PAPA FRANSISKO AONYA
Baba Mtakatifu Francisko akiwahutubia mahujaji na wageni katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 7 Agosti 2016, alionya dhidi ya tabia ya kushikamana na mali na fedha akisema , wakati wa kifo yote hubaki hapa dunia, haijalishi kama una mali nyingi au fedha , maana sanda halina mifuko ya kubeba mali. Papa aliasa wakati akitafakari kifungu cha Injili ya Luka 12.32-48, ambamo Yesu aliwazungumzia wanafunzi wake juu ya itakavyokuwa siku ya mwisho ya kukutana nae. Kukutana kunakopaswa kuwa kichochea na msukumo kwa mtu kuishi kwa wema. Yesu aliwahimiza wanafunzi wake kusaidia wengine na kujiwekea akiba katika mfuko usiochakaa, yaani kujiwekea hazina salama mbinguni ambako hakuna Mwizi wala nondo wa kuitafuta.
Papa alisisitiza kwamba huu ni mwaliko wa thamani wa majitoleo ya sadaka katika kazi za matendo ya huruma na sio kuweka tumaini katika mambo ya kidunia yanayopita kwa kasi kama upepo . Ni mwaliko wa kujinasua na ubinafsi, na kuishi kwa mujibu wa mantiki ya Mungu, kutoa kipaumbele kwa wengine, ni mantiki upendo. Na inawezekana kuishi hivyo bila kushikamana na fedha, maana hata kama tungekuwa na mali nyingi na fedha nyingi, saa ya mwisho ya maisha ikifika, hatuwezi kuvichukuahuko tuendako baada ya maisha ya kidunia. Papa alieleza na kukumbusha kwamba, "sanda hana mifuko."
Kwa hiyo akasema , mifano mifupi mitatu iliyotolewa na Yesu katika fungu hili la Injili: kuweka akiba mbinguni; Watumishi waangalifu ; na mtumishi aminifu na asiye aminifu , ni somo juu ya usimamizi wa mali, ambamo tunaonywa kwamba , ni muhimu: kuangalia na kuwa macho na aminifu katika maisha. Alinukuu"Heri watumishi wale ambao Bwana wao atakaporudi atawakuwa wako tayari”. Papa alitafakari aya hizo akisema , zinaonyesha furaha ya kusubiri katika imani Bwana , katika mtazamo wa huduma, na hasa huduma kwa maskini. Papa alieleza na kuomba msaada wa Ulinzi wa kimama wa Bikira Maria.
Na baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Papa akisalimia makundi mbalimbali, aliutumia muda huo kutoa ombi lake kwa mara nyingine kwa ajili ya wahanga wa machafuko ya Kisiasa nchini Syria akiomba amani . Alionyesha kujali kwamba, taarifa mbaya zinaendelea kusikika tokea Syria jinsi raia wanvyoathirika na vita na hasa katika eneo la Aleppo. Alikemea dhuluma hizo akisema kuwa haikubaliki kwamba watu wanyonge wakiwemo watoto wengi wanafanywa kuwa sadaka ya machafuko yanayofanywa na watu wenye roho ngumu . Kafara hao wanatamani amani itawale miongoni mwao lakini wananyiwa haki hiyo na kundi dogo la watu wenye mabavu. Kwa maneno hayo alitoa mwaliko kwa watu wote.kupitia sala kushikamana na raia wema wa Syria, wake kwa waume , na aliyakabidhi yote chini ya Ulinzi wa Kimama wawa Mama Maria. Aliwasihi wote kukaa kimya kwa muda mfupi na kisha wakasali sala ya Salaam Maria.
Comments
Post a Comment