INJILI YA FAMILIA



Kongamano la kichungaji Jimbo kuu la Roma lililozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na litakalohitimishwa hapo tarehe 19 Septemba 2016, imekuwa ni fursa kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma kufanya tafakari ya kina mintarafu Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris letitia” ambao kwa sasa ni dir ana mwongozo wa Kanisa katika utume wa familia, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kubadilika na kuambata huruma na upendo wa Mungu kwa familia zinazojikuta katika shida, magumu na changamoto za maisha!
Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu kuzungumza na wajumbe wa Kongamano la Kikanisa Jimbo kuu la Roma, anasema, familia ya Mungu inaitwa kwa namna ya pekee kuishi, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia kwa ari na moyo mkuu licha ya: matatizo, changamoto na fursa zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa familia. Lengo ni kutoa majibu muafaka kwa wito na utume wa maisha ya Kikristo, kwa kusoma alama za nyakati, ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kutekeleza kwa kina na mapana utume wa familia katika ulimwengu mamboleo.
Kardinali Vallini anakaza kusema, kati ya changamoto kubwa katika maisha ya ndoa na familia kwa nyakati hizi ni ni uaminifu na udumifu wa upendo wa dhati ndani ya familia; mambo ambayo yalichambuliwa na Mababa wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia na matunda ya maadhimisho haya ni Wosia wa kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia”, uliochapishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko.
Huu ni mwongozi na dira kwa viongozi wa Kanisa, lakini pia ni Wosia mahususi kwa wanandoa na familia kwani wao wanaguswa moja kwa moja na mashauri yaliyomo kwenye Wosia huu wa kitume. Kumbe, Mama Kanisa anawahamasisha wanandoa kujitaabisha kusoma na kutafakari Wosia huu, tayari kuufanyia kazi kama sehemu ya majiundo yao endelevu katika maisha ya ndoa na familia, tayari kukabiliana na chagamoto za maisha kwa imani na matumaini thabiti!
Baba Mtakatifu anawahamasisha viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajifunga kibwebe ili kusaidia familia za Kikristo katika maisha na utume wake, ili waamini watambue na kuthamini umuhimu wa ndoa na familia ya Kikristo, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia unaojikita katika Injili ya familia na maisha. Hapa Kanisa linakazia mafundisho yake tanzu pamoja na kuambata huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu anayetubu na kumwongokea.
Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, analitaka Kanisa kuwa karibu na familia ambazo kwa kiasi kikubwa zinaogelea katika dimbwi la mahangaiko na hali ya kukata tamaa pale ambapo waamini bado wanataabika kujenga mahusiano yao katika furaha na amani ya ndani. Baba Mtakatifu katika Wosia huu wa kitume anagusa undani wa maisha ya ndoa na familia katika ukweli wake mpana hata kama ukweli unauma si tu kwa jamii mamboleo hata kwa Kanisa lenyewe.
Ndiyo maana Jimbo kuu la Roma katika sera na mikakati yake, linaendeleza mchakato wa tafakari ya kina, ili kuibua sera makini na madhubuti za utume wa familia, kwa kuishirikisha mihimili yote ya Uinjilishaji katika hija ya upyaisho wa maisha ya ndoa na familia; toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na mwelekeo mpya kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia. Lengo ni kuwawezesha waamini kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho, kiutu na kitume kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo anasema Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma.

 Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI