MABABA ASKOFU WAASWA
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Julai 2016 wakati akiwa nchini Poland alikutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Poland katika Kanisa kuu la Jimbo kuu la Cracovia. Alitumia nafasi hii kuzungumza na ndugu zake katika Urika wa Uaskofu bila ya uwepo wa vyombo vya habari, ili kushirikishana: furaha, matumaini, changamoto na magumu wanayokabiliana nayo katika dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Poland.
Baba Mtakatifu alizungumzia masuala kadhaa katika maisha na utume wa Kanisa, lakini zaidi kuhusu: Dhana ya ukanimungu; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi Barani Ulaya; Mahusiano bora kati ya Maaskofu na Wakleri wao; Umuhimu wa Parokia katika shughuli za kichungaji. Idhaa ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha kwa muhtasari yale yaliyojiri katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Baraza la Maaskofu Katoliki Poland.
Baba Mtakatifu anasema, changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo ni ukanimungu na tasaufi isiyomwambata na kumweka Mungu, Kristo na Kanisa kuwa ni sehemu ya vipaumbele vyake. Kanisa ni Mama na mwalimu anasema Baba Mtakatifu kwani hapa waamini wanapata maisha mapya yanayofumbatwa katika Neno na Sakramenti za Kanisa. Ili kukabiliana na changamoto ya ukanimungu kuna haja kwa Kanisa kujenga na kukuza utamaduni wa kuwa karibu zaidi na waamini wanaounda Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.
Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa waamini wao kwa: kuwafundisha, kuwaongoza, kuwatakatifuza, na kuwafariji! Maaskofu pia wanapaswa kuwa karibu zaidi na Mapadre wao kwa ni hawa ni wasaidizi wao wa karibu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Huruma na upendo unaooneshwa na Maaskofu kwa Mapadre wao, utaweza kuwafikia waamini huko Maparokiani ambako ndiko kuna Jumuiya kubwa ya waamini.
Kwa uwepo na ukaribu wa Maaskofu kwa watu wao, wataweza kusimama kidete kupambana na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; kwa kuwathamini vijana katika maisha, matumaini na mahangaiko yao pamoja na kuendelea kuwaenzi wazee ambao ni hazina na urithi mkubwa wa Jamii husika katika masuala ya imani, tamaduni na mapokeo.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, ulimwengu mamboleo una kiu na hamu ya haki, amani, upendo na mshikamano, changamoto na mwaliko wa kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu. Huruma ya Mungu ni nguzo na kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Hii ni dhana iliyofanyiwa kazi na Mwenyeheri Paulo VI, ikavaliwa njuga na Yohane Paulo II na sasa inafanyiwa kazi na Papa Francisko katika maisha na utume wake. Wakristo wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha kama njia ya kupambana na Vita kuu ya Tatu ya Dunia inayojikita katika mafao na faida ya watu binafsi: kiuchumi, kisiasa na kitamaduni.
Ulimwengu mamboleo umegubikwa kwa kiasi kikubwa na vita, ukosefu wa misingi ya haki, dhuluma na nyanyaso bila kusahau rushwa na ufisadi ambao umekuwa ni saratani ya watu wengi duniani. Uchu wa fedha, mali na madaraka ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kwani kuna baadhi ya watu anasema Baba Mtakatifu kwa kuwa na fedha wanaweza kununua kila kitu hata kumununua binadamu!
Ndiyo maana biashara ya binadamu na utumwa mamboleo inaendelea kushamiri kwa kasi kubwa sehemu mbali mbali za dunia. Sera na mikakati ya kiuchumi bado inatawaliwa na watu wachache na matokeo yake ni kupamba kwa rushwa na ufisadi, ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana pamoja na athari nyingi za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Vijana wanataka maisha ya mkato ili kukabiliana na changamoto za maisha na matokeo yake ni kuacha masomo hata kabla ya wakati! Hatari kubwa kwa siku za usoni.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, leo hii kuna maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia lakini kuna umati mkubwa wa watu wasiofahamu mafundisho muhimu ya dini zao na matokeo yake ni misimamo mikali ya kidini na kiimani, inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwasaidia waamini wao katika mchakato wa kuimarisha imani kama safari ya maisha ya kiroho; imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Parokia ni mahali muafaka pa Uinjilishaji na ujenzi wa Jumuiya inayo amini, inayoadhimisha Mafumbo ya Kanisa, inayomwilisha Amri za Mungu na Kusali kwa pamoja. Parokia zinapaswa kuendelezwa na kuboreswa zaidi ili ziweze kukidhi mahitaji ya mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa kujikita katika ukarimu, huruma na mapendo na kuwapatia waamini fursa ya kuweza kushirikiana na kushikamana kwa njia ya vyama na mashirika ya kitume, ili kuendelezana kiroho.
Parokia haina mbadala katika maisha na utume wa Kanisa, kwani hapa ni mahali pa ugunduzi na rejea katika maisha na utume wa Kanisa. Parokia iwe ni mahali ambapo waamini wanajisikia kuwa wako nyumbani wakati wa raha na shida; mahali ambapo watu wanathaminiwa, wanasikilizwa na kutekelezewa shida na mahangaiko yao: kiroho na kimwili! Parokia si hoteli ambapo mtu anaingia na kutoka, hapa ni mahali ambapo waamini wanapaswa kujisikia kweli wanakaribishwa na kuthaminiwa na viongozi wao wa kiroho vinginevyo Parokia inaweza kugeuka kuwa ni kituo cha Polisi!
Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya wakimbizi na wahamiaji. Hawa ni watu wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao. Hawa ni watu wanaokimbia vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na biashara haramu ya silaha, kwani kuna baadhi ya wafanyabiashara wanataka kujitajirisha kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia, ndiyo maana si rahisi kusitisha vita kwani migogoro yote hii inafumbata masilahi ya kisiasa na kiuchumi kwa wahusika.
Leo hii bado kuna ukoloni mamboleo unaoendelea kuibuka kwa kasi kiasi kwamba, kuna baadhi ya watu wanataka usawa wa jinsia na ndoa za watu wa jinsia moja; mambo ambayo yanaenezwa kwa kasi kutokana na misaada ya fedha na uchumi kwa nchi changa. Ukarimu na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji uzingatie utamaduni wa nchi husika, uwezo na fursa zilizopo, lakini ukarimu na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni dhamana ya kiutu na kimaadili, hakuna mtu anayeweza kuikwepa! Baba Mtakatifu anasema, hapa kuna haja ya kumwilisha Injili ya huruma, ukaribu, upendo, haki na amani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment