MTAKATIFU BERNARDO NA MAFUNZO YAKE KWETU
Bernardo wa Clairvaux (Fontaine-lès-Dijon, Ufaransa, 1090 - Ville-sous-la-Ferté, Ufaransa, 20 Agosti 1153) alikuwa padri, abati na mwenezaji mkuu wa urekebisho wa Citeaux wa shirika la Benedikto wa Nursia.
Aliitwa “Babu wa mwisho” kwa sababu alitetea na kustawisha teolojia ya mababu wa Kanisa wakati wa kujitokeza teolojia mpya ya shule.
Ndiye mtu muhimu zaidi wa karne ya 12 katika Kanisa Katoliki, ambalo linamheshimu kama mtakatifu (alivyotangazwa na Papa Alexander III mwaka 1174) na mwalimu wa Kanisa (alivyotangazwa na Papa Pius VIII mwaka 1830).
Ni msimamizi wa wakulima.
Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 20 Agosti.
Bernardo alizaliwa huko
Fontaine-lès-Dijon, leo nchini Ufaransa, mwaka 1090. Alikuwa mtoto wa tatu kati
ya saba waliozaliwa na Teshelino na Aleta, wote wa koo bora za watawala wadogo
wa ufalme wa Borgogne
(leo nchini Ufaransa).
Alisoma hasa lugha na hoja kwa Wakanoni wa kanisa la Nôtre Dame de
Saint-Vorles, karibu na Châtillon-sur-Seine.
Kisha kurudi katika ngome ya baba yake huko Fontaines, mwaka 1111 alitawa pamoja na
ndugu zake 5 na jamaa na marafiki kadhaa katika nyumba ya Châtillon,
mpaka mwaka uliofuata akajiunga pamoja na wenzake 30 na monasteri ya
Cîteaux (karibu na Dijon),
iliyoanzishwa miaka 15 ya nyuma na Roberto wa Molesmes. Wakati
huo ilikuwa chini ya Stefano Harding, abati wa tatu.
Urekebisho huo ulishika kwa bidii sana
mashauri ya Kiinjili, hasa ufukara, bila kulemewa na mapokeo mengi ya
ziada yaliyofuatwa katika monasteri ya kawaida.
Mwaka 1115, alipokuwa na
miaka 25 tu, Stefano Harding alimtuma kuanzisha monasteri mpya, hivyo alihamia
pamoja na wamonaki
wenzake 12 katika mkoa
wa Champagne, walipozawadiwa shamba
kubwa karibu na mto Aube,
wakaliita Clairvaux, yaani bonde angavu.
Akiwa hivyo na nafasi ya kutekeleza umonaki
alivyouona yeye, alifaulu kuunganisha sala na masomo na
utendaji mkubwa. Akiangalia hali ya monasteri nyingi, alisisitiza haja ya
kuishi kwa kiasi
katika chakula,
mavazi na
majengo na ya kushughulikia mafukara.
Kwa muda mfupi Abasia ya Clairvaux ikawa
kivutio kikubwa kwa miito ya utawa hata ikaweza kuanzia mwaka 1118 kutuma wamonaki
wake kuanzisha sehemu nyingine kama vile huko Trois-Fontaines, Fontenay, Foigny, Autun, Laon. Bernardo
alipokufa abasia
za urekebisho wa Citeaux zilikuwa 343, ambazo 66 kati yake zilianzishwa au
kurekebishwa naye, kutoka Hispania hadi Siria, kutoka Italia visiwani hadi Uswedi. Mbali ya kuwa mahali pa kuishi
kidini, zilikuwa pia vyuo vya kilimo na ufundi.
Kipindi kilichotangulia mwaka 1130 Bernardo
aliandikiana sana na watu wa kila aina. Mbali ya barua hizo nyingi,
alitoa hotuba nyingi na vitabu mbalimbali.
Tangu mwaka 1130 alianza
kushughulikia masuala mengi mazito ya Kanisa na ya Upapa. Kwa ajili hiyo ilimbidi aondoke utawani mara nyingi
zaidi na zaidi hata kusafiri pengine nje ya Ufaransa, pia kwa kuanzisha
monasteri za wanawake.
