Sudani inahitaji msaada wetu nchi za AMECEA: Rais wa AMECEA asisitiza

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanachama Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki (AMECEA), Mwadhama Berhaneyesus Kardinali D. Souraphiel, wa Addis Ababa Ethiopia amesisitiza nchi wanachama wa AMECEA kuisaidia Sudani Kusini  kwa sala na majitoleo mbalimbali ili vita vikome nchini humo.
Kardinali  Souraphiel amesema hayo hivi karibuni wakati akifunga Warsha kuhusu namna ya uratibu madhubuti wa rasilimali fedha na watu pamoja na kuandika miradi kwa ufasaha iliyoandaliwa na Idara ya Mawasiliano na Kichungaji AMECEA kwa wanahabari pamoja na Makatibu wa Idara za Uchungaji  nchi wanachama wa AMECEA  iliyofanyika katika Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia –Addis Ababa kuanzia 9-12 Aprili mwaka huu.
Kardinali Souraphiel amesema kuwa waamini wa Kanisa Katoliki Afrika hususani nchi wanachama wa AMECEA kuguswa na mahangaiko ya waamini wa Sudani na Sudani Kusini kwa kuwapokea wageni kutoka nchi hizo, kuwasaidia kusali na kuhamasisha mazungumzo ya amani.
“Nchi hizi mbili kwa kweli zinahitaji maombi yetu. AMECEA iliweka Tume ya umoja na mshikamano ambayo tayari imeanza kazi. Baadhi ya wajumbe wa Tume tayari alitembelea Sudan Kusini kukutana na kujadili na wadau mbalimbali wa Kanisa na viongozi wa serikali juu ya ujenzi wa amani,” alisema na kuongeza kuwa “Wakati fulani kabla Sudan Kusini haijapata uhuru wao, sisi tulituma wajumbe wakiongozwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wa Tanzania  kwenda katika jimbo la Rumbek kukutana na wawakilishi wawili kutoka serikalini na viongozi wa Kanisa Katoliki ili kujadili namna ya kupata suluhu ya mafarakano.
Wakati Sudan Kusini ilipopata uhuru sisi pia tulimtuma mjumbe mwingine kuonyesha mshikamano wetu. Kwa bahati mbaya miaka miwili baadaye wakarudia vita tena, “Kardinali Berhaneyesus ameeleza.
Aidha amesikitishwa na viongozi wa serikali wa pande zote mbili kukataa mazungumzo ya amani huku wakiendelea kuwatesa wananchi wao hususani watoto, wazee na akina mama.
“Kwa sasa nchi ya Sudani na Sudani Kusini ina idadi kubwa ya wakimbizi hivyo nchi za AMECEA mtoe ushirikiano kadri iwezekanavyo ili kuwapa faraja wenzetu waliopo katika mateso,” amesisitiza.
Hata hivyo amesikitishwa na kukosa wajumbe kutoka Sudani  katika warsha hiyo pevu ya rasilimali akisema hata shughuli za kichungaji zinakwama kwasababu ya vita na mafarakano.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI