JIMBO KATOLIKI MBULU:WATAWA 12 WAWEKA NADHIRI ZA DAIMA
Watawa kwa njia ya nadhiri ya usafi kamili, utii na ufukara wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na mitume wa huruma ya Mungu kwa watu wake na kielelezo madhubuti cha ushuhuda wa kinabii. Watawa wanapaswa kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani na upatanisho katika ulimwengu ambamo binadamu anaendelea kuogelea katika dimbwi la vita, mipasuko na misuguano ya kijamii, hali ambayo inaendelea kusababisha hofu na wasi wasi mkubwa kati ya watu. Maisha ya kijumuiya ni kielelezo makini cha umoja na mshikamano wa kidugu unaofumbatwa katika tofauti za mahali anapotoka mtu, kabila, elimu na uwezo wa kifamilia.
Kumbe, maisha ya Kijumuiya yanakuwa kwa namna ya pekee, chemchemi ya furaha, umoja, upendo, udugu na mshikamano katika Kristo Yesu; udugu unaoimarishwa kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, maisha ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika huduma ya kiroho na kimwili; hasa wakati Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Watawa wanapaswa kuwa waaminifu na wabunifu kwa karama za mashirika yao, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati, ili kushirikisha maisha na utume wao katika ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia.
Askofu Isack Amani wa Jimbo Katoliki Moshi, Tanzania ambaye pia ni msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Mbulu, amewataka watawa wa Shirika la Mama wa Mkombozi Jimbo Katoliki la Mbulu walioweka nadhiri zao za daima hivi karibuni, kwenye Kanisa la Bikira Maria Kupalizwa mbinguni kuhakikisha kwamba, wanaziishi na kuzimwilisha nadhiri zao. Wazazi na walezi waendelee kuwasindikiza watoto wao, ili kweli waweze kuwa ni vyombo, mashuhuda na mitume wa huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Mbulu.
Watawa hawa kwa kuwekwa wakfu, wanajifunga daima na Kristo Yesu, mchumba wao kwa maisha yao yote; kwa kujikita katika Sala, Tafakari na Neno la Mungu, Nadhiri na huduma makini, kama chemchemi ya furaha ya maisha ya kuwekwa wakfu ndani ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, palipo na mtawa hapo pana chemchemi ya furaha ya maisha! Watawa wanatakiwa kumwambata Kristo Yesu katika hija ya maisha yao hapa duniani, kwa kuwa waadilifu na mifano bora ya kuigwa na watu wengine ndani ya jamii, ili siku moja waweze kuvikwa taji ya utukufu baada ya hija ya maisha yao hapa duniani.
Utakatifu wa maisha ni jambo linalowezekana ikiwa kama watawa watakita maisha yao katika mambo msingi yanayobainishwa na Mama Kanisa, huku Kristo akiwa ni lengo kuu la maisha yao. Askofu Amani, amewataka watawa walioweka nadhiri zao za daima, kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha kwa kusahau yaliyopita, ili kuganga ya sasa na yale yajayo!
Masista wa Shirika la Mama wa Mkombozi Jimbo Katoliki Mbulu walioweka nadhiri zao za daima ni: Sr. Anunsiata Karoli, Sr. Lucia Dionisi, Sr. Anna Leonce, Sr. Anastasia Valerian, Sr. Magret Paulo, Sr. Restituta Salvatori, Sr. Sylvia Lucas, Sr. Agnes Kanje, Sr Bernedeta Jakobo, Sr. Sekunda Gervas na Sr. Maria Joseph.
Na Sr. Edith Temu.
Jimbo Katoliki Mbulu, Tanzania.
Comments
Post a Comment