Maisha yake yote Bernardo akawa
mtetezi shujaa wa imani sahihi na wa mamlaka ya Kanisa.
Katika maandishi yake ya kupinga uzushi, alimlenga hasa Abelardo, msomi mahiri aliyebuni namna mpya ya
kufanya teolojia akitumia zaidi mantiki na hoja za falsafa. Kisha
kupata hukumu ya Sinodi ya Sens ya mwaka 1140 dhidi ya baadhi
ya mafundisho ya Abelardo, hatimaye alifaulu kupatana naye kwa msaada wa Petro Mhashamu wa Cluny.
Zaidi tena alipinga Wakatari, waliodharau ulimwengu wa
maada pamoja na mwili wa binadamu, na hivyo
walimkosea shukrani Muumba wa vyote.
Kinyume chake aliwajibika kutetea Wayahudi dhidi
ya mashambulizi yaliyowapata mara nyingi zaidi na zaidi.
Miaka hiyohiyo Bernardo aliandika
vitabu vyake maarufu zaidi, kama vile Hotuba juu ya Wimbo
Ulio Bora.
Alipatanisha Wakristo (na
watawala wao) waliokuwa wanagombana. Vita
vya msalaba vya mwaka 1147 vilifanikiwa kuungwa mkono na watu wa Ufaransa na Ujerumani
kutokana na mahubiri yake.
Miaka ya mwisho alilazimika
kupunguza safari
zake, hivyo alipata nafasi zaidi kwa maandishi yake, akiyapitia upya na
kuyaongeza.
Kitabu cha pekee cha mwaka 1145 ambacho kinaitwa
“Kuzingatia” alikiandika kwa ajili ya mwanafunzi wake Bernardo Pignatelli ili
kumuongoza katika majukumu yake mapya alipochaguliwa kuwa Papa kwa jina la Eugene III. Humo unajitokeza pia
mtazamo wa dhati juu ya fumbo la Kanisa ambao kupitia fumbo la Kristo unaishia kuzama
katika fumbo la Utatu.
Mwishoni mwa mwaka 1152 alikuwa ameishiwa
nguvu, lakini alisafiri hadi Metz ili kutuliza fujo za mji huo.
Alipokuwa akirudi Clairvaux, akariki
Ville-sous-la-Ferté, tarehe 20 Agosti 1153.
Njia
ya sala ya Bernardo
Bernardo hakuelekea ujuzi unaotokana
na mantiki,
bali ule unaopatikana kwa kuzama katika mafumbo kwa sala ya kumiminiwa. Kwake
ndiyo njia pekee ya kumfahamu kweli Mungu na kufikia amani na heri ya kuwa naye.
Hivyo, akipinga teolojia ya shule iliyokuwa
inaanzaanza, alishikilia mapokeo ya Biblia, ya mababu
wa Kanisa, ya liturujia na ya umonaki, pia kwa
lengo la kulinda imani sahili ya waamini wa kawaida.
Kwake upendo mkubwa
zaidi na zaidi ndio lengo pekee la teolojia, alivyoeleza katika kitabu
“Kumpenda Mungu”. Safari hiyo ya roho ina hatua mbalimbali ambazo alizifafanua
kinaganaga na ambazo zinakamilika katika ulevi wa upendo
usiosemeka.
Tangu hapa duniani mtu anaweza
kufikia muungano
huo na Neno wa Mungu ambao Bernardo aliuita “arusi ya kiroho”. Hapo Neno
anaitembelea roho,
anakomesha ndani yake dalili za mwisho za ukaidi, anaiangaza, anaiwasha na
kuigeuza.
Fikra zetu kuhusu
mafumbo ya Mungu ziko katika hatari ya kugeuka zoezi la bure la akili zisipotegemea
imani ya dhati iliyolishwa na sala hasa katika uhusiano wa dhati na Bwana: ndiyo “ujuzi
wa watakatifu” ambao unatolewa na Roho
Mtakatifu na kuhitajiwa na teolojia.
“Ni lazima tuendelee kumtafuta Mungu
huyo, asiyetafutwa bado vya kutosha, lakini inaweza kuwa rahisi zaidi kumtafuta
na kumpata katika sala kuliko katika mijadala”. Mtume
Yohane, aliyeegama kichwa chake kifuani pa Yesu, anabaki kielelezo cha mwanateolojia na cha
mwinjilishaji bora.
Mbele ya hoja kali zilizozidi
kutolewa katika mihadara ya shule, Bernardo alisisitiza kwamba Yesu tu ni “asali kinywani, wimbo sikioni, shangilio moyoni… Lishe yote ya roho ni kavu isipolainishwa
na mafuta hayo;
haina ladha isipotiwa chumvi hiyo.
Unachoandika hakininogei nisiposoma Yesu ndani yake”.
Ndiyo sababu mapokeo yamemuita
“Doctor Mellifluus”, yaani “Mwalimu mtamu kama asali”, kwa jinsi masifu yake
kwa Kristo yalivyobubujika kwa utamu.
Pamoja naye alimmiminia sifa Bikira
Maria, kiasi kwamba miaka 150 hivi baada ya kifo chake, Dante
Alighieri alimtia mdomoni maneno haya: “Bikira Mama, binti wa Mwanao, mnyenyekevu na mkuu kuliko viumbe, shabaha maalumu ya mpango wa milele”.
Bernardo hakuwa na shaka: ni kwa njia
ya Maria kwamba tunamuendea Yesu (kwa Kilatini, “Per
Mariam ad Iesum”). Ndiyo sababu alihimiza, “Katika hatari, katika huzuni, katika shaka, umfikirie Maria,
umuitie Maria. Yeye asiache kamwe midomo yako, asibandukane kamwe na moyo wako;
na ili uweze kupata msaada wa sala zake, usisahau kamwe mfano wa maisha yake.
Ukimfuata, huwezi kusita; ukimuomba, huwezi kukata tamaa; ukimfikiria, huwezui
kukosea. Akikutegemeza, hutajikwaa; akikulinda, huna la kuogopa; akikuongoza,
hutaanguka kamwe; akiwa upande wako, utafikia lengo lako”.
Kulingana na mapokeo, Bernardo alishuhudia
kwamba Maria yuko chini ya Kristo, lakini pia alisisitiza nafasi ya pekee
aliyonayo katika mpango wa wokovu, kutokana na jinsi alivyoshiriki kikamilifu sadaka ya Mwanae.
Alimuambia hivi wakati wa kuhubiri,
“Mama mwenye heri, kweli upanga ulichoma
roho yako!… Ukali wa uchungu ulichoma roho yako kwa ndani
hivi kwamba ni haki tukuite mfiadini, kwa sababu ndani mwako ushiriki wa mateso ya Mwanao unazidi kabisa kwa
ukali mateso ya kimwili ya kufia dini”.
Katika vitabu vingi, hasa vya ufafanuzi wa Biblia, alivyoviandika,
unajitokeza upendo
hai uliomuongoza daima kama alivyoandika, “Upendo ndio nguvu kuu ya maisha
ya kiroho”.
Sala
yake
Bwana, mema yangu ni kukaa katika
tabu, mradi wewe uwe nami.
Ni bora kuliko kutawala pasipo wewe,
kula karamuni pasipo wewe, kujitukuza pasipo wewe.
Bwana, mema yangu ni kukukumbatia
wewe katika tabu, kuwa nawe katika tanuri, kuliko kubaki pasipo wewe, hata kama
ingekuwa mbinguni.
Kwangu kuna nini zaidi mbinguni,
nami natamani nini zaidi ya wewe duniani?
Moto unatakasa dhahabu na jaribio la
tabu linatakasa waadilifu.
Humo, Bwana, u pamoja nao; humo
unakaa kati ya wale waliokusanyika kwa jina lako, kama zamani na vijana watatu.
Comments
Post a Comment