KAMUSI YA UKRISTO YAZINDULIWA
IMEELEZWA
kuwa kuzinduliwa kwa Kamusi ya Ukristo nchini kutasaidia siyo tu uelewa wa
imani na kukua kwa lugha ya Kiswahili, bali pia kutachochea upendo na amani
nchini.
Hayo yameelezwa hivi
karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Utamaduni kutoka Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Lily Beleko wakati akitoa salamu za serikali kwa
niaba ya Waziri wa wizara hiyo, katika uzinduzi wa Kamusi ya Ukristo
uliofanyika katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
“Maneno yakitafsiriwa
visivyo huweza kusababisha chuki na vurugu. Uwepo wa Kamusi hii utarahisisha
uelewa wa imani kwa jamii na kuleta upendo na amani. Wamisionari wa mwanzo
walisaidia kukua kwa Kiswahili kupitia vitabu na machapisho yao mbalimbali. Ni
imani yangu kuwa kamusi hii itachochea kukua kwa lugha ya Kiswahili” ameeleza.
Aidha kupitia hotuba
hiyo, Beleko ameongeza kuwa, ni imani ya serikali kuwa watumiaji wa kamusi hiyo
wataongeza maarifa huku wakiimarisha umoja, amani na uzalendo. Ameeleza kuwa
serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza lugha ya Kiswahili na
utamaduni wake, zinazofanywa na watu na taasisi mbalimbali.
Kwa upande wake
mwandishi wa kamusi hiyo Padri Dkt. Jordan Nyenyembe ametoa wito kwa watanzania
kuenzi utamaduni wa kusoma kwa kuwa unachochea hamu ya kutafuta ukweli na
kuchambua mambo kwa makini.
“Dini zetu zimeletwa
kwa njia ya vitabu, hivyo hatuwezi kukwepa kusoma. Anayesoma vitabu anasali tofauti,
na anafikiri tofauti. Kazi ya uandishi bila ya kuwa na wasomaji wa uhakika
inakua na ukakasi” ameeleza Padri Nyenyembe.
Naye Mkurugenzi wa
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Dkt. Selemani Sewangi amesema kuwa kamusi
hiyo ya kihistoria itasaidia kukidhi matumizi ya istilahi za kanisa ambazo
hazipati maana kusudiwa katika kamusi ya kawaida.
“Kanisa lina msamiati
wake unaopaswa kueleweka vizuri. Kamusi ya kawaida haitoshelezi maana kusudiwa.
Katika uga wa ukristo, kwa mfano neno Mbingu, katika kamusi ya kawaida lina
maana ya anga ya juu, lakini kwa maana ya kikristo bado haijatosheleza. Hivyo
uwepo wa kamusi hii utasaidia kutoa maana halisi za istilahi za kikristo”
ameeleza.
Kazi ya uandishi wa
kamusi hiyo ya ukristo ilianza mwaka 2004 ambapo kupitia gazeti hili la
Kiongozi, Padri Nyanyembe aliandika mfululizo wa makala isemayo ‘Kiswahili cha
wanakanisa’, ambayo ndiyo imezaa wazo la kuwa na kamusi hiyo ya ukristo.
Na: Paschal Mwanache,TEC
Comments
Post a Comment