PANAMA,MWENYEJI SIKU YA VIJANA DUNIANI 2019
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Cracovia Jumapili tarehe 31 Julai 2016 kama sehemu ya maadhimisho ya kufunga rasmi maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016, kabla ya kusali Sala ya Malaika wa Bwana na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, aliwashukuru wadau mbali mbali waliojisadaka kwa ajili ya kuandaa na hatimaye kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Anawashukuru na kuwapongeza vijana walionesha na kushuhudia furaha na imani yao Jimboni Cracovia. Hawa ni vijana ambao wamemfurahisha sana Mtakatifu Yohane Paulo II huko mbinguni na kwamba, atawasaidia kupeleka Injili ya furaha kwa watu wa mataifa! Maadhimisho haya yamewawezesha vijana kuonja uzuri wa udugu katika Kristo kiini cha matumaini yao katika maisha. Wamesikiliza kwa makini sauti ya Kristo mchungaji mwema, wakaona na kuonja mwanga, msamaha na neema zake. Vijana wameonja uzuri wa maisha ya sala, chachu ya maboresho ya maisha ya kiroho, ili kuishi na kutembea katika huruma ya Mungu wanaporejea nchini na katika Jumuiya zao!
Baba Mtakatifu amewaonesha Picha ya Bikira Maria iliyoheshimiwa sana na Mtakatifu Yohane Paulo II, picha ambayo imehifadhiwa kwenye Madhabahu ya Calvaria. Bikira Maria anawafunda vijana jinsi ya kumwilisha mambo mazuri waliyojipatia huko Poland, ili waweze kuyatunza nyoyoni mwao na hatimaye, kuzaa matunda kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kila mmoja wao kadiri ya uwezo na nafasi yake anatakiwa kuwa ni shuhuda wa Kristo katika medani mbali mbali za maisha.
Baba Mtakatifu anasema, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyoanzishwa kunako mwaka 1985 na Mtakatifu Yohane Paulo II yanaendelea kushika kasi na baada ya maadhimisho ya Siku ya Vijana kwa ngazi ya Kijimbo katika kipindi cha miaka miwili, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yatafanyika kunako mwaka 2019 huko nchini Panama. Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu katoliki kutoka Panama wametoa baraka zao kwa ajili ya maandalizi ya maadhimisho haya.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment