NINI KIFANYIKE WANANDOA WANAPOSHINDWA KUVUMILIANA?
Nini kifanyike wanandoa wanaposhindwa kabisa
kuvumiliana?
Na Philip Komba,
0754 054 004
Ni kweli, kwamba ndoa iliyofikia mwungano
na mshikamano kwa mujibu wa Sheria ya Kanisa Na. 1141 haiwezi kuvunjwa au kutanguliwa
na mtu yeyote wala na serikali wala na Kanisa isipokuwa na kifo tu. Sheria hii
ya Kanisa Na 1141 inasema wazi kabisa kuwa ndoa iliyothibitishwa au
iliyoidhinishwa na iliyopata ridhaa na kutiliwa sahini na wahusika, na halafu
ndoa hiyo ikakamilishwa kwa tendo la ndoa haiwezi kamwe kutanguliwa kwa uwezo
wowote ule wa binadamu au kwa sababu
iwayo yoyote isipokuwa kifo.
Swali la kujiuliza ni hilo lililo hapo
juu. Nini basi kifanyike pale wanandoa walio katika mwungano usioweza
kutanguliwa wanapofikia kiwango cha juu kabisa cha kushindwa kuvumiliana katika
ndoa yao? Tuseme kwa mfano, mmoja wa wanandoa hawa ameficha silaha chini ya
godoro la kitanda chao na muda wowote ule anaweza kuitumia kumdhuru mwanandoa
mwenzake. Ni sawa kweli, huyu mwanandoa mwenzake asubiri tu hadi hapo hiyo silaha iliyofichwa
itumike kwa kumwua na ndipo ndoa yao ikome kama sheria ya Kanisa Na. 1141
inavyosema?
Ni wazi kabisa, si sawa. Kutokana na
ukweli huu kwamba kufanya hivyo si sawa, Kanisa Katoliki lina njia nyingine ya
kuyashughulikia masuala kama haya. Njia hii ni ile ya kutengua na kamwe si ya
kutangua ndoa kama hizo kwa kuzingatia Sheria
ya Kanisa Katoliki Na.1152. Sheria hii ni ile ya kuwaruhusu wanandoa hawa walio
katika mwungano huu usioweza kutanguliwa, kutengana. Hata hivyo ruhusa hii ya
kutengana kwa kutumia hiyo sheria ya Kanisa, inatolewa kwa shingo upande sana;
na Kanisa Katoliki huitoa hiyo ruhusa baada ya masharti mengi ya kujaribu kutafuta
njia ya kuwafanya wanandoa hawa kusameheana. Kwa mfano, yule anayetakiwa
kumsamehe mwenzake aonyeshe waziwazi kabisa kuwa amemsamehe huyu mwenzake au
anaweza hata kutoa msamaha huo
kimyakimya tu. Kukubali kutoa msamaha kimyakimya ni kukubali kufanya tendo la ndoa naye ingawa
anajua kuwa amefanya hilo tendo la ndoa
na mwingine. Kama hali hii ya kusamehe kimyakimya ikiendelea kwa angalau miezi
sita bila kupelekana kwa wakuu wa Kanisa au wakuu wa Serikali, basi mambo huwa
poa na tatizo huwa limekwisha kwa kufikiriwa kuwa yule aliyekataa kusamehe sasa
amesamehe. Inatakiwa pia yule anayekataa kumsamehe mwenzake, asiwe anatoa mwanya
wa kumwingiza mwanandoa mwenzake katika kishawishi cha kumfanya afanye tendo la
ndoa na mwingine kwa kukataa, kwa mfano, kufanya tendo la ndoa naye bila sababu
za msingi. Inatakiwa pia kwamba yeye mwenyewe huyu asiyetaka kusamehe asiwe anafanya tendo la ndoa na wengine.
Lakini kwa upande mwingine, kama hata baada ya
kipindi hicho cha kutokuwa na uhusiano wa maisha ya pamoja kama wanandoa kupita,
na yule aliyekosewa bado anaendelea kuvuta kamba tu ya kukataa katakata
kumsamehe mwenzake, basi yule aliyekosewa apeleke shauri lake la kutengana kwa
Wakuu wa Kanisa. Wakuu hao wa Kanisa, nao watafanya uchunguzi wa kina wa
mazingira yote yanayohusiana na shauri lenyewe; na bado, hata baada ya kufanya
uchunguzi kama huo, wataendelea kumshauri
yule anayekataa kumsamehe mwanandoa mwenzake abadili msimamo wake, na atoe
msamaha kwa huyu mwenzake na hivyo
utengano ufikie mwisho. Kama hata hilo likishindikana, shauri la kutengana kwa
wanandoa hawa wabatizwa na wenye mwungano wa ndoa ya Kikristo usioweza kutanguliwa, linaweza kumalizwa kwa agizo la Askofu wa
Jimbo au kwa hukumu ya hakimu wa Mahakama ya Kanisa kwa kuzingatia sheria
husika za Kanisa Katoliki.
Kwa kuwa mashauri ya kutengana yanaishia
katika kugawanya mali iliyopatikana wakati wanandoa hawa walipokuwa wanaishi
pamoja, na pia maafikiano kuhusu matunzo na huduma kwa watoto iwapo walikuwa na watoto katika ndoa yao,
Askofu wa Jimbo anaruhusiwa kwa mujibu wa sheria kutoa kibali kwa wanandoa hawa
kupeleka shauri lao kwenye mahakama ya kiraia. Mahakama ya kiraia inayo, kwa
kawaida, vyombo vya dola vya kuhakikisha kuwa mgawanyo wa mali iliyochumwa na
wanandoa hawa kwa kushirikiana, unafanywa itakiwavyo kwa kuzingatia sheria za
nchi na watoto kama wapo wanapata huduma wanayostahili.
Wanandoa wanaofikia hatua hii, ambayo kwa
kweli haipendezi, ya kutengana kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Kanisa
Katoliki, lazima waelewe kuwa ndoa yao inabaki palepale yaani inabaki ndoa
ambayo ni halali na kwa mujibu wa Kanisa Katoliki hakuna anayeruhusiwa kufunga
ndoa nyingine tena kanisani.
Imetayarishwa kwa msaada wa Kitabu cha Sheria za Kanisa: “The Code of
Canon Law: A Text and Commentary”
Mwandishi ni Mhadhiri mstaafu,
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania,
Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment