"WANYONGE WAPEWE KIPAUMBELE" ASKOFU KASSALA
Na Sarah Pelaji, Dar es Salaam
SERIKALI na taasisi za kidini
zisipomgusa mnyonge zina ubaridi na kasoro katika utendaji wake.
Askofu
wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala
ametoa rai hiyo wakati akifafanua juu ya kikundi cha watu nchini Marekani kilivyotaka
kuharibu sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni pamoja na kuzungumzia suala
la Mama Thereza wa Kalkuta kutangazwa Mtakatifu Septemba mwaka huu.
“Huo ni mmomonyoko wa maadili na kukosa imani ya hali ya juu kwa
kumdhihaki Mama Mtakatifu. Jitihada zifanyike kuwazuia vijana wetu wasiingie
katika uanachama wa kuabudu shetani.” Amesisitiza
Askofu Kassala ameeleza kuwa, Si nchini Marekani tu ambapo
baadhi ya watu wanajaribu kuchafua Sherehe ya Bikira Maria bali hata baadhi ya
wananchi nchini Italia wamekosa mwelekeo wa kiimani kwa kugeuza sherehe za Bikira
Maria kuwa sherehe za kutatapanya mali kwa kufunga kipindi cha kiangazi na
kujiandaa na kipindi cha baridi.
“Sherehe ya Bikira Maria katika mazingira ya Italia inachukuliwa
katika sehemu mbili, kwanza ni sherehe ya Kanisa pili ni sherehe ya mazingira
ya kidunia.
Huwa wanasherehekea mazingira yao ya kufunga kipindi cha joto
kwa kufanya sherehe kubwa za kutapanya mali na kufanya kila aina ya starehe.
Huwa wanawapeleka wazee kwenye nyumba za kutunzia wazee ili
wapate nafasi ya kustarehe na kutapanya mali ili baada ya hapo wakusanye kwa
ajili ya kipindi kingine cha joto kinachoanza Juni mpaka August.
Hivyo ukiangalia hawa ni kinyume na maisha ya Mama Thereza
kwamba wanatumia mali kwa kumtenga maskini na wasiojiweza. Mama Thereza
alitumia muda na nguvu zake kuwasaidia masikini.
Aligusa maisha ya mnyonge ambaye amekosa matumaini. Ndio maana
anaenda kutangazwa Mtakatifu kwa maisha yake ya kumfanya mnyonge kujisikia huru
na binadamu mwenye furaha na matumaini.”
Ameiasa serikali kugusa maisha ya mnyonge kwa kumuinua kutoka
majalalani, kukaa barabarani na kumpeleka katika mazingira bora. Isimuinue mtu
ambaye tayari ameshainuka bali imuinue yule ambaye anatamani kuinuka lakini
hana uwezo.
“Kiongozi bora anagusa maisha ya watu, anajibu changamoto za
watu wake hususani wasiojiweza na masikini. Kanisa kadhalika lisiwe baridi
kujibu changamoto za waamini wake ambao wanahitaji faraja na kupata matumaini
kupitia kwake”.
Askofu Kassala anaongeza. “Kiongozi bora ni yule anayesoma alama
za nyakati. Haishi kwa kushika kanuni tu bali analinganisha kanuni na mazingira
ya watu wake. Kanisa pia lisome ishara za nyakati kwa kutafsiri kanuni na
changamoto za sasa ili waamini wake wasiweke kasoro na maswali mengi dhidi
yake. Kumbe utendaji ni uleule lakini kwa mfumo tofauti,”
Mwito wake kwa jamii ni kuzingatia maadili na kufanya mambo ya
msingi yanayomuinua mwingine badala ya kumkandamiza.
“Wengi wetu tunaweza kuwa Mama Thereza kama tunafanya kazi kama
inavyopaswa kwa furaha na matumaini, kumuangalia aliyeko dhaifu miongoni mwetu
na kumtetea pale anapokandamizwa”.
“ Ukiangalia utendaji wa serikali utaona ubinafsi katika baadhi
ya watendaji. Wanafunzi wanaketi chini hakuna madawati, watu wanakufa kwa kiu
bila maji, njaa na mengine lakini kila mwaka bajeti inapitishwa. Je, bajeti
hiyo ni kwa ajili ya nani? Serikali ijipange kuwainua wanyonge ambao wanahitaji
nguvu yake ili wainuke badala ya kuinua wale ambao tayari wameshainuka.” Amesisitiza.
Hivi karibuni Baba Mtakatifu Fransisko wakati wa Malaika wa
Bwana mjini Vatikani amesema kuwa, Kanisa halihitaji kuwa na utendaji wenye
urasimu kutumikia kwa upendo na huruma katika kujali mahitaji ya
watu hasa waliosahaulika pembezoni katika umaskini na upweke.
Papa alionya kwamba, waamini wa Kanisa bila kuwa na mioyo
iliyojaa huruma na upendo , kuna hatari kwa Kanisa kuwa baridi katika utendaji
wake.
Alitaja ubaridi huo au imani ya uvuguuvugu tu, maana yake
, ni kuwa na utendaji usioonyesha dhahiri utambulisho wa Kanisa
katika maisha ya kijamii.
Ifahamike kuwa, huko Marekani katika mji wa Oklahoma, Maaskofu
wa Kanisa Katoliki waliwaasa waamini duniani kusali sala maalumukupinga ibada
ya mashetani iliyokuwa imepangwa na wanachama wake ili kumkejeli Bikira Maria
siku ya Sherehe ya Kupalizwa kwake Mbinguni August 15 mwaka huu.
Kufuru hiyo dhidi ya Bikira Maria ilipangwa ifanyike katika mji
huo huku wafuasi wa kikundi hicho wakiwa wameshika sanamu ya Bikira Maria wakiidhihaki.
Askofu Mkuu wa Oklahoma Mhashamu
Paul Coakley aliitisha sala maalumu ili kuungana na waamini kusali kama
familia kuzuia jambo hilo ovu.
Hata hivyo alilaumu serikali za mitaa kushindwa kuzuia ama
kushughulikia nia ya kufanya dhihaka hiyo.
Comments
Post a Comment