IMANI HUPONYA MAUMIVU YA NDOA


Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” ni matunda ya umoja na ushirikiano wa urika wa Maaskofu, umwilishaji wa dhana ya Sinodi miongoni mwa watu wa familia ya Mungu pamoja na utekelezaji wa utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Yote haya yamefanyika kwa kujibu maswali dodoso yaliyotolewa na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu wakati wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia kwa mwaka 2014 na Mwaka 2015.
Majibu kutoka sehemu mbali mbali za dunia yaliyogusa watu kutoka katika tamaduni na medani mbali mbali za maisha pamoja na majibu ya Mabaraza ya Maaskofu yalishughulikiwa na hatimaye kukapatikana “Hati ya Kutendea Kazi” “Instrumentum Laboris”. Wajumbe kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu wakashiriki katika kusali, kutafakari na kushirikisha mang’amuzi, fursa, matatizo na changamoto zinazoikabili familia katika utekelezaji wa dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.
Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu aliwataka Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, wanachangia mada mbali mbali katika ukweli na uwazi kwa kuwajibika mbele ya Mungu na Kanisa! Mababa wa Sinodi wakafurahia mchakato wa maadhimisho haya ambayo yamepata sura mpya kabisa pengine, tangu mara baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Vyombo vya upashanaji habari havikukawia kuwagawa Mababa wa Sinodi katika makundi makuu mawili, kundi la kwanza ni lile lilionekana kubaki nyuma kwa kujikita katika Mapokeo ya Kanisa hawa wakaitwa kwa Kiingereza “Conservative”.
Kundi la pili ni lile la Maaskofu “walioendelea” “Progressive” ambalo lilionekana kusoma alama za nyakati kadiri ya mtazamo wa vyombo vya habari, likataka kuchangia mawazo mapya mintarafu changamoto za maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo! Makundi yote mawili yalishirikiana bega kwa bega kuendeleza mchakato wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia kwa kuonesha umoja wa Kanisa unaofumbatwa katika utofauti wenye mvuto, mashiko na upatanisho, daima kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Injili ya familia, inayojikita katika: Utii kwa Neno la Mungu, Mapokeo ya Kanisa pamoja na kusoma alama za nyakati.
Hivi ndivyo Askofu Bruno Forte, aliyekuwa katibu maalum wa Sinodi za Maaskofu kuhusu familia anavyofatakari chemchemi ya Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Upendo ndani ya familia”. Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, wakati wa maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Sinodi za Maaskofu, chombo maalum cha ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro!
Baba Mtakatifu alikaza kusema, katika ulimwengu mamboleo, Kanisa linatakiwa kupenda na kuongoza hata wakati mwingine katika mitafaruku ya kijamii kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linatekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Sinodi za Maaskofu ni kielelezo makini cha umoja na urika wa Maaskofu kwa kushirikiana na Khalifa wa Mtakatifu Petro aliyekabidhiwa dhamana ya kuliongoza Kanisa la Kristo.
Dhana ya Sinodi inaliwezesha Kanisa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kuthamini mchango unaootolewa na wanakanisa mbali mbali, ili kumwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kuwaongoza Watu wa Mungu kwa ufanisi mkubwa zaidi. Dhana ya kusikiliza inalisaidia Kanisa kujifunza kutoka kwa Roho Mtakatifu ambaye ni Roho wa ukweli, ili kuliwezesha Kanisa kutambua kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kulielekeza Kanisa kwa wakati huu!
Huu ni mwelekeo mpya wa utekelezaji wa maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, dhamana ambayo kwa sasa inavaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujikita pia katika majadiliano ya kiekumene anapotekeleza wajibu wake. Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Upendo ndani ya familia” unaonesha uaminifu kwa Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia na hivyo kufungua mwelekeo mpya wa utekelezaji wa mafundisho haya katika shughuli za kichungaji, kwa kuwawajibisha zaidi viongozi wa Kanisa kuwa na mang’amuzi mapana katika utume wa ndoa na familia.
Kimsingi, viongozi wa Kanisa wanahamasishwa kuwapokea wanafamilia wanaoogelea katika shida na magumu ya maisha na kuanza mchakato wa kuwasindikiza! Hapa ndipo kiini cha dhana ya Sinodi kinapojionesha kwa dhati kabisa kadiri ya utenzi wa upendo unavyofundishwa na Mtakatifu Paulo katika Waraka wake kwa Wakorintho. 1 Kor. 13: 4- 7, Sura ya tano inayojikita katika upendo ndani ya familia!
Hapa Kanisa limeonesha ushindi dhidi ya sinodi zilizokuwa zinaendeshwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii, vilivyotaka kudhalilisha Injili ya familia! Kanisa likasimama kidete kuonesha mwelekeo wa imani, mapendo na matumaini na dhamana katika maisha ya ndoa na familia mintarafu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ni mwaliko wa kutafakari dhana ya familia kadiri ya mwanga wa Neno la Mungu, ili kuunda familia inayojikita katika uwelewa wa umoja unaofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Upendo katika maisha ya ndoa na familia si swala na vionjo na hali ya kujisikia tu “Eros”.
Hapa Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu; umoja, ushirikiano na mkamilishano kati ya mwanaume na mwanamke na matunda ya muungano huu ni watoto ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mungu. Hapa Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuonesha moyo wa ukarimu kwa kuwapokea wanandoa, kuwasindikiza, kufanya mang’amuzi, ili hatimaye, kuwashirikisha katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, kuna familia ambazo zimejeruhiwa vibaya sana katika maisha na utume wake.
Wote hawa ni sehemu ya Kanisa la Kristo, wanaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha yao. Ushirikishwaji huu si udhaifu katika maisha ya ndoa na familia, bali ni kielelezo makini cha upendo na huduma kwa wanandoa na familia zao. Changamoto, matatizo na fursa zinazojitokeza katika maisha ya ndoa na familia zinapaswa kushughulikiwa kwa kuwa na mwelekeo chanya, ili kusaidia safari ya utilimifu wa maisha ya ndoa kadiri ya mwanga wa Injili, ili kuwashirikisha na kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, bila kumtenga mtu awaye yote!
Baba Mtakatifu Francisko katika wosia wake wa kitume “Furaha ya Upendo ndani ya familia” anatoa kanuni za jumla: uwajibikaji na mang’amuzi ya mtu binafsi kwa kesi maalum. Hii ni dhamana anayowakabidhi viongozi wa Kanisa, lakini inawajibisha Jumuiya nzima ya waamini, ili kuwa aminifu kwa Mafundisho tanzu ya Kanisa mintarafu ndoa na familia na utamadunisho wa imani.
Ndani ya Kanisa lazima kuwepo na umoja katika Mafundisho tanzu ya Kanisa, lakini pia Kanisa liwe makini kusoma alama za nyakati kwa kutoa suluhu kadiri ya tamaduni na mazingira ya watu husika! Hapa ukweli wa kichungaji hauna budi kuambata huruma ya Mungu. Kanisa lioneshe huruma kwa waamini wanaoogelea katika mahangaiko ya maisha ya ndoa na familia.
Waamini watambue kupenda na kupendwa; upendo uwe ni nguvu inayowaunganisha wapendanao, kwa kuwaimaarisha na kuwatakatifuza kwa neema na baraka kutoka kwa Mungu. Wanandoa waoneshe upendo, huruma na msamaha kwa kupokea changamoto, matatizo na fursa mbali mbali za maisha katika mwanga wa Injili anasema Askofu Bruno Forte katika tafakari yake ya kina kuhusu Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia”.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI