MBINGA: WATANZANIA WATAKIWA KUDUMISHA TUNU ZA UMOJA NA AMANI
Watanzania wameshauriwa kudumisha umoja na mshikamano uliopo
ili tunu ya amani iliyopo katika nchi iweze kudumu. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Padre Christian Mhagama wakati akihubiri
katika misa takatifu ya jubilee ya mapadri 11 wa jimbo la Mbinga katika kanisa
kuu la Mtakatifu Kilian jimboni Mbinga.
Padre Christian amesema kuwa,” haitoshi kuimba tu kuwa
Tanzania ni kisiwa cha amani pasipo kuienzi mifumo ya umoja na mshikamano
iliyowekwa na waasisi wetu.” Amesema migogoro iliyopo kati ya wakulima na
wafugaji inaashiria kupoteza tunu hiyo
ya amani na kuiweka Tanzania kuonekana kwa ndani kuwa sio kisiwa cha amani.
Aidha amewataka mapadri
hao kumi na moja {11} kuulinda umoja walioudhamiria kuufuata katika kauli mbiu
yao waliyoichagua wakati walipopata upadri. Amesema mapadri hao katika sherehe yao ya
upadri waliandika maneno “Kwa kuwa mkate
ni mmoja sisi tuliowengi tu mwili mmoja kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya
ule mkate mmoja”
Padri Christian amefafanua kuwa, kauli mbiu hiyo ni ya watu
wote na mataifa yote. Amesema Bwana wetu Yesu Kristo alijihusisha sana na
kuwafanya watu wote wawe pamoja . Kazi yake ilikuwa kubomoa ukuta au utengano
uliopo kati ya watu waliotengana kimila na kidesturi,alibomoa ukuta kati ya
wayahudi na wasamalia na watu wa mataifa
mengine kuwa kitu kimoja. Amesema Yesu aliondoa pia utengano uliokuwepo kati ya
wanaume na wanawake.
Ameelezea kuwa, mapadri hao walifanya vema kuchukua maneno
yenye dhamira ya kuwataka kuwa kitu kimoja, Amesema “idadi hiyo ya mapadri 11 inawakilisha
idadi ya mitume 11, kasoro mmoja ambaye ni Yuda Iskarioti. Amesema kama wangekuwa 12 leo tungemtafuta msaliti”,
Naye naibu waziri wa elimu sayansi na teknolojia , mbunge wa
Nyasa Mheshimiwa Stella Manyanya, akitoa nasaa katia sherehe hizo za jubilei ya mapadre
hao 11 ameitaka jamii kuwaendeleza watoto katika suala la elimu ili kupata
taifa lenye watu wanaokubalika katika jamii yoyote.
Amesema “elimu inasaidia kumtengeneza mtu ili aweze kufanya
kazi kadiri ya wito alionao kwa kuisaidia jamii
na hatimaye kuleta maendeleo yanayokusudiwa.”
Mapadri
waliofanya jubilee zao za miaka 25 ya upadri mwaka huu katika jimbo
katoliki la Mbinga ni Padri Aidan Nchimbi, Padri Amon Nchimbi, Padri
Alfred Komba, Padri Bosco Ndiu, Padri Christopher Mapunda, Padri Filbeth
Mbunda, Padri Joakim Lipanga, Padri Kallo Komba, Padri Mendrad
Nyandindi, Padri Timoth Ndunguru na Padri Thadei Kinyero.
Sister Tuzo Nyoni, Mbinga
Comments
Post a Comment