DUNIA NA KIU YA MSAMAHA


Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi ni tukio ambalo linawakumbusha waamini nia thabiti ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyetamani kuwaona watu wote wakiwa mbinguni baada ya kupata zawadi ya ukombozi, maisha ya uzima wa milele na furaha isiyokuwa na mwisho ambayo imeletwa na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wake! Mbinguni ni kielelezo cha fumbo la upendo wa Mungu unaomuunganisha na binadamu; upendo ambao Mama Kanisa anauungama daima kwa kuonesha ushirikiano na watakatifu wake.
Waamini wanashirikiana imani yao na watakatifu, wenyeheri, ndugu na jamaa ambao wameshuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko! Umoja wa waamini unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo inayowakirimia waamini nguvu ya Roho Mtakatifu. Rehema kamili ambayo Mtakatifu Francisko alikuwa anaiomba kwa Papa Onorio III ilikuwa ni kwa ajili ya kuwapatia waamini maisha ya uzima wa milele kwani alitambua kwamba, nyumbani kwa Baba wa mbinguni kuna makazi ya kutosha na ndiyo maana Yesu alikwenda mbinguni ili kuwaandalia waja wake makao ya uzima wa milele, ili waweze kuishi pamoja naye huko mbinguni!
Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 4 Agosti 2016 alipotembelea Kikanisa cha Porziuncola, mjini Assisi kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa msamaha kama njia inayowawezesha waamini kufika mbinguni. Mazingira ya Kikanisa cha Poriziuncola yanajikita katika dhana ya msamaha, zawadi kubwa ambayo Kristo Yesu amewakirimia waja wake kwa kuwafundisha kusamehe na kusahau. Kumbe, hapa changamoto ni kuhakikisha kwamba, waamini wanakuwa walau na ile nia ya kusamehe, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.
Waamini wajenge utamaduni wa kusamehe kwa kutambua kwamba, kwanza kabisa wao wamesamehewa dhambi zao na Baba wa mbinguni. Kama wao walivyosamehewa na Mwenyezi Mungu, waamini pia wawe na ujasiri wa kuwasamehe wale waliowakosea, ili kuwaonjesha huruma na msamaha, ili kuwa na moyo safi badala ya kujikita katika hasira na kutaka kulipiza kisasi. Yesu amewafundisha wafuasi wake kusamehe katika Sala ya Baba Yetu “utusamehe na sisi kama tunavyowasamehe wale waliotukosea”.
Dhambi ni deni mbele ya Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko wa kukimbilia upendo na huruma ya Mungu katika Sakramenti ya upatanisho, kwani Mwenyezi Mungu yuko tayari daima kusamehe na kusahau pale waamini wanapomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Mwenyezi Mungu anawajalia waja wake upendo, huruma na msamaha kila wakati wanapokimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu ambao haina mipaka na inawafikia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi. Huruma hii inagusa undani wa mtu anayejitambua kuwa ni mdhambi na anataka kumrudia Muumba wake kwa toba na wongofu wa ndani. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu anaangalia moyo wa mwamini anayetaka kutubu na kumwongokea. Lakini, Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, mara nyingi binadamu ni mgumu sana kusamehe na kusahau, wao wanataka huruma kutoka kwa Mungu, lakini kwa jirani zao wanataka haki itendeke: huu si mtindo wa maisha ya Kikristo hata kidogo.
Yesu amewafundisha wafuasi wake kusamehe bila ukomo, kwani upendo na huruma ya Mungu haina mipaka. Wakristo watambue kwamba, wamekirimiwa huruma na upendo pale chini ya Msalaba na sasa ni zamu yao kuwashirikisha jirani zao huruma na upendo huo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba. Mtakatifu Francisko katika Kikanisa cha Porziuncola amekuwa ni chombo na shuhuda wa msamaha, wito na mwaliko wa kuitafuta mbingu. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Msamaha unapata kipaumbele cha pekee kabisa kama chachu ya kulipyaisha Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ulimwengu mamboleo unawahitaji mashuhuda wa huruma ya Mungu na kwamba, hii ni dhamana ambayo kila mtu anawajibika kuitekeleza kwa makini katika hija ya maisha yake. Ulimwengu unahitaji msamaha kwani kuna watu wengi ambao wamejifungia katika undani wa maisha  yao binafsi na huko wanaelemewa na chuki pamoja na uhasama, kwa sababu hawana uwezo wa kusamahe, hali inayoharibu si tu maisha ya mtu binafsi, bali hata na yale ya jirani zake badala ya kutafuta furaha, amani na utulivu wa ndani.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mtakatifu Francisko wa Assisi awaombee ili waweze kuwa wanyenyekevu, alama ya msamaha na chombo cha huruma. Mara baada ya tafakari hii, Baba Mtakatifu aliwaalika Mapadre na Maaskofu waliokuwemo Kanisani humo, kutawanyika sehemu mbali mbali za Kanisa hilo li kutoa Sakramenti ya Upatanisho. Baba Mtakatifu mwenyewe amekuwa wa kwanza kwa kukaa saa moja katika kiti cha maungamo na kubahatika kuwaungamisha waamini 19. Baada ya Ibada hii ya maungamo Baba Mtakatifu alisalimiana na Maaskofu pamoja na Imam wa Mji wa Perugia na mwishoni ametembelea kituo cha Wakleri wagonjwa na wazee ilikuwasalimia na kuwafariji!
Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI