mafanikio anasema Askofu mkuu Auza zinaanza kuonekana, ingawa bado Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe ili kweli biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo viweze kupewa kisogo!
Baba Mtakatifu hivi karibuni akizungumza na wajumbe wa RENATE, yaani Mtandao wa Mashirika ya Kitawa Kimataifa katika Mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu alikaza kusema, utumwa mamboleo ni matokeo ya umaskini, ukosefu wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; ubaguzi na ukosefu wa elimu, fursa za ajira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kumbe, hata utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya utumwa mamboleo na kwamba, huu ni utashi wa kimaadili unaopaswa kufanyiwa kazi na wadau mbali mbali duniani.
Askofu mkuu Bernardito Auza anasema, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kujiwekea malengo ya kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kama sehemu ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Kanisa litaendelea kujizatiti katika mapambano haya sanjari na kuwasaidia waathirika kama sehemu muhimu sana ya huduma kwa maskini na wanyonge sehemu mbali mbali za dunia; kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Ni matumaini ya Vatican kwamba, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa pamoja na wadau mbali mbali wataunganisha nguvu na utashi wao wa kisiasa na kimaadili, kwa hakika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo vitaweza kupewa kisogo. Hivi ndivyo Askofu mkuu Bernardito Auza, anavyohitimisha hotuba yake kwenye Chuo Kikuu cha Fordham kuhusu mchango wa Vatican katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, changamoto inayovaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
Ni vema sana Kanisa kujizatiti katika ukombozi wa mtu. Hongera Kanisa Katoliki kupambana na hili janga haramu la usafirishaji holela wa binadamu. Tuendelee na moyo huu kwani binadamu kwa kuumbwa kwake anahitaji ukombozi wa kiroho na kimwili.
ReplyDelete