SALA YA PAPA FRANCISKO YA KUIOMBEA AMANI DUNIA
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 30 Julai 2016 alipokuwa anakwenda kwenye mkesha wa maadhimisho ya kufunga Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 alisimama na na kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani dhidi ya vitendo vya kigaidi kwenye Kanisa la Mtakatifu Francisko, mahali ambapo, familia ya Mungu nchini Poland inawaheshimu mashuhuda wa imani kutoka PerĂ¹. Padre Zbigniew Stzalkowski na Michele Tomaszek, waliotangazwa kuwa wenyeheri kunako tarehe 5 Desemba 2015.
Baba Mtakatifu katika sala yake anamwambia Mwenyezi Mungu, kile ulichokiumba ni chema na kizuri; upendo na huruma yako haina kifani kwa wadhambi. Anasema, waamini wanakuja mbele yake ili kuomba tunza na amani duniani, kwa kuwaondolea watu vitisho na vitendo vya kigaidi; ili kujenga na kudumisha miongoni mwa binadamu: urafiki, imani na uwajibikaji wa kusamehe. Baba Mtakatifu amesali na kuwakumbuka wale wote waliofariki dunia kutokana na vitendo vya kigaidi, ili aweze kuwakirimia maisha ya uzima wa milele. Awalinde walimwengu ambao kwa sasa wamechoshwa na vita pamoja na kinzani za kijamii.
Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu, Mfalme wa amani, kuwafariji wale walioathirika kutokana na vita; wale waliomezwa na machafuko na kinzani; awaguse na kuwaponya: kiroho na kimwili; awafariji na kuwapatia nguvu y akuweza kufuta ndani mwao chuki na uhasama pamoja na kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi. Anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuzitembelea na kuzifariji familia ambazo zimeathirika kutokana na vitendo vya kigaidi, ili aweze kuzifunika na joho lake la huruma ya Kimungu pamoja na kujipatia tena nguvu ya kujisikia kuwa ni ndugu na wamoja; kwa kuwasaidia wenye shida na mahangaiko ya maisha, lakini zaidi wakimbizi na wahamiaji, ili kuonesha na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu.
Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kugusa nyo za magaidi, ili waweze kutambua ubaya wavitendo vyao, ili hatimaye, waweze kurejea tena katika amani, wema, heshima ya maisha na utu wa binadamu wote bila kujali dini, mahali anapotoka, utajiri au umaskini wake. Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kusikiliza sala yao katika huruma wakati huu ulimwengu unapoonesha hali ya kukata tamaa. Waamini wanamkimbilia Mungu kwa imani na matumaini makubwa katika huruma na upendo wake, kwa kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza la Bikira Maria aliyewakirimia ujasiri wafiadini kutoka PerĂ¹ yaani Zbigniew na Michele walioshuhudia Injili kiasi hata cha kumwaga damu yao; wanawaomba ili kuombea zawadi ya amani pamoja na kuwaondolea madonda ya vitendo vya kigaidi.
VATICAN
Comments
Post a Comment