UJUMBE WA BABA MTAKATIFU PAPA FRANSISKO MAADHIMISHO YA 50 YA SIKU YA MAWASILIANO DUNIANI
UJUMBE WA BABA MTAKATIFU PAPA FRANSISKO MAADHIMISHO YA 50 YA SIKU YA
MAWASILIANO DUNIANI
Mawasiliano na Huruma: Makutano yenye Tija
Wapendwa dada na kaka zangu,
Mwaka
Mtakatifu wa Huruma unatualika sote kwa pamoja kutafakari uhusiano uliopo
baina ya mawasiliano na huruma. Kanisa,
katika umoja na Kristo, aliye umwiliko hai wa Baba wa huruma, linakumbushwa
kutekeleza huruma kama tofauti bainishi ya uwepo wake na kwa kila kitu
litendalo. Kile tunachokisema na jinsi tunavyokisema, kila neno na tendo letu linapaswa
kuwa kielelezo cha huruma, ukarimu na msamaha wa Mungu kwa wote. Upendo, kwa
asili yake, ni mawasiliano; na huongoza kwenye uwazi na ushirikiano. Kama mioyo
na matendo yanaongozwa na upendo wa Mungu, basi mawasiliano yetu yatakuwa
yameguswa na nguvu za Mungu mwenyewe.
Kama
watoto wa Mungu, tunakumbushwa kuwasiliana na kila mtu, pasipo kubagua.
Kimsingi, maneno na matendo ya Kanisa yanalenga kufikisha huruma, kugusa mioyo
ya watu na kuisaidia katika safari ya kuelekea ukamilifu wa maisha ambao Yesu Kristo
alitumwa na Baba kuuleta kwa wote. Hii inamaanisha kwamba sisi wenyewe lazima
tuwe tayari kulikubali joto la Mama Kanisa na kuwagawia wengine joto hilo, ili
Yesu ajulikane na apendwe. Joto hilo ndilo linalolipatia neno la imani maana
yake; kwa mahubiri yetu na ushuhuda, na kutoa cheche ambazo huwapatia watu
uhai.
Mawasiliano
yana nguvu ya kujenga madaraja, kuwezesha kukutana na kushirikishwa, na hivyo
kuimarisha jamii. Hupendeza kiasi gani pindi watu wakichagua maneno yao na
matendo kwa uangalifu, katika jitihada za kuepusha kutokuelewana, kutibu
kumbukumbu za majeraha na kujenga amani na maelewano. Maneno yanaweza kujenga
madaraja kati ya watu binafsi na katika familia, makundi ya kijamii na watu.
Hii inawezekana katika dunia ya vitu na dunia ya utandawazi. Maneno na matendo
yetu lazima yaweze kutusaidia sote kukwepa hali isiyokatika ya kuhukumu na
kulipiza kisasi ambavyo huendelea kuwanasa watu binafsi na mataifa, ikihimiza
hisia za chuki. Maneno ya wakristo yanapaswa kuwa faraja ya kudumu katika kujenga
ushirika, hata katika matukio ambapo ni lazima kuulaani uovu bila hofu, ili
kamwe yasijaribu kuvunja mahusiano na mawasiliano.
Kwa
sababu hiyo, nawaalika watu wote wenye mapenzi mema kuivumbua upya nguvu ya
huruma inayoponya mahusiano yaliyojeruhiwa na kuleta amani na maelewano kwa
familia na jamii mbalimbali. Sisi sote tunajua ni namna gani majeraha ya zamani
na chuki vinavyoweza kuwanasa watu na kuweka kizingiti katika njia ya
mawasiliano na maridhiano. Hali hii inajidhihirisha pia katika mahusiano baina
ya watu. Katika kila tukio, huruma inaweza kuanzisha aina mpya ya hotuba na
mijadala. Shakespeare aliongea kwa ufasaha aliposema; “Ubora wa huruma
hautetereshwi. Unashuka kama mvua mwanana toka mbinguni mpaka chini ardhini.
Imebarikiwa mara mbili: inambariki inayeitoa na yeye anayeipokea” (Mabepari wa Venisi 4,I).
Lugha
yetu ya kisiasa na kidiplomasia ingeboreka kama ingesukumwa na huruma, ambayo
kamwe haikosi tumaini. Natoa rai kwa wenye majukumu ya kitaasisi na kisiasa, na
wale wenye jukumu la kuunda maoni ya umma, kuweka tahadhari katika namna
wanavyoongea dhidi ya wale wanaofikiri au kutenda tofauti nao au wale ambao
watakuwa wametenda makosa. Ni rahisi kushawishika kutumia hali hizo na kuwasha
moto wa kutokuaminiana, hofu na chuki. Badala yake, ujasiri unahitajika
kuwaongoza watu kuelekea kwenye mchakato wa maridhiano. Ni ujasiri wa ubunifu
chanya ambao hutoa suluhu ya ukweli kwa migogoro ya zamani na fursa ya
kujenga amani ya kudumu. “Heri
wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu.” (Mt 5:7-9).
Jinsi
ninavyotamani namna yetu ya kuwasiliana, pia huduma yetu kama wachungaji wa
Kanisa isiwe kamwe ya kiburi na kujivuna dhidi ya adui, au kuwatafsiri vibaya
wale ambao dunia inawachukulia kuwa wapotevu na kuwapuuzia. Huruma yaweza
kusaidia kupunguza mikasa ya maisha na kutoa joto kwa wale waliojua ubaridi tu
wa hukumu. Namna yetu ya kuwasiliana isaidie kuondokana na fikra
zinazowatenganisha wadhambi na wenye haki. Tunaweza na lazima tuhukumu hali za
dhambi - kama vile ukatili, rushwa na unyonyaji - lakini hatuwezi kuhukumu
watu, kwani ni Mungu pekee anayeweza kuona undani wa mioyo yao. Ni kazi yetu
kuwaonya wale wenye kufanya makosa kuupinga uovu na udhalimu kwa namna fulani,
kwa ajili ya kuwaacha huru waathirika na kuwanyanyua wale walioanguka. Injili ya
Yohane inatuambia kuwa “ukweli utawaweka huru”(Yn 8:32). Ukweli muhimu zaidi ni
Yesu mwenyewe, ambaye ukarimu wake wa huruma ni kipimo cha kupimia namna
tunavyoonyesha wazi ukweli na kuupinga udhalimu. Kazi yetu kuu ni kuunga mkono
ukweli kwa upendo (rej. Eph 4:15). Maneno pekee yanayosemwa kwa upendo na
kwenda sambamba na ukarimu na huruma yanaweza kugusa mioyo yetu yenye dhambi.
Maneno, matendo na misimamo mikali ya kimaadili inahatarisha kuwatenga zaidi
wale tunaotamani kuwaongoza kwenye uongofu na uhuru, kwa kuzifanya hisia zao
ziwe za kukataa na kujihami.
Baadhi hufikiri kuwa maono ya jamii iliyo na
mizizi yake katika huruma hayana maana. Lakini hebu tujaribu na tukumbuke
uzoefu wetu wa kwanza wa mahusiano, ndani ya familia zetu. Wazazi wetu walitupenda
na kututhamini kwa jinsi tulivyo zaidi kuliko kujali uwezo na mafanikio yetu.
Wazazi kwa asili hutaka mafanikio kwa watoto wao, lakini upendo huo kamwe
hautegemei watoto kutimiza masharti fulani. Nyumba ya familia ni mahali ambapo
muda wote tunakaribishwa (rej.Lk 15:11-32). Nataka kumhamasisha kila mtu kuiona
jamii siyo kama jukwaa ambapo wageni hushindana na kujaribu kuibuka washindi,
bali kama nyumbani au familia, ambapo mlango upo wazi muda wote na kila mtu
anajisikia kukaribishwa.
Ili
jambo lipate kutokea,ni lazima kwanza tusikilize.Kuwasiliana kunamaanisha
kushirikishana, na kushirikishana kunahitaji kusikiliza na kupokea. Kusikiliza
ni zaidi ya kusikia. Kusikia ni kupokea taarifa, wakati kusikiliza ni
kuwasiliana ambako kunadai ukaribu. Kusikiliza huturuhusu kuelewa kwa usahihi,
na siyo kuwa watazamaji tu au watumiaji. Kusikiliza pia kunamaanisha kuwa tayari kushirikishana maswali na mashaka, kusafiri sambamba,
kukomesha madai yote ya mamlaka ya kiimla na kuweka uwezo wetu na vipawa katika
huduma ya manufaa ya wote.
Kusikiliza
siyo rahisi. Mara nyingi ni rahisi kujifanya viziwi. Kusikiliza humaanisha kuwa
na umakini, kutaka kuelewa, kuthamini, kuheshimu anachosema mtu mwingine.
Huhusisha aina ya kifodini au kujitoa sadaka, tukijaribu kumuiga Musa mbele ya
kichaka kinachoteketea: inabidi tuvue viatu vyetu tunaposimama “ mahali
patakatifu” katika kukutana kwetu na yule aongeaye name (rej.Kut 3:5).Kujua
jinsi ya kusikiliza ni neema kubwa, ni zawadi tunayotakiwa kuiomba na kufanya
kila juhudi kuitekeleza.
Barua
pepe, ujumbe mfupi, mitandao ya kijamii na kuchati vyaweza pia kuwa mbinu
kamili za mawasiliano ya wanadamu. Siyo teknolojia inayoamua kama mawasiliano
ni sahihi ama siyo, bali moyo wa mwanadamu na uwezo wetu wa kutumia kwa busara
mbinu tulizonazo. Mitandao ya kijamii yaweza kuwezesha mahusiano na kutangaza
mazuri ya jamii, lakini pia yanaweza kusababisha ubaguzi na mtengano kati ya
watu binafsi na makundi. Dunia ya kisasa ni duara la wazi, eneo la kukutana
ambapo twaweza kuhamasisha ama kutenganisha, kushiriki katika mijadala yenye
mantiki ama mashambulizi yasiyo na usawa. Nasali ili Jubilei hii, tukiishi kwa
huruma, “itufungue zaidi kuwa na bidii katika mazungumzano ili tuweze kujuana
na kuelewana vizuri zaidi; na iweze kuondoa namna zozote za fikra zilizofungwa
na zisizo na nidhamu, na kuondoa kila namna ya ukatili na ubaguzi” (Misericordiae
Vultus, “Uso wa Huruma”, 23). Mtandao wa intaneti waweza kutusaidia
kuwa raia wema. Upatikanaji wa mitandao ya kisasa unahusu wajibu kwa jirani
yetu ambaye hatumwoni, ambaye lakini ni mtu halisi na mwenye hadhi ya utu
ambayo ni lazima iheshimiwe. Mtandao wa intaneti waweza kutumika kiungwana
kujenga jamii yenye afya na iliyo wazi katika kushirikishana.
Mawasiliano, popote na kwa namna yoyote
yanapofanyika, yamefungua upeo mpana zaidi kwa watu wengi. Hii ni zawadi ya
Mungu inayodai uwajibikaji mkubwa. Napenda kurejea kwenye hii nguvu ya
mawasiliano kama “ukaribu”. Kutano kati ya mawasiliano na huruma litazaa
matunda endapo litaleta ukaribu unaojali, kufariji, kutibu, kusaidia na
kusherehekea. Katika dunia iliyomeguka vipande vipande, kuwasiliana kwa huruma
humaanisha kusaidia kutengeneza ukaribu wenye nguvu, huru na undugu zaidi kati
ya watoto wa Mungu na dada na kaka zetu wote
katika familia moja ya kibinadamu.
Kutoka Vatikani, 24 Januari 2016
Comments
Post a Comment