Askofu Minde awataka mapadri kuwapa ushirikiano UWAKA Kahama
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Kahama Mhashamu Ludovick Minde amewataka
mapadri kuwasaidia wanaume wa Umoja wa Wanaume Katoliki
(UWAKA) kuutambua umuhimu wao katika kazi za utume na uinjilishaji ndani ya Kanisa pia juu ya kulitegemeza Kanisa kuanzia ngazi ya familia,
Jumuiya na Parokia zao.
Askofu Minde ameyasema hayo katika
misa takatifu ya kuhitimisha semina ya mafunzo ya siku 5 ya
kiroho na sala kwa viongozi
wa Umoja wa Wanaume Katoliki ( UWAKA
) Jimbo Katoliki Kahama.
Amesema mafunzo waliyoyapata katika semina hiyo juu ya umuhimu wao katika
mambo ya kiroho, sala na utume wao kwa Kanisa yawasaidie kujitambua katika kazi
za kitume juu ya kulitegemeza Kanisa.
Amesema nafasi ya UWAKA ndani ya Kanisa ni pana hivyo lazima ionekane kwa
kutimiza wajibu wao kwa matendo kuanzia kwenye familia, jumuiya, vigango,
kiparokia na kijimbo na kuwataka wawajibike katika kulitegemeza Kanisa kwa sara
na kiroho.
Askofu Minde amesema uwepo wa UWAKA ni muhimu sana ndani ya Kanisa
katika kazi za uinjilishaji na utume wa
sala na kiroho, hivyo kwa nafasi
hiyo wanapaswa wawe wa kuwajibika kwa Kanisa na familia kwa kutimiza wajibu wao na uonekane wazi.
“Utume wa wanaume wakatoliki ( UWAKA ) siyo wa kisiasa, ni utume wa kiroho
ndani ya Kanisa katika kazi za
uinjilishaji kwa sala na lazima uonekane kwa kuchukua nafasi waliyonayo ya baba kuanzia kwenye familia, Kanisa, katika
mambo ya imani ya Kanisa Katoliki,” amesema Askofu Minde.
Askofu Minde amewataka UWAKA kufungua ukurasa mpya katika maisha ya utume
wao ndani ya Kanisa kwa sifa na utukufu wa Mungu sababu yupo pamoja nao katika
kutekeleza wajibu wa nafasi waliyonayo katika mambo ya kiroho na kimwili.
Akisoma taarifa ya UWAKA ya jimbo baada ya misa Dr.Sostenes Nkombe pamoja
na kumshukuru Askofu Minde kwa semina hiyo amekiri kuwa imewapatia ari na uwezo
wa kutekeleza majukumu yote yawapasayo wanaume wakatoliki.
Dr.Nkombe amesema katika hitimisho la semina yao wameazimia kutekeleza malengo 10 ambayo ni sala, uwaka
na elimu, uwajibikaji, majitoleo, uaminifu, uwaka na utume wetu, vikao ,
uchaguzi wa viongozi, uwaka na sensa na uwaka na malezi.
Pia wameahidi kushirikiana kwa karibu na Askofu Minde, mapadri, watawa na
vyama vyote vya kitume jimboni Kahama.
Taarifa njema
ReplyDelete