MAADHIMISHO YA SIKU YA VIJANA DUNIANI NI FUNZO


Heri za mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu ndilo Neno la Mungu lililoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Agosti 2016, iliyojikita kwa ufupi kabisa, katika hija yake ya kitume nchini Poland ambamo ameadhimisha Siku ya XXXI ya Vijana Duniani sanjari na kilele cha Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland. Maadhimisho haya anasema Baba Mtakatifu yamefanyika miaka 25 baada ya kuanguka kwa utawala wa "Pazia la Chuma" nchini Poland, hali ambayo ilileta mabadiliko makubwa Barani Ulaya. Siku ya Vijana Duniani imekuwa ni alama ya kinabii nchini Poland, Ulaya na ulimwenguni kote.
Vijana wa kizazi kipya wanaendeleza hija ya maadhimisho haya ambao ni urithi mkubwa uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kama jibu muafaka la kukabiliana na changamoto katika maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya; kwa kuwapatia matumaini yanayofumbatwa katika udugu ili kujenga mahusiano mema kati ya watu walioathirika kwa vita. Hii ni alama ya ukaribu unaofumbatwa katika majadiliano na urafiki wa kweli ili vijana waweze kuwa ni alama ya matumaini yanayojikita katika udugu.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, walengwa wa kwanza katika hija yake ya kitume nchini Poland, walikuwa vijana ambao baadhi yao walikuwepo kwenye  Ukumbi wa mikutano wa Paulo VI mjini Vatican. Hawa ni vijana waliotoka sehemu mbali mbali za dunia, waliokuwa wanakuzunguza lugha tofauti, lakini waliweza kuelewana kwa kutumia lugha ya udugu, ili kujenga na kudumisha madaraja ya udugu. Hawa ni vijana waliokuwa na majeraha ya madonda makubwa mwilini na mioyoni mwao; vijana waliokuwa na maswali, lakini zaidi walikuwa na furaha ya kuweza kukutana na vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kujenga umoja na udugu katika Kristo Yesu, kielelezo makini cha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Haya yalikuwa ni maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vijana wa kizazi kipya, tayari kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na mitume wa huruma ya Mungu kwa watu mbali mbali. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza vijana waliothubutu kwenda Poland kuungana naye kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani bila kuwasahau vijana waliojiunga nao kiroho kwa kuadhimisha Siku hii katika nchi, majimbo na parokia zao. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka msichana Susanna kutoka Roma aliyefariki dunia huko Vienna, akiwa njiani kurejea kutoka Poland. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwafariji wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu Susanna.
Baba Mtakatifu amekumbuka kwa namna ya pekee hija yake kwenye Madhabahu ya Bikira Maria ya Jasna Gora,  mjini Czestochowa, mahali ambapo familia ya Mungu nchini Poland daima imekuwa ikikimbilia ili kuomba ulinzi na tunza kutoka kwa Mama wa Mungu, ili kuitegemeza katika imani na matumaini hata pale inapoanguka, daima Fumbo la Msalaba likiwa mbele ya macho yake. Hapa unaweza kuonja imani, matumaini, busara na hekima; uwiano bora kati ya Mapokeo na upyaisho wa maisha ya kiroho; kati ya kumbu kumbu na matumaini kwa siku za usoni; changamoto ya Poland kama zilivyo nchi nyingine za Ulaya kukita mizizi yake katika tunu msingi za maisha na mwono wa Kikristo, bila kusahau huruma iliyomwilishwa katika matendo na Mtakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina Kowalska, waasisi wa Ibada ya huruma ya Mungu duniani!
Baba Mtakatifu anasema, ametembelea na kusali kwa ukimya katika kambi za mateso na kifo za Auschwitz na Birkenau. Katika hali ya ukimya amesikia roho ya watu waliopitia katika kambi hizi za mateso, akawaombea huruma ya Mungu na kwamba, kuna baadhi ya watakatifu wameweza kuvuka adha hii na leo hii wanaheshimiwa huko mbinguni. Baba Mtakatifu anasema, amesali kwa ajili ya kuombea waathirika wote wa vita, migogoro na mipasuko ya kijami sehemu mbali mbali za dunia. Bado hata katika ulimwengu mamboleo, kuna vita, chuki, uhasama na masikitiko katika maisha, ndiyo maana waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasichoke kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani.
Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wadau mbali mbali waliofanikisha hija yake ya kitume nchini Poland, ili kujenga na kudumisha udugu na amani nchini Poland. Anawashukuru vijana waliojisadaka kwa ajili ya huduma kwa vijana wenzao ili kufanikisha maadhimisho haya pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii vilivyowezesha tukio hili kushuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia.
Baba Mtakatifu anamkumbuka na kumwombea Marehemu Anna Maria ”Bianchini” Jacobin, mwandishi wa habari kutoka Italia aliyefariki ghafla hivi karibuni. Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Mapadre, lakini zaidi wa Maparoko, anapenda kuchukua fursa hii kuwataka vijana, wagonjwa na wanandoa wapya kujitahidi kuishi maisha yao kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kujiachilia na kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili kushuhudia ujasiri na imani ya Kikristo pasi na aibu!
Baba Mtakatifu amehitimisha katekesi yake kwa kusema, Alhamisi tarehe 4 Agosti 2016 atatembelea na kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Malaika na kwenye Kikanisa cha Porziuncola mjini Assisi kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi. Baba Mtakatifu anasema, anakwenda huko kama hujaji wa kawaida, lakini, tukio hili ni muhimu sana katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza katika hija hii ya maisha ya kiroho, wakimwombea mwanga na nguvu ya Roho Mtakatifu pamoja na maombezi ya Mtakatifu Francisko wa Assisi.
 Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